Home » » MJUMBE ATAKA KATIBA ITAMKE UMRI WA MTOTO, KIJANA,MZEE

MJUMBE ATAKA KATIBA ITAMKE UMRI WA MTOTO, KIJANA,MZEE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Siti Abasi Ally, amesema ni lazima katiba mpya itamke umri wa mtoto, kijana na mzee ili kuwezesha wanajamii wote kupata haki za msingi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, alisema sura ya haki za binadamu imeeleza haki za watoto, lakini umri wa mtoto haujaelezwa, huku sheria ikieleza mtoto ni tangu kuzaliwa hadi kufikisha miaka 18.

“Ni lazima rasimu itamke umri wa mtoto, haki na wajibu wa mtoto na mambo ya kumshirikisha na iwekwe wazi mtoto ashirikishwe kwa mambo yanayomhusu, umri wa mzee na kijana utajwe. Wapo watakaosema kijana ni hadi miaka 60, lakini ukweli siyo hivyo. Katiba itamke,”  alisema.

Alisema katika kamati hiyo wamependekeza umri wa mtoto ni miaka 18, kijana asizidi miaka 40 na mzee ni kuanzia miaka hiyo kuendelea, tunataka kuondoa utata uliopo kwa sasa wapo wazee wanajitahidi vijana na watoto wakiolewa katika umri mdogo kutokana na ukinzani wa sheria.

Kuhusu haki za wafungwa, alisema limeleta mvutano kwenye kamati yao kwa kuwa mfungwa mwanamke mwenye mimba akijifungua akiwa gerezani ni lazima kuwe na usalama wa mtoto ikiwamo kutunzwa vizuri ili asiathiriwe na mazingira ya gerezani.

“Mfungwa mjamzito apate haki ya kwenda kliniki na kupata lishe nzuri kwa kuwa katika hali ya ujauzito mwanamke hapendi kula... tumeangalia kwa kina na kuhakikisha haki za wafungwa hasa wanawake wajawazito,” alisema.

Siti, ambaye pia ni kutoka Jumuiya ya Wanawake Wanasheria Zanzibar, alisema changamoto kubwa kwa Zanzibar ni wanaume kutelekeza watoto na kuoa mke mwingine na ndiyo maana wanataka baba na mama kuwa na wajibu wa kutunza watoto wanapotengana.

Alibainisha kuwa kuna uzalilishaji wa kijinsia katika maeneo mengi, ikiwamo sehemu za kazi, ambako watumishi wengi ni wanaume na kwamba, ni lazima katiba itamke kila nafasi ya uongozi kuwe na usawa wa kijinsia.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa