Home » » SITTA AWACHOKONOA VIONGOZI WA DINI

SITTA AWACHOKONOA VIONGOZI WA DINI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, amewachokoza viongozi wa dini nchini kwa kuwataka waumini wa madhehebu mbalimbali kupuuza nyaraka zinatolewa na viongozi hao kwa madai kuwa baadhi ya nyaraka hizo hazina utukufu wowote wa Mwenyezi Mungu.
Alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati wa kipindi cha matangazo huku akiwatambulisha na kuwakaribisha bungeni wageni 13 wa Mjumbe wa Bunge Maalum ya Katiba (BMK), Fortunata Moses Kabeja, ambao ni waumini wa Kanisa Katoliki kutoka Jumuiya ya Mtaa wa Image, Kanisa Kuu la Mt. Paulo wa Msalaba, Dodoma.

“Nawaombeni waumini wa makanisani, muwe wangaalifu sana na nyaraka zinazosomwa siku hizi kwenu, baadhi ya nyaraka hazina utukufu wowote wa Mwenyezi Mungu,” alisema Sitta.

Alisema baadhi ya nyaraka zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa madhehebu nchini siyo nzuri na hazina utukufu wowote wa Mungu, hivyo waumini wanapaswa kuwa waangalifu na kuzipuuza.

Hata hivyo, wakati Sitta akiwataka waumini wa madhehebu mbalimbali kupuunza maagizo ya viongozi wao, BMK jana lililazimika kuwatumia viongozi hao hao wa dini, ambao ni wajumbe wa Bunge hilo kutuliza hasira za baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu ambao walitishia kukwamisha Rasimu ya Katiba inayopendekezwa baada ya suala la Mahakama ya Kadhi kugonga ukuta kwenye rasimu.

Viongozi ambao jana walilazimika kusimama bungeni kwa zaidi ya nusu saa kwa ajili ya kuwaweka sawa waumini wao ni pamoja na Sheikh Hamid Masoud Jongo, Sheikh Thabit Jongo na Askofu Dornald Mtetemelwa.

Sitta ametoa kauli hiyo, takriban mwezi mmoja tu tangu Jukwaa la Wakristo Tanzania litoe tamko kuhusu mchakato wa Katiba wakitaka Bunge hilo lisitishwe kwa kuwa limepuuza maoni ya wananchi.

Wajumbe wa Jukwaa la Wakristo Tanzania, waliokutana Agosti 27 na 28, 2014, jijini Dar es Salaam, waliipongeza iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakieleza kuwa ilikusanya maoni ya wananchi wengi bila kujali dini zao, upande wa Muungano walikotoka, hali zao za kimaisha, jinsia na kabila.

Jukwaa hilo lilieleza kuwa Tume iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, ilifanya kazi kizalendo na kwamba waliandaa rasimu kwa kuzingatia maslahi mapana ya wananchi lakini katika hali isiyotarajiwa, Bunge limeyapuuza.

Tamko hilo lilieleza kuwa wajumbe wa iliyokuwa tume ya Jaji Warioba waliheshimu viapo hivyo walifanya kazi kwa uaminifu na uadilifu na kwamba hawakushawishiwa au kupokea rushwa kutoka kwa kundi, dini au chama chochote cha siasa wakati wa zoezi hilo.

Aidha, Jukwaa hilo lilisema baada ya Tume kuwasilisha Rasimu kwenye Bunge Maalum la Katiba, Taifa likaanza kushuhudia ‘uasi wote na uovu wa wanadamu wapingao kweli kwa uovu’ kwa kutoweka maslahi ya wananchi mbele.

Jukwaa hilo linaloundwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste (CPCT), Wasabato (SDA) na Jumuiya ya Kikristo (CCT), lilisema BMK, limekuwa likiendesha vikao vyake huku likiwapotosha wananchi kwa makusudi.

“Matumizi ya ubabe na wingi wa Wabunge wa Chama Tawala (CCM), badala ya Kanuni za Bunge na maridhiano, kumefanya mchakato wa Katiba kuhodhiwa na Chama Tawala dhidi ya maslahi ya wananchi,” ilisema sehemu ya tamko hilo.

Ilieleza pia kuwa mijadala katika BMK imekuwa ya kejeli, matusi, vitisho, ubabe na kupuuza hata kupotosha maoni yaliyotolewa na wananchi kwa Tume, jambo ambalo limeshusha hadhi ya bunge na kufanya wananchi walipuuze na kumtaka Rais Jakaya Kikwete, aliahirishe ili kuruhusu majadiliano na maridhiano.

Hivi karibuni, kumekuwapo taarifa za kusambazwa kwa waraka unaowataka viongozi wa Kanisa Katoliki nchini, pamoja na mambo mengine, kuorodhesha majina ya mapadri wasiokipenda CCM, ili wanachama wao wasiende kusali huko, waraka unaodaiwa kusambazwa kwenye Bunge Maalum la Katiba na Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Cyril Chami.

AWASIFIA ADC
Katika hatua nyingine, Sitta aliwasifia na kuwapigia debe kwenye baadhi ya majimbo viongozi ambao walijitoa katika Chama cha Wananchi (CUF) na kujiunga na Chama kipya cha Alliance for Democratic Party (ADC).

Sitta jana alisikika akiwasifia viongozi hao wakati akiwatambulisha ndani ya BMK walikokwenda kwa mwaliko wa Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid.

Viongozi wa ADC waliotembelea BMK jana na kutambulishwa na Sitta ni Mwenyekiti, Said Miraji, ambaye Sitta alimsifia kuwa aliwahi kuwa Kampeni Meneja wa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, kwenye mbio zake za urais mwaka 2010.

Aidha, Sitta alisema kuwa Miraji pia aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Idara mbalimbali za CUF kwa zaidi ya miaka 15 na kusema lakini amechoka kuendelea kuwa CUF na kuamua kwenda ADC.

Kiongozi mwingine aliyesifiwa na Sitta jana bungeni ni Adela Stella Mkilindi, Makamu Mwenyekiti wa ADC kwa upande wa Tanzania Bara.
Alisema kuwa Adela aliwahi kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kuanzia mwaka 1995 ambaye pia ameamua kuachana na CUF na kwenda ADC ambako alidai kuwa huko kuna mfumo mpya ambao una mfumo fulani unaotetemesha huko CUF walikotoka.

Akiendelea na utambulisho wake, Sitta alimtaja Faki Khamis Lima, Makamu Mwenyekiti wa ADC Zanzibar kuwa na yeye alikuwa ‘kigogo’ huko CUF, akimsifia kuwa aliwahi kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la CUF kwa zaidi ya miaka 15.

Wengine waliotajwa na Sitta ni Musa Mangale, aliyedai kwamba aliwahi kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Segerea kwa tiketi ya CUF, Shoka Hamis Juma aliyesema kuwa alikuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa muda mrefu kupitia CUF katika jimbo la Micheweni kwa vipindi vitatu na kuwa pia alikuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF huku akidai kuwa kwa taarifa alizonazo ni kwamba Mangale anajiandaa tena kuliteka Jimbo la Micheweni.

  Sitta aliendelea kuwataja Lydia Bendera, Katibu Mkuu wa ADC aliyewahi kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Kibaha kwa tiketi ya CUF mwaka 2010.

“Jamani tuangalie hawa jamaa wamejipanga vizuri sana, mchanganyiko wao unatoa fursa kwa viongozi kwa akina mama wanawake kuanzia ngazi ya taifa, ” alisema Sitta.

Hamad Rashid Mohamed, aliyekuwa mwenyeji wa viongozi hao wa ADC, amekuwa akihusishwa na chama hicho baada ya kuvuliwa uanachama wa CUF kwa madai ya kuasi chama hicho, hivyo kuitwa Mbunge wa Mahakama.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa