Home » » TURUFU YA RASIMU YA SITTA HII HAPA

TURUFU YA RASIMU YA SITTA HII HAPA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

RASIMU ya tatu ya Katiba maarufu kama Rasimu ya Sitta ambayo leo inaanza kupigiwa kura imejikita katika kutetea mahitaji na maslahi mahususi ya makundi makubwa ya jamii ili ikubalike kirahisi.
Rasimu hiyo ya Sitta imebeba na kutetea maslahi ya kundi la wanawake, ambao ni zaidi ya asilimia 50 ya wananchi, vijana ambao ni zaidi ya asilimia 70 na nguvu kazi ya taifa na makundi makubwa ya uzalishaji ya wafanyakazi, wakulima, wafugaji, wavuvi na wachimbaji wadogo.
Katika rasimu hiyo iliyowasilishwa bungeni mapema wiki iliyopita, imetetea wanawake, kwa kutamka bayana haki na mahitaji ambayo hayakutamkwa katika rasimu zilizopita kuliko Rasimu ya Pili ya Katiba, iliyopewa jina la Rasimu ya Warioba.
Wanawake na madaraka
Moja ya haki iliyotamkwa ya wanawake, ni uwakilishi wa uwiano ulio sawa na wanaume katika vyombo vya kufanya uamuzi ambapo sasa katika majimbo ya uchaguzi, atachaguliwa mtu mwanamume na mtu mwanamke.
Katika Ibara iliyotengwa mahususi kwa ajili ya haki za wanawake iliyokuwa katika Rasimu ya Warioba, Rasimu ya Sitta imeifanyia marekebisho kwa kutamka bayana baadhi ya haki ambazo zilikuwa ‘zimefichwa’.
Kwa mfano wakati Rasimu ya Warioba katika Ibara ya 47, ibara ndogo ya kwanza (a) imesema; “ kila mwanamke ana haki ya kuheshimiwa utu wake,” Rasimu ya Sitta ilienda mbele zaidi ya hapo. Katika rasimu hiyo ya Sitta Ibara ya 54 (a), imeandikwa; “Kila mwanamke ana haki ya kuheshimiwa, kuthaminiwa na kutambuliwa utu wake.”
Ibara ya 47, Ibara ndogo ya kwanza (b), Rasimu ya Warioba imetamka kuwa; “kila mwanamke ana haki ya kuwa salama dhidi ya unyonyaji na ukatili.”
Sehemu (e) Rasimu ya Warioba imeeleza; “kila mwanamke ana haki ya kulindwa dhidi ya ubaguzi, uonevu na mila zenye madhara”. Kwa upande wa Rasimu ya Sitta, ilienda mbele zaidi ya hapo.
Rasimu hiyo ya Sitta katika ibara ya 54 (b) imesema; “Kila mwanamke ana haki ya kulindwa dhidi ya ubaguzi, udhalilishaji, dhuluma, unyanyasaji, ukatili wa kijinsia na mila potofu.”
Katika huduma za afya, Rasimu ya Warioba imetamka kuwa kila mwanamke ana haki ya kupata huduma bora ya afya, lakini Rasimu ya Sitta imeenda mbali zaidi na kutamka kwamba kila mwanamke, ana haki ya kupata huduma bora za afya, ikiwemo afya ya uzazi salama.
Haki za kiuchumi
Moja ya mambo yaliyofurahiwa na wanawake wengi bungeni, ni kitendo cha Rasimu ya Sitta katika Ibara ya 22, ibara ndogo ya pili (d), kutamka “kila mwanamke atakuwa na haki ya kupata, kumiliki, kuendeleza na kusimamia ardhi kwa masharti yale yale kama ilivyo kwa mwanamume.”
Haki hiyo haikuwepo katika Rasimu ya Warioba ingawa tayari imesababisha malalamiko kutoka kwa baadhi ya wajumbe, wakidai inakiuka sheria za dini.
Fursa kwa vijana
Kwa upande wa vijana, tofauti kubwa ya Rasimu ya Sitta kuingiza Bunge kutunga sheria itakayosimamia uanzishwaji, muundo, majukumu na uendeshwaji wa Baraza la Vijana la Taifa, ambalo halikuwepo katika Ibara ya 44 ya Rasimu ya Warioba, iliyozungumzia haki za vijana.
Katika fursa na haki za vijana, zimezingatiwa pia katika haki za wafanyakazi, ambapo pamoja na mambo mengine, Rasimu ya Sitta imeongeza Ibara ya 44, Ibara ndogo ya kwanza (e) ambapo mfanyakazi amepewa haki ya, “kupata hifadhi ya afya na usalama wake katika sehemu za kazi.”
Katika haki ya kumiliki mali, Rasimu ya Sitta imeongeza kipengele cha haki ya kulipwa fidia, ambayo haikuwepo katika Rasimu ya Warioba. Haki hiyo ya kulipwa fidia imefurahiwa zaidi na wazalishaji wanaotumia zaidi ardhi; yaani wakulima, wafugaji na wachimbaji wadogo wa madini.
Katika Ibara ya 45, Ibara ndogo ya pili imeandikwa “…itakuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kunyang’anywa mali yake, kwa madhumuni ya kuitaifisha au madhumuni mengine, bila ya idhini ya sheria, ambayo imeweka masharti ya kutoa fidia, inayolingana na thamani halisi.”
Haki ya elimu Katika haki ya kupata elimu, Rasimu ya Sitta iliongeza Ibara ya kuiwajibisha Serikali katika kutoa huduma kwa wananchi ambayo ni ibara ya 49, Ibara ndogo ya 4.
Ibara hiyo inasema; “Serikali itahakikisha kuwepo kwa mfumo wa elimu unaozingatia uwezo na mahitaji ya taifa”.
Hata hivyo, wajumbe wa kamati karibu zote 12 za Bunge Maalumu la Katiba, walitaka neno elimu ya msingi na sekondari bure, liwekwe kwenye Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa, na suala hilo linasubiriwa katika Rasimu itakayopigiwa kura leo baada ya marekebisho.
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa