Home » » BUNGE LA KATIBA:MSHITUKO

BUNGE LA KATIBA:MSHITUKO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Kura za hapana zaiibua kamati ya mashauriano

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Ali Seif Iddi, (kushoto) na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho (wapili kushoto), wakijadiliana jambo nyeti na wajumbe wenzao wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Zanzibar, wakati zoezi la upigaji kura wa katiba lilipokuwa likiendelea kwa siku ya pili jana.Picha/ Khalfan Said

Uamuzi wa baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kupiga kura ya hapana kwa ibara zote za rasimu mpya ya katiba inayopendekezwa imeibua mkanganyiko na sasa Kamati ya Mashauriano imeundwa kukutana na waliopiga kura hizo.

Juzi wajumbe walianza kupiga kura kupitisha sura na ibara moja baada ya nyingine, kwa wazi au siri, huku wengi wakisema kuwa wanaunga mkono, lakini pia wakiwamo wachache waliosema hapana kwa sura zote 10 na ibara zote kuanzia ya kwanza hadi ya 157.

Jana Mwenyekiti wa Bunge hilo, alitaja kamati hiyo kuwa inaundwa na Makamu Mwenyekiti wa BMK, Samiah Hassan Suluhu, Rashid Mtuta, Shamsi Vuai Nahodha, Omari Yusuph Mzee, Andrew Chenge, Asha-Rose Migiro, Dk. Francis Michael, Brigedia Jenerali Mstaafu Hassan Ngwilizi na Mohammed Aboud.

Bunge hilo limefikia hatua ya kupiga kura ambayo ni nyeti zaidi kwani zitahitajika theluthi mbili kutoka kila upande wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ili kufanikisha upitishwaji wa rasimu hiyo.

Kulingana na mahudhurio yaliyokuwako juzi kabla ya kuanza kwa kazi ya upigaji kura, wajumbe kutoka Tanzania Bara walikuwa 295, huku kutoka Zanzibar wakiwa ni 142.
Kulingana na hesabu hizo, zitahitajika kura 140 kutoka Zanzibar na kura 280 kutoka Tanzania Bara ili kupitisha ibara hizo. 

Kwa mahudhurio ya juzi, Zanzibar ilikuwa na wajumbe wawili zaidi ya idadi ya theluthi mbili inayohitajika huku bara kukiwa na wajumbe 15 zaidi ya theluthi mbili ya kura zinazohitajika.

Hata hivyo, siyo wajumbe wote walipiga kura za ndiyo na hata waliopiga za ndiyo wapo waliokataa baadhi ya ibara. Walikuwapo waliokataa huku wengine wakipiga kura za siri, ambazo haijulikani waliamua nini.

  Hali hii inatafsiriwa kama juhudi za kusaka theluthi mbili ya kura za wajumbe kutoka Zanzibar, kwa ajili yakupitisha Rasimu hiyo.

Mwenyekiti wa Bunge hilo juzi alisema kwa kuzingatia idadi ya wabunge waliokuwamo bungeni kwa wakati huo, upande wa Zanzibar ulikuwa na wajumbe wawili tu wanaozidi idadi ya inayotakiwa kupata theluthi mbili, hivyo akawaomba wote wapige kura ya ndiyo ili kutimiza matakwa ya kisheria.

Hata hivyo, zoezi la kupiga kura lilipoanza, wabunge saba kutoka Zanzibar walipiga kura ya wazi ya hapana, huku wengine zaidi ya 20 wakipiga kura ya siri.
Hali hiyo imelifanya BMK kushtuka kutokana na kuwapo kwa dalili ya kukosekana kwa theluthi mbili ya kura za ndiyo kutoka Zanzibar, hivyo kuufanya uongozi wa Bunge hilo kuanza kuhangaika kuweka ‘mambo sawa’.

Kamati ya mashauriano iliundwa kwa ajili ya kuwasikiliza wajumbe waliopiga kura ya hapana dhidi ya rasimu nzima.

Akizungumza saa 5:50 wakati wa kipindi cha Matangazo jana, Mwenyekiti wa BMK, alisema kuwa uongozi umeshtushwa na uamuzi wa wajumbe hao kupiga kura ya hapana kwa rasimu nzima huku wakiwa wametumia muda mwingi kuijadili jambo ambalo siyo la kawaida.

Alisema kuwa kutokana na hali hiyo, ameamua kuunda Kamati ya Mashauriano kwa ajili ya kuwasikiliza, huku akidai kuwa wajumbe wawili kati ya waliopiga kura ya kuipinga rasimu hiyo waliomba kusikilizwa.

Alisema kuwa kanuni ya 54, kanuni ndogo ya nne inasema kwamba ‘Mwenyekiti baada ya kushauriana na Kamati ya Uongozi anaweza kuunda kamati ya mashauriano pale anapoona linajitokeza suala linalohitaji mashauriano’.

“Nina suala mbele yangu linalohitaji mashauriano kutokana na baadhi ya wabunge wenzetu ambao jana (juzi) walipiga kura ya hapana kwa ibara zote kitu ambacho si cha kawaida kwa sababu haiwezekani kuwa hivyo,” alisema Mwenyekiti huyo.

 “Tunaomba Kamati hii ifanye kazi leo (jana) na sisi tutapokea matokeo baadaye na kuyaleta ndani ya Bunge hili kwa wakati unaofaa,” alieleza Mwenyekiti huyo. 

Alisema kuwa ingawa wajumbe wawili kati ya waliokataa Rasimu hiyo juzi walimuomba kusikilizwa pia milango ya kamati hiyo itakuwa wazi hata kwa wajumbe wengine ambao hawajaomba ili ieleweke kwanini wakae wakati walikaa kipindi chote bungeni kisha waikatae rasimu yote.

Baadhi ya wajumbe wa BMK waliozungumza na NIPASHE jana mjini Dodoma walielezea kutoridhishwa na hatua hiyo, wakiamini kanuni ililenga kuundwa kwa kamati wakati wa vipindi vingine vya uhai wa BMK, lakini siyo katika kipindi hiki cha upigaji kura.

Walisema kuwa kitendo cha kuundwa kamati hiyo katika kipindi cha kupiga kura, wanakitafsiri kuwa ni kuingilia uhuru wao wa kufanya maamuzi.

Dk. Alley Nassoro, alisema yeye siyo miongoni mwa walioelezwa na Mwenyekiti wa BMK, kuwa wameomba kusikilizwa na kwamba hajutii kupiga kura ya hapana kwa rasimu yote kwa sababu ana amini ndiyo msimamo halisi alionao juu ya kazi yote aliyofanya tangu BMK lilipoanza.

“Sababu zangu kuu ni mbili tu ambazo zimesababisha nipige kura ya hapana, ya kwanza ni imani na uzawa wangu; nikimaanisha dini ya kiislamu kunyimwa haki ya Mahakama ya Kadhi kutambuliwa na kuheshimiwa kikatiba lakini ya pili ni maslahi ya nchi yangu  Zanzibar, kutozingatiwa na Katiba hii kwa kiwango cha kukidhi matarajio yangu,” alisema Dk. Alley.

Alisema hata ahadi iliyotolewa bungeni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati wa mijadala ya kuboresha Rasimu hiyo ya Katiba inayopendekezwa, kwamba Mahakama ya Kadhi itatungiwa sheria haafikiani nayo kwa sababu siyo mara ya kwanza kwa serikali kutoa ahadi juu ya jambo hilo.

Alisema kwamba hata ikitungwa sheria ya aina hiyo, utekelezaji wake unaweza usifanyike kwa sababu utategemea zaidi uongozi utakaokuwa madarakani tofauti na kama haki hiyo ingewekwa kwenye Katiba ambayo ndiyo sheria mama.

“Hii Katiba inayopendekezwa kwa jinsi ilivyowekwa ni dhahiri hata kama ikitungwa sheria ya kuanzisha Mahakama ya Kadhi, utekelezaji wake utakuwa mgumu kwa sababu baadhi ya watu wanachukulia baadhi ya masharti katika imani yetu kuwa ni yenye chembe za kibaguzi hususan katika umiliki wa mali baina ya mwanamke na mwanaume,” alieleza Dk. Aley.

Suala la kupata theluthi mbili ya kura za upande wa Zanzibar linakuwa tete kutokana na wabunge wa Chama cha Wananchi, CUF pamoja na wale wa kundi la 201 ambao waliungana na kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kuondoka bungeni, hali inayosababisha idadi ya wajumbe waliobaki kupata wakati mugumu kutimiza matakwa ya kisheria ya kuhakikisha Rasimu hiyo inapitishwa na theluthi mbili ya kura za wajumbe wote kutoka katika kila nchi washirika.

CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa