Home » » CHADEMA YATANGAZA KIAMA KWA WASALITI

CHADEMA YATANGAZA KIAMA KWA WASALITI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Dodoma, Jella Mambo
UONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mkoa waDodoma umetangaza kiama kwa wanachama mamluki ambao wamekuwa wakitumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa ajili ya kusababisha migogoro ndani ya chama hicho.
Mbali ya kutangaziwa kiama, pia wanachama ambao wanaonekana kuwa vibaraka kutoka CCM wametakiwa kuondoka wenyewe au wakibainika watafukuzwa bila kujali cheo.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Dodoma, Jella Mambo, alipokuwa akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari ofisini kwake juu ya aliyekuwa Katibu wa CHADEMA jimbo la Mtera, John Lubote kujiunga na CCM.
Jella, alisema kuondoka kwa Lubote na kujiunga CCM kumesaidia sana kutokana na mwanachama huyo kuwa mamluki wa siku nyingi na kushiriki mara kadhaa kukihujumu chama.
Aidha, kiongozi huyo alisema kuwa kamati ya ulinzi na usalama wa Chama hicho, tayari walishabaini kuwa Lubote ni kati ya wanachama ambao wanatumiwa na makada wa CCM kwa ajili ya kutaka kuvuruga CHADEMA kwa maslahi yake binafsi.
“Lubote amesoma alama za nyakati kutokana na unafiki, umamluki na kutokuwa na msimamo, CHADEMA Mkoa ilikuwa inafanya uangalizi wa mwisho ili kuweza kumwajibisha kwa mujibu, kanuni na sheria…
“Kujiengua kwake hakututishi hata kidogo, amejua kuwa kwa sasa hakuwa na sifa na kilichomtisha zaidi ni pale ambapo aliona vijana wengi wenye sifa ya kugombea nafasi ya ubunge wakijitokeza kutangaza nia ya kugombea Mtera…

“CHADEMA ni chama makini sana, tumekuwa tukifuatilia nyendo zake mara kwa mara, amekuwa ni mtu ambaye alihusika sana katika kuhujumu chama na kusababisha kukosekana kwa ushindi katika uchaguzi mdogo wa madiwani Kata ya Mpwayungu…
“Muda mwingi alikuwa akinywa pombe wakati wa kampeini huku akiambatana na makada wa CCM, jambo ambalo pia lilisababisha chama Jimbo la Mtera kulega lega…
“Mbaya zaidi katika uchaguzi wa ngazi za matawi, Lubote alishindwa kusimamia uchaguzi kwa hiyo kutokana na waraka wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Lubote anakosa sifa ya kuwa mgombea wa nafasi yoyote na hadi anajiuzuru ama anajiondoa CDM hakuwa na cheo chochote ndani ya Wilaya au kata,” alielezea Jella.
Alipotafutwa Lobote kwa ajili ya kuelezea ni kwanini amefanya uamuzi wa kujiunga na CCM, pamoja na mambo mengine alisema kuwa viongozi wa CCM wamemuahidi kumpandisha ndege na kuzunguka naye nchi nzima.
“Ndugu mwandishi hapa mimi nipo nakunywa bia ile mbaya, kwa taarifa yako nimeamua kuachana na CHADEMA, nimetumika muda mrefu lakini kwa sasa CCM wameisha nipatia kitengo maalum nitakuwa nazunguka na ndege nchi nzima kwa ajili ya kutoa elimu juu ya Demokrasia, uzuri wa Katiba iliyopendekezwa, umuhimu kuwa na Baraza la Vijana pamoja na haki za akina mama…
“Kwa taarifa yako mimi nitakuwa meneja mkuu wa benki mpya inayofunguliwa hapo Uhindini ya Equity bank na nimeishajaza mikataba kila kitu, hivyo kwa sasa maisha yangu yanaelekea kunyooka,” alisema na kuongeza.
Unajua kwa sasa lazima uangalie maslahi yako yakoje, siwezi kuendelea kutumikia CHADEMA ambapo sipati kitu chochote nazidi kuwa masikini lakini CCM ndo mambo yote kiongozi.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa