Home » » KURA YA MAONI KABLA YA UCHAGUZI HAIWEZEKANI

KURA YA MAONI KABLA YA UCHAGUZI HAIWEZEKANI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema hakuna uwezekano wa kura ya maoni kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na NIPASHE, Jaji Warioba alisema ameona taarifa inayoeleza kuwa kura ya maoni inatarajiwa kufanyika Machi, mwakani.
Hata hivyo, alisema kama kuna umakini kura hiyo haitawezekana kufanyika.

“Kura ya maoni inaendeshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec). Katika mchakato wa katiba, kulikuwa na awamu mbalimbali. Ya kwanza ni Tume ya Mabadiliko ya Katiba kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa rasimu. Ya pili, Bunge Maalumu kujadili rasimu na kutoa katiba inayopendekezwa. Kazi hizi zimekamilika. Awamu ya tatu ni wananchi kupiga kura ya maoni,” alisema Jaji Warioba.

Alisema awamu mbili za kwanza zilitekelezwa chini ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo ilitoa utaratibu wake na kwamba, kura ya maoni itaongozwa na Sheria ya Kura ya Maoni.

Jaji Warioba alisema sheria hiyo imeweka utaratibu wake na kwamba, suala hilo ni muhimu, hivyo ni vyema ukafuatwa utaratibu uliowekwa na sheria husika.
Alisema sheria hiyo imeeleza baada ya katiba inayopendekezwa kukabidhiwa kwa Rais katika muda wa wiki mbili, itachapishwa katika Gazeti la Serikali na kuiagiza kuanza mchakato.

MCHAKATO UKOJE?
Jaji Warioba alisema kwa mujibu wa mchakato huo, baada ya siku saba tangu Rais kuipa Nec kazi ya kuanza mchakato, itatunga swali, ambalo litajibiwa na wapigakura.
Alisema hatua hiyo itafuatiwa na elimu kwa umma, ambayo itaendeshwa na Nec kwa kushirikiana na asasi za kiraia, ambayo inatakiwa kutolewa kwa muda usiopungua miezi miwili na baadaye Nec kutangaza utaratibu wa kampeni.

“Sheria ile inasema zitaundwa kamati mbili kitaifa na kwenye majimbo. Moja itakuwa ya kuunga mkono katiba inayopendekezwa na nyingine ya kupinga. Hizo kamati ndizo zitaendesha kampeni kwa muda wa mwezi mmoja…huu ndiyo utaratibu wa Sheria ya Kura ya Maoni,” alisema Jaji Warioba.

Jaji Warioba alisema Nec haiwezi kuanza mchakato huo mpaka imalize kuandaa daftari la wapigakura.

“Mpaka sasa tunavyozungumza, Nec haijaanza kuandikisha wapigakura. Navyosikia itaanza kuandikisha mwakani. Na wenyewe walivyosema labda watamaliza mwezi Aprili au Mei. Lakini kwa vyovyote vile wasianze mchakato huo mpaka wamemaliza kuandikisha wapigakura,” alisema Jaji Warioba.

Aliongeza: “Katika mazingira haya, sioni kama kura ya maoni tunaweza kuamua itakuwa lini. Na hasa ukichukulia shughuli za Nec. Uchaguzi wa serikali za mitaa ni Desemba, hivyo katika kipindi hiki, Tume itashughulikia mambo ya uchaguzi wa serikali za mitaa. Haiwezi kufanya kazi nyingine kwa ufanisi, bali muda wake utumike kuandaa na kuendesha uchaguzi huo.”

Alisema kwa mazingira hayo, inategemewa itaanza kuandikisha wapigakura baada ya kumalizika uchaguzi huo na kwamba, hata ikianza Januari na Februari, mwakani, ikimaliza lazima kuwapo na kipindi cha kutosha kwa elimu kwa umma.

“Haiwezekani mwezi wa tatu kuwa na kura ya maoni. Kwa vyovyote hata ingekuwa hivyo, mwezi huo siyo mzuri wa kupiga kura. Ni wakati wa mvua. Wananchi wanashughulika na mashamba yao. Kwa kawaida upigaji kura unapangwa ili wananchi wapate nafasi. Ukiwapangia kipindi cha mvua, wana shughuli nyingi. Itakuwa vigumu kwa wananchi wote kushiriki. Kwa hali tuliyonayo, lazima tuangalie sheria, ifanyiwe marekebisho ili shughuli zote, hasa elimu kwa umma ipate nafasi ya kutosha,” alisema Jaji Warioba.

Alisema ni vizuri serikali ikafanya jitihada kubwa ya kusambaza katiba inayopendekezwa ili wananchi wapate nafasi.
Jaji Warioba alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipewa miezi 18 na kuongezewa miwili, BMK lilipewa siku 70 na kuongeza siku 70 na nyongeza ya siku 20 na lilitumia mara mbili ya muda uliotengwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

“Kwa wananchi ni muhimu zaidi kupata nafasi. Tusilifanye jambo hilo kwa kulipua. Ni jambo zito. Wananchi lazima wapewe nafasi ya kutosha kuelewa nini wanakipigia kura,” alisema Jaji Warioba.

Alisema hata kama ni mapema, ifanyike Juni au Julai, mwaka 2015, muda ambao maandalizi yamekamilika na wananchi hawana shughuli za shamba.

“Lakini tujue mwakani ni uchaguzi mkuu. Ukiwa na mlolongo wa uchaguzi, Desemba, Juni na Oktoba, lazima wananchi watachoka,” alisema Jaji Warioba.
Katiba inayopendekezwa ilikabidhiwa Oktoba 4, mwaka huu, baada ya BMK kumaliza kazi yake.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa