Home » » SAFARI YA UKAWA ILIVYOANZIA DODOMA

SAFARI YA UKAWA ILIVYOANZIA DODOMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Siku moja kabla ya kuanza kikao cha Bunge Maalumu la Katiba, usiku wa kuamkia Aprili 16, mwaka huu baadhi ya wajumbe walikuwa wameafikiana kugoma.
Kulikuwa na ‘chemba’ kadhaa usiku huo kwa baadhi ya wajumbe kukutana na kuweka mkakati wa kususia Bunge. Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ndiye aliyepewa kazi ya kupiga zumari.
Siku hiyo, saa 4.31 asubuhi, Profesa Lipumba alifanya kazi hiyo na kuhitimisha uchangiaji wake akisema: “Ukawa hatuwezi kuendelea kushiriki dhuluma dhidi ya wananchi kwa kupitisha Katiba ambayo ni kinyume cha matakwa yao.”
Baada ya kauli hiyo, alikusanya makabrasha yake na kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge akifuatiwa na Mwenyekiti wa Ukawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia na wajumbe wengine. Ukimya ulitawala takriban kwa dakika mbili hivi na baada ya wajumbe hao kutoka, Makamu Mwenyekiti wa lililokuwa Bunge Maalumu, Samia Suluhu Hassan aliwaelekeza makatibu kuhesabu wajumbe ili kuona kama akidi imetimia ili waendelee na kikao.
Baadaye aliliambia Bunge kuwa makatibu walimweleza hawahitaji akidi kwa kuwa akidi ilitimia mwanzoni kabla ya Ukawa kutoka.
Hotuba ya Lipumba
Profesa Lipumba alianza kwa kunukuu Gazeti la Mwananchi la Aprili 14, mwaka huu katika sehemu inayosema; “Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), ameanza kampeni kanisani kwa kuwataka wananchi kupinga serikali tatu zilizopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, vinginevyo nchi itatawaliwa na jeshi kwa kuwa serikali ya muungano itashindwa kuwalipa mishahara wanajeshi.”
“Hii ni kauli ya Waziri Lukuvi ndani ya Kanisa la Methodist wakati wa sherehe ya kumsimika Mchungaji Joseph Bundala kuwa Askofu na Waziri Lukuvi alikuwa anamwakilisha Waziri Mkuu.”
Alisema inasikitisha kwa sababu kauli hiyo inafanana na ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa wakati akihutubia Bunge Maalumu.
Profesa Lipumba alisema kauli za Lukuvi zinatisha baada ya kusema Wazanzibari ambao wanataka kuwa na nchi yao hawawezi kujitegemea, bali wanataka wapate nafasi ya kujitangazia kuwa ni nchi ya Kiislamu.
“Waziri anaweza kusema hivyo ndani ya kanisa? Kawahamasisha mpaka yule kiongozi wa kanisa akasema ili kudumisha Muungano, bora Katiba ya Zanzibar ifutwe ili iwepo moja ya nchi moja ambayo inadumisha Muungano,” alisema.
Alisema Lukuvi alikuwa akiwaaminisha kuwa mfumo wa serikali tatu ukipita kutakuwa na mapinduzi na nchi haitatawalika na hivyo watu watashindwa kwenda kusali kanisani.
“Kama ndugu zetu wa Zanzibar wangekuwa wanahitaji serikali moja, tungekuwa na utaratibu mzuri tu, lakini siyo wanachama wa CUF, siyo wa CCM, Wazanzibari wote hawataki muungano wa serikali moja,” alisema.
Alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa mapendekezo ya serikali tatu kutokana na ukweli huo. “Hoja zilizoletwa hapa ni hoja za serikali moja, si hoja za serikali mbili lakini wenzetu moja hawataki, kwa hiyo tunahitaji Muungano ambao tutakuwa na maridhiano ya pande zote mbili.
“Wengi wamenukuu makala niliyoitoa katika Kituo cha TCD (Kituo cha Demokrasia Tanzania), ambayo iliunda Baraza la Katiba na mimi nilichambua mapendekezo ya Tume nikasema kwa mapendekezo yaliyomo ndani ya Rasimu ya Katiba hayatakidhi mapato ya shirikisho.” Alisema wajumbe wanaomnukuu wanaishia hapo bila kwenda katika mapendekezo aliyoyatoa.
“Wamenisifu sana ni mchumi mahiri, basi waendeleze sifa hizo kwa mapendekezo niliyoyatoa ya mapato ya kukidhi uendeshaji wa serikali ya shirikisho.
“Nimeeleza katika hali halisi kuwa utaratibu mzuri ni mapato ya kila serikali kuchangia katika shirikisho na mambo haya yaandikwe katika Katiba. Katiba inaweza ikasema wazi asilimia 20 ya mapato yote yanayokusanywa Zanzibar au Tanganyika yataenda kwenye shirikisho.”
Alisema ukurasa wa kwanza wa Rasimu ya Katiba unaeleza kuwa; “toleo hili la Rasimu ya Katiba lilichapishwa katika Gazeti la Serikali kwa mujibu wa Kifungu cha 20(2) ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83,” hivyo akasema ni rasimu ya Tume ya Rais na si ya Wapemba.
Hata hivyo, alisema mjadala unaoendelea bungeni umekuwa na utaratibu wa ubaguzi... “Watu wamebaguliwa humu na viongozi wakubwa wanapiga makofi, Bunge hili limekuwa kama Bunge la Intarahamwe. Hii ni hatari kwa nchi yetu. Wapemba, Waarabu, Wahindi, Wakongo,” alisema.
“Hii hatuhitaji, tunahitaji Katiba ambayo itahakikisha kila mwananchi anapata haki yake, wote tuwe sawa bila kujali rangi zetu, jinsia zetu, makabila yetu, huu ndiyo msingi aliotuachia Mwalimu Nyerere tuenzi msingi huo.”
Profesa Lipumba alilalamikia kile alichokiita ubaguzi ndani ya Bunge huku akihoji kama Serikali haikutaka Katiba Mpya kwa nini imepeleka wabunge Dodoma kwa gharama kubwa?
Pia alihoji ni kwa nini ilitumia Sh70 bilioni katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Kwa nini mmetufikisha hapa? Jengo hili nimeambiwa limekarabatiwa kwa Sh8.2 bilioni hali hamuamini Rasimu ya Katiba au ilikuwa ni utaratibu wa kupata hizo asilimia 10, ndiyo maana mmekarabati kwa gharama kubwa?” alisema.
“… Tumechoka kusikiliza matusi. Tumechoka kudharau mawazo ya wananchi, tumechoka ubaguzi, hatuwezi kuwa sehemu ya kundi linalohamasisha ubaguzi ndani ya Tanzania, hili hatukubali,” alisema.
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa