Home » » WAPINGA RUZUKU KWA VYAMA VISIVYO NA WAWAKILISHI

WAPINGA RUZUKU KWA VYAMA VISIVYO NA WAWAKILISHI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwanasiasa mkongwe nchini na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hassy Kitine


Wananchi mbalimbali wamepinga pendekezo la baadhi ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba la kutoa ruzuku kwa vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu.

Kamati Namba Sita ikiwasilisha maoni yake kupitia kwa Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage, ilipendekeza iwekwe ibara katika katiba inayoeleza vyama vyote vyenye usajili wa kudumu kupewa ruzuku ili kuweka mazingira sawa kwa vyama vyote pamoja na kuboresha demokrasia nchini.

Hata hivyo, Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 1996 inataja vigezo vya kupata ruzuku kuwa ni kupata asilimia tano ya kura wakati wa uchaguzi mkuu, kuwa na wabunge na madiwani.

Mwanasiasa mkongwe nchini na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hassy Kitine, alipinga azma ya kutaka kutoa ruzuku kwa vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu, akieleza kuwa ni ufujaji wa fedha za umma.

Dk. Kitine ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, alisema kama azma hiyo itafanikiwa, itatoa mwanya kwa wajanja kuanzisha chama cha siasa kwa nia ya kupata ruzuku pekee.

“Kwamba mtu akitaka fedha za bure anaanzisha chama cha siasa, halafu anaingia mitini; hii siyo sahihi. Mimi nadhani vingepewa tu vyama vyenye wabunge.” alisema.

Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Haji Semboja, alisema wazo hilo ni zuri, lakini linaweza lisitekelezwe ipasavyo kwa kuwa bajeti ya serikali haitoshi.

“Wazo ni zuri na nina amini wataweka vigezo vya vyama ambavyo vinaweza kupewa ruzuku, lakini kiuteundaji serikali haina fedha, kwa hiyo wanaweza wasipewe hiyo ruzuku,” alisema.

Naye Mhadhiri mwingine wa UDSM, Dk. Benson Bana, alisema jambo hilo ni zuri kwa kuwa ni ngumu kwa vyama vichanga na visivyo na fedha kushindana na vyama vikubwa vinavyopata ruzuku ya hadi shilingi bilioni moja kwenye uchaguzi.

“Nafikiri ni jambo jema, vyama hivi vinafanyakazi ya siasa tuweke vigezo mahsusi lakini kwa kweli ni lazima wote tuwawezeshe ili kuweka uwanja sawa wa ushindani ili kufanya uchaguzi huru na wa haki,” alisema.

MWANZA
Wakazi kadhaa wa jijini Mwanza, wameishauri Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kusitisha utoaji wa ruzuku kwa vyama ambavyo havina malengo na pesa za wananchi.
Gerald Urio alisema: “Tatizo ni msajili wa vyama ambaye anashindwa kufuatilia fedha zinazotolewa kwa vyama kutojua zinafanya kazi ipi…pia vyama visivyo makini havina malengo mazuri na pesa hizo na vinaweza kuzitumia kwa maslahi ya viongozi wao pekee.”

Mwamvita Ismail alisema ofisi ya msajili inatakiwa iwe na vigezo kwa kutoa ruzuku kwa vyama vyenye uwakilishi. Aman Abdallah, alisema vyama vingi vipo kiujanja-ujanja, hivyo visipewe ruzuku kwani pale vinapopatiwa pesa hizo zinawa elekeza wanachama wake.

ARUSHA
Mkazi wa jijini Arusha, Samson Pantaleo, alisema vyama vilivyopo nchini vingi ni mamluki wa chama tawala.

“Kutokana na hilo waache kuleta propaganda ya kuchezea fedha za umma na havistahili kabisa kupewa ruzuku kwa sababu hawana kazi,” alisema.

Naye Joshua Sulle, alisema vyama visivyo na uwakilishi wa madiwani na wabunge havistahili kupewa ruzuku kwa sababu havina wawakilishi wa wananchi.

Mwanachama wa Chama cha Viziwi Tanzania mkoani Arusha, Anna John, alisema wanastahili kupewa sababu ni chama kilichosajiliwa na kipo kwa mujibu wa sheria za nchi.

MOROGORO
Mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo Kikuu cha St. Jodan, Juvenal Mallya, alisema vyama hivyo havistahili kupewa fedha hizo kwakuwa vingi havina uwakilishi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Alisema kuwa ili chama kiweze kuonekana kinafanya vizuri ni lazima kiwe na wabunge au idadi kubwa ya madiwani, hivyo vyama hivyo vidogo kama havina uwakilishi huo visipatiwe ruzuku inatokana na kodi za wananchi.

Mwimboni Salum, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Waislamu mjini Morogoro, alisema hata kama kuna vyama vinavyopewa ruzuku bila kuwa na idadi kubwa ya wabunge na madiwani vinapaswa kufutiwa ruzuku kwa kuwa havina faida kwa wananchi.

“Ninachojua chama cha siasa kinajiandaa kushika dola, kwa kuanzia lazima kishawishi wananchi wawachague katika udiwani na ubunge kama havipati kabisa sasa vina faida gani kwa wananchi, hivyo vinyimwe ruzuku inayotokana na kodi zetu,” alisema Salum.

Musa Ngayatu, msomi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua), alisema vyama  vyote havistahili kuendelea kupewa ruzuku kwa kuwa  hakuna cha maana na faida kwa wananchi zaidi ya kujineemesha viongozi kwa kuwa vyama hivyo vina nia ya kuongoza dola, vinapaswa kuwashawishi wanachama wao kuchangia shughuli zao na harakati badala ya kupewa fedha za wananchi.

IRINGA
Timotheo Mkanyia kutoka Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO) mkoani Iringa,  alisema ruzuku inatolewa kwa vyama kwa kuzingatia umakini wa chama ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa majukumu kikamilifu kwa manufaa ya wananchi walipa kodi.

“Kuna baadhi ya vyama vina wabunge wachache na madiwani wachache, lakini mtizamo wao ni katika ujenzi bora wa taifa, hivyo vinastahili kupewa,” alisema.
Michael Noel wa Chuo Kikuu cha Iringa, alisema vyama visivyokuwa  na uwakilishi havitakiwi kupewa ruzuku kwani inakuwa kama kuwapa mtaji viongozi wake.

DODOMA
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanataaluma katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udomasa), Paul Loisulie, alisema vyama hivyo havistahili kupewa ruzuku kwani kitendo hicho kitahamasisha watu wengi kuunda vyama kwa ajili ya motisha ya ruzuku.

“Tunaweza kujikuta na vyama vingi pasipo na sababu halafu unakuwa mzigo kwa bajeti ambayo kimsingi ni ndogo siku zote, hapana visipewe,” alisema Loisulie.

Shekhe wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu, alisema  ruzuku hiyo haina tija kwa vyama ambavyo havina wabunge wala madiwani na matokeo yake itaishia kwa viongozi bila kusaidia wananchi.

“Hivi vyama ambavyo vina madiwani na wabunge ndio wawakilishi wa wananchi na kupitia wao ndipo wanaweza kupata  mahitaji yao…Isije ikawa mtu anaanzisha chama chake kwa maslahi yake binafsi,” alisema Shekhe huyo. 

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wilaya ya Chamwino, Amani Msanga, alisema ili kupanua demokrasia nchini vinapaswa kupewa ruzuku ili viweze kujiendesha na kuwafikia wanachama, lakini alipendekeza  kuwapo na ukomo wa vyama vya siasa kwa kuwekwa masharti kusije kukawa na utitiri wa vyama  kwa ajili ya maslahi.

TANGA
Mjini Tanga, Ramadhan Manyeko, Kamishna wa Chama cha NCCR-Mageuzi, alisema vyama vidogo ambavyo vinashindwa hata kushiriki kwenye uchaguzi mkuu na badala yake hukaa na kusubiri kufanya makongamano havina sababu ya kuendelea kuwapo kwenye orodha ya msajili wa vyama vya siasa nchini.

“Vipo pia baadhi ya vyama vya siasa ambavyo  vinapewa ruzuku ya serikali wakati havina shughuli yoyote ya msingi katika kuwanufaisha wananchi, fedha ambazo zingeweza kutumika katika kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi kwenye sekta muhimu kama elimu, afya na maji....ni bora vingefutwa,” alisema Manyeko.

Mosses Francis, mwanafunzi wa Sheria Chuo Kikuu cha Cambridge alisema: “Mfano hai ni kuanzia sasa hadi mwakani  ambao ni mwaka wa uchaguzi, kutaibuka vyama vingi, lakini ukiangali muundo wa chama husika ni ubabaishaji mtupu sasa kwa nini viendelee kupata usajili na mwisho wa siku kupewa ruzuku kwa sababu tu wana diwani mmoja.”

Neema Ambrosy, Mkurugenzi wa Kituo cha Kutetea Haki za Wanawake, alisema hakuna sababu ya kuwa na orodha ndefu ya vyama vya siasa nchini ambavyo husikika nyakati za uchaguzi mkuu na ule wa serikali za mitaa kwa ajili ya maslahi binafsi na kuongeza:

“Katika hili tumuombe Msajili wa Vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi kuanza mchakato wa kuvifuta baadhi ya vyama ambavyo utendaji wake unasuasua….maana huu ni wizi.”

KILIMANJARO
Mhadhiri Msaidizi wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii ya Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Emanuel Damalo, alisema vyama vidogo vya siasa ambavyo vinaendeshwa kwa ujanja ujanja kutokana na kutofanya chaguzi huku baadhi ya viongozi kung’ang’ania madaraka, havistahili kupewa ruzuku kutokana kutumia usajili wake kujinufaisha.

“Vyama hivyo havistahili ruzuku inayotokana na fedha za walipa kodi kwa sababu havijipambanui kwa wananchi, wala kufungua matawi yao kwenye ngazi za wilaya, lakini pia hakuna uongozi wa chini ukiacha ule wa kitaifa. Hakuna zaidi ya kutafuta maslahi kupitia usajili wanaopewa,” alisema Damalo. 

Imeandikwa na  Daniel Mkate, Mwanza; Ashton Balaigwa, Morogoro; George Tarimo, Iringa; Augusta Njoji, Dodoma; Restuta James; Dar, Lulu George, Tanga; Godfrey Mushi, Moshi na Cynthia Mwilolezi, Arusha.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa