Home » » MJADALA WA ESCROW: BUNGENI VURUGU TUPU

MJADALA WA ESCROW: BUNGENI VURUGU TUPU

 MJADALA kuhusu ripoti ya uchunguzi wa fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow iliyowasilishwa bungeni Mjini Dodoma na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na utetezi wa Serikali kuhusu sakata hilo, jana umewagawa wabunge.

Ripoti ya PAC inatokana na uchunguzi uliofanywa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambapo mjadala huo ulianza jana jioni ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bunge ambaye ni Mbunge wa Ilala, Bw. Mussa Azzan Zungu.
 Kabla ya kuanza mjadala huo, Bw. Zungu aliwataka wabunge kuijadili ripoti hiyo kwa utulivu na kuvumiliana lakini hali ilikuwa tofauti na maombi yake.

Wabunge waliokuwa wakichangia mjadala huo, walitofautiana kimtazamo juu ya sakata hilo baadhi yao wakitaka viongozi waliotajwa wawajibishwe na wengine wakipinga.
Mbunge wa Singida Mashariki, Bw. Tundu Lissu (CHADEMA), alisema wanaotajwa katika ripoti hiyo lazima waachie ngazi kuanzia Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema pamoja na viongozi wengine.

Alijenga hoja kuwa fedha za Akaunti ya Escrow hazikuwa binafsi kwani haiwezekani fedha binafsi zipate maelekezo ya kutolewa kwenye akaunti kwa ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwenda Ikulu.
Alisema barua ya kutolewa fedha hizo kwenye akaunti hiyo iliandikwa na Ikulu kwa niaba ya Rais wakati fedha binafsi haziwezi kutolewa maelezo na Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mwanasheria wa Serikali wala Ikulu.

Aliongeza kuwa, kwa msingi huo fedha hizo zilikuwa za umma hivyo waliohusika kuanzia Waziri Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mawaziri na wabunge, wawajibishwe na kuwajibika.
Bw. Lissu alienda mbali zaidi akimtaka Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa Taifa kuwajibika kwani haiwezekani miamala ya fedha ifanyike bila wao kujua kinachoendelea.

"Wale wanaodai fedha hizo si za umma ni wale waliohongwa," alisema Bw. Lissu na kuongeza kuwa, wote waliotajwa kupokea mgawo wa fedha hizo wakiwemo watumishi wa Serikali wamelitia aibu Taifa.
Mbunge wa Muleba Kaskazini, Bw. Charles Mwijage (CCM), alisema jambo sakala hilo ni zito lakini kwa kuwa Kamati ya PAC imelifikisha mbele ya Bunge, linapaswa kufanyiwakazi na maamuzi magumu yatolewe na wabunge wote.

Alisema tangu kuanzishwa IPTL mwaka 1994, haoni sababu ya mtu kama Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Stephen Massele, kuambiwa awajibike kwa sababu ya kumsema Balozi wa Uingereza na kusisitiza Bunge linapaswa kuondoa kibuyu ambacho kimekuwa mzigo.
Aliongeza kuwa, katika ripoti ya CAG haoni sehemu ambayo Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, anaguswa na kutakiwa kuwajibika na mapendekezo ya PAC kutaka mitambo ya IPTL itaifishwe, alionya wabunge kuwa makini kwani kufanya hivyo ni kubeba mzigo wa deni linalodaiwa na Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong.

Alisema deni hilo linatosha kununua mtambo mpya ukafungwa Kinyerezi na kazalisha umeme mwingi zaidi ya ule wa IPTL.
Chanzo;Majira
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa