Home » » SAKATA LA ESCROW: KAFULILA: NILITISHWA SANA, SASA YAMETIMIA

SAKATA LA ESCROW: KAFULILA: NILITISHWA SANA, SASA YAMETIMIA

 SIKU moja baada ya Bunge kupitisha maazimio nane ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (PAC), kutokana na sakata la uchotaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, Mbunge wa Kigoma Kusini, Bw. David Kafulila (NCCR-Mageuzi), ameweka wazi usumbufu alioupata katika sakata hilo.

Akizungumza na Majira jana, Bw. Kafulila ambaye ndiye aliyeliibua sakata hilo bungeni, alilishukuru Bunge kwa hatua waliyochukua baada ya kupokea ripoti ya PAC, kuijadili na kufikia uamuzi wa kuchukua hatua kwa wahusika.

Alisema baada ya kuibua ufisadi huo bungeni, aliingia katika vita kubwa na wabunge waliokuwa wanatumiwa na mafisadi pamoja na mafisadi wenyewe.

"Kutokana na vitisho nilivyokuwa nikivipata katika simu yangu ya mkononi na mitandao mingine, niliishi kwa tabu Mjini Dodoma nikibadili hoteli...sikuishia hapo bali nilikwenda polisi Dodoma mara mbili," alisema.

"Nilikuwa nakunywa kwa uangalifu sana hasa nikiwa Dodoma ingawa hata Dar es Salaam nilichukua tahadhari, ninachoweza kusema, ufisadi huu ni mkubwa uliohusisha mfumo mzima serikalini," alisema Bw. Kafulila.

Aliongeza kuwa, hatua tulizochukua kama Bunge zinaweza kuonekana kutosha kwa Bunge changa kama hilo lakini kwa mabunge yaliyokomaa, sakata hilo lilitosha kuiingiza nchi katika Uchaguzi Mkuu.

"Ni vyema Rais Jakaya Kikwete asafishe watendaji wake Ikulu ili aweze kuendesha nchi kwa misingi ya sheria na utawala bora...Benki ya Stanbic lazima warudishe fedha kwa kushiriki utakatishaji fedha haramu.

"Huu ni utaratibu wa kimataifa kama ilivyokuwa nchini Nigeria ambapo Stanbic imeingia kwenye kashfa ikidaiwa kushiriki utakatishaji fedha takriban dola za Marekani bilioni nane," alisisitiza Bw. Kafulila.

Juzi sakata hilo lilihitimishwa katika hatua nzuri bungeni baada ya Bunge kuazimia viongozi wote waliotajwa katika ripoti ya CAG wakihusishwa na sakata hilo, wawajibishwe.

Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Bw. Zitto Kabwe, alisema maazimio hayo yamefikiwa na Kamati ya Maridhiano katika kikao kilichoshirikisha Kambi ya Upinzani, CCM na Serikali.

Alisema Bunge hilo limeazimia mamlaka ya uteuzi iwawajibishe na kutengua uteuzi wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliachim Maswi na wajumbe wa Bodi ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO).

Maazimio mengine ni Rais kuunda tume ya kijaji ili kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Euden Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Mengine ni mamlaka husika za kifedha na kiuchunguzi ziitaje Benki ya Stanbic Tanzania Ltd na benki nyingine yoyote itakayogundulika kujihusisha na utakatishaji fedha zilizotolewa katika akaunti hiyo kuwa ni taasisi za utakatishaji fedha haramu.

Bw. Kabwe aliyataja maazimio mengine kuwa Serikali iandae na kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria iliyoiunda Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), kwa lengo la kuanzisha taasisi mahususi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa Taifa.

Pia walishauri Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO ili kuokoa fedha za shirika hilo na Serikali iwasilishe taarifa za utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme kabla ya kumalizika mkutano wa Bunge la Bajeti.

Azimio lingine Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, viwachukulie hatua stahiki za kisheria watu wote waliotajwa katika taarifa maalumu ya kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya akaunti hiyo na wengine ambao watagundulika kuhusika katika vitendo hivyo kutokana na uchunguzi unaoendelea.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa