KWA HERI MWAKA 2014 ULIONOGESHWA NA FILAMU YA KATIBA NA ESCROW

 
 Waziri Mkuu Mstaafu na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Joseph Warioba (aliyekaa) akikingwa  na wsaidizi  kufuatia vurugu zilizozuka alipok
Hatmaye miezi 12 imekamilika leo ikiashiria kumalizika kwa mwaka 2014 utakaokumbukwa na wengi kwa kuwa na matukio motomoto.
Matukio ya kukumbukwa ni mengi, hata hivyo jarida la Ndani ya Habari leo linahitimisha mwaka kwa kuangazia baadhi ya matukio muhimu yalivyoibua mijadala ya kitaifa na kuvuta hisia za watu wengi.
Tanzania Kinara wa ujangili
Februari 10, 2014, ikiwa ni siku chache kabla ya Rais Jakaya Kikwete kuhudhuria mkutano jijini London, Uingereza, uliohusu ajenda ya kuokoa viumbe vilivyo hatarini kutoweka duniani, tatizo la ujangili lilibua kashfa nzito nchini.
Taarifa ya gazeti la The Mail on Sunday la Uingereza la Februari 8, mwaka huu liliitaja Tanzania kama kinara wa ujangili kwa kuua zaidi ya tembo 11,000 kwa mwaka, huku Rais wake (Jakaya Kikwete) akielezwa kuwa anafumbia macho tatizo hilo.
Sehemu ya taarifa hiyo ilinukuliwa ikisema: “Utawala wa Rais Kikwete umetawaliwa na mauaji ya tembo yaliyovunja rekodi katika historia ya nchi yake. Kibaya zaidi, wahifadhi wanasisitiza kuwa ndani ya Serikali kuna viongozi wanaoshiriki biashara hiyo.”
Hata hivyo, Serikali iliagiza kufanya uchunguzi wa kujiridhisha na taarifa hizo, lakini mpaka mwaka unakatika hakuna taarifa zozote zilizotolewa kuhusu tuhuma hizo.
Mfumo mpya wa madaraja ya ufaulu kuibua mjadala
Februari 22, mwaka huu, Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), lilitangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wa 2013, huku ufaulu ukiongezeka kwa asilimia 15.17 kupitia mfumo mpya wa upangaji ambao ulipanua wigo wa alama na madaraja ya ufaulu.
Upangaji mpya wa alama hizo ulikuwa ni A: 75-100, B+:60-74, B:50-59, C:40-49, D:30-39, E:20-29 na F:0-19. Kabla ya mabadiliko hayo, alama zilizokuwa zikitumiwa kupanga matokeo ya kidato cha nne zilikuwa ni A:80-100, B:65-79, C:50-64, D:35-49 na F: 0-34.
Wadau wengi waliokosoa mfumo huo ambao mbali ya kuongeza wigo wa watu kufaulu hata kama hawana sifa, walisema ulikuwa ni mpango maalumu wenye utashi wa kisiasa uliolenga kuwaridhisha wananchi
Ajira Uhamiaji
Ajira imeendelea kuwa wimbo wa kwa vijana wengi hasa wahitimu. Takwimu kutoka Wizara ya Kazi na Ajira zinazoenysha kuwa taifa lina uwezo wa kukidhi mahitaji ya ajira 80,000 mpaka 100,000 kwa mwaka ukilinganisha na mzigo wa vijana 400,000 mpaka milioni moja wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka.
Katika kudhihirisha hilo, Juni 13 kulitokea tukio la aina yake katika historia ya nchi baada ya zaidi ya watu 10,000 waliomba kazi ya wakaguzi wasaidizi wa uhamiaji kuitwa na kufanyiwa usaili kwenye Uwanja wa Taifa.
Kilichoshtua wengi katika tukio hili ni idadi kubwa ya wasailiwa hali iliyolazimu wahusika kutumia uwanja wa mpira kufanya usaili wa maandishi.
Hata hivyo, siku chache baadaye, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nachi ilitoa taarifa ikisema wingi wa wasailiwa ni matokeo ya kidemokrasia ya kutoa nafasi kwa kila raia kushindania nafasi za ajira zinazotolewa nchini ili mradi awe na sifa.
‘Filamu’ ya Bunge la Katiba
Bunge la Maalumu la Katiba lilikuwa ni moja kati ya habari zilizoteka vyombo vya habari na hisia za Watanzania wengi kutokana na mijadala mikali, na hata vurugu. Kikubwa katika mchakato wa Bunge la Katiba ilikuwa ni kuwekwa kando kwa hoja ya muundo wa Muungano wa serikali tatu, jambo lilowafanya wajumbe kutoka vyama vya upinzani kuungana na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), na baadaye kususia vikao vya chombo hicho cha kuandika Katiba.
Bunge la Katiba lilianza Aprili 2 likitakiwa kuwa na wajumbe 629 huku matarajio ya wengi yakiwa wajumbe wangetumia nafasi hiyo kujadili mapendekezo ya Rasimu ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kwa mshangao wa wengi, bunge hilo lililotawaliwa na hisia na itikadi za CCM kwa kiasi kikubwa liliyapa kisogo mapendekezo ya tume na hatimaye kumalizika kwa kuingiza mapendekezo mapya kwenye Katiba Inayopendekezwa iliyokabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete Oktoba 9.
Kashfa ziara ya Rais wa China
Novemba 7, mwaka huu, ziara ya Rais Xi Jinping wa China aliyoifanya nchini Machi mwaka jana, ilizua kizaazaa na kuitia doa sifa ya Tanzania kimataifa, baada ya maofisa waliokuwa wameambatana naye kutuhumniwa kuhusika na biashara haramu ya meno ya tembo.
Ripoti iliyotolewa na taasisi ya kimataifa ya Uingereza Environmental Investigation Agency(IEA), inayojihusisha na uchunguzi wa masuala ya mazingira, inadai kuwa maofisa hao walinunua kiasi kikubwa cha bidhaa hizo katika soko la Mwenge, Dar es Salaam kisha kuzisafirisha kidiplomasia kwa ndege ya rais huyo.
Baada ya kulipotiwa taarifa hizo Watanzania walishtushwa na taarifa hiyo huku serikali ikikanusha vikali madai hayo kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kabla ya kuunda jopo la uchunguzi wa kujiridhisha na ukweli huo.

Hata hivyo, mpaka sasa hakuna taarifa zozote juu ya kamati ya uchunguzi kuhusu kashfa hiyo.
Sakata la Ecrow
Sakata la utata wa kuchotwa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow kwenda IPTL, lilichukua nafasi kubwa ya mjadala kwa mwaka 2014. Lilinogesha ajenda za viongozi wa dini, wanaharakati na jamii huku vituo vya daladala za Tegeta zikipewa majina ya escrow.
Sakata hilo lilikuwa na sura mbalimbali kama vile umiliki wa hisa za Kampuni ya Pan Africa Power Solution Tanzania Limited (PAP), nani mmiliki halali wa fedha za akaunti hiyo, ukwepaji wa kodi, tuhuma za rushwa kwa viongozi na miamala ya malipo iliyotokea katika benki kadhaa.
Ni sakata lililoibuliwa na gazeti la The Citizen ambalo ni gazeti dada na Mwananchi na hatimaye kujadiliwa bungeni na kutolewa maazimio nane, yakiwamo kuwajibishwa baadhi ya watendaji wakuu serikalini, na kupitia upya mikataba yote ya Tanesco na kampuni za umeme.
Baada ya maazimio ya Bunge macho na masikio yalielekezwa kwa Rais Jakaya Kikwete kufanyia kazi mapendekezo. Hatimaye Desemba 22 Rais alikutana na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam na kuelezea kwa kina sakata la Escrow na maazimio ya Bunge.
Ukiondoa kuteungua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kwa jumla mazungumzo ya Rais hayakukidhi matarajio ya wananchi hasa kwa kuyafanyia kazi maazimio ya Bunge.
Hata hivyo, Ikulu ilitangaza kumsimamisha katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi akisubiri uchunguzi. Awali aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Frederic Werema aliandika barua ya kujiuzulu akieleza kuwa ushauri wake haukueleweka na ulizua tafrani
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

SHEIKH SHARIF AZUA MAPYA YA URAIS 2015.


Sheikh Shariff Matongo  akizungumza leo na waandishi wa habari ofisini kwake  jijini Dar es Salaam (hawapo pichani)kuhusu  ndoto yake ambayo ameoteshwa kuelekea mwaka 2015.

NA CHALILA KIBUDA,GLOBU YA JAMII,DAR.

Sheikh Sharif Matongo amesema ameoteshwa ndoto ya mwaka 2015 na kupata ushauri kwa mashekh mbalimbali Duniani ambavyo vitatokea nchini na viongozi wasipuuze ndoto hiyo. Sharif aliyasema hayo leo ofisini kwake alipokutana na waandishi wa habari ,alisema ameoteshwa mambo saba likiwemo la kupata Rais ajaye ambaye kiongozi ambaye muda mwingi ameishi nje ya nchi kwa kufanya kazi.

Alisema katika ndoto nyingine kifo cha kiongozi mkubwa  ambaye ameshika nyadhifa mbalimbali na  mwenye kambi katika Chama cha Mapinduzi (CCM). Sheikh  alisema ndoto nyingine  kutokea kwa mvua nyingi ambapo watu wanaoishi mabondeni ,kutokea kwa vifo vya watoto vingi ,wafanyabiashara kupata mafanikio  makubwa kwa mwaka utaoanza kesho.

Vijana wengi watashinda katika uchaguzi ujao na wazee wataangushwa sana hivyo wanatakiwa kujitokeza,katiba inayopendekezwa  itapita lakini kutakuwa na vurugu ambazo zitaibuliwa na vijana.

‘’Ndoto yangu  niliooteshwa sikukaa nayo peke yangu, niliweza kupata ushauri kutoka kwa watu mbalimbali akiwemo Mufti wa  Abhu Dhabi,Mufti wa Nigeria  na wengine wote wakaniambia suala hilo nisikae nalo,niwashirikishe na Watanzania wenzangu’’alisema Sheikh Shariff Matongo.

Sheikh Shariff alisema katika usafiri wa bahari utakuwa mbaya kutokana na bahari kuchafuka na chombo kimoja kitazama kutokana na kuchafuka huko.


Alisema ndoto hizo ni lazima kuzingatia kutokana na kupata ushauri wa watu wengi wenye kuaminika katika jamii katika mataifa mbalimbali ulimwenguni.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

DODOMA YATINGA FAINALI KWA KISHINDO

Dodoma imeiduwaza Kigoma baada ya kuichapa mabao 2-1 na kufanikiwa kutinga fainali ya mashindano ya Copa-Coca-Cola jana kwenye Uwanja wa Karuma, Dar es Salaam.
Hii ni mara ya kwanza kwa timu ya Dodoma kufuzu hatua hatua ya fainali tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo 2007.
Mshujaa wa Dodoma katika mchezo huo  Juma Magid na Pius Raphael walifunga mabao mawili wakati Nashri Adam akifunga bao la kutokana na machozi kwa Kigoma.
Kocha wa Dodoma, Mussa Fiurutuni alisema  nimefurahi sana timu yangu kuingia hatua ya fainali kwa mara ya kwanza.
“Wachezaji wangu walicheza kwa ari kubwa na kujituma jambo lililochangia kupata ushindi huu, nimefurahi sana kwa kweli,” alisema kocha huyo.
Kigoma walipewa nafasi kubwa ya kuibuka bingwa wa mashindano haya ya mwaka huu walikuwa wa kwanza kupata bao dakika pili lililofungwa na Nashri Adam aliyeunganisha kwa umakini mpira uliopigwa na Shaban Maneno na kumwacha kipa wa Dodoma asijue la kufanya.
Baada ya bao hilo Dodoma iliamka na kusawazisha dakika ya 19 kupitia kwa Juma Magid kwa kichwa baada ya kuunganisha mpira wa adhabu ndogo na kufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare 1-1.
Dodoma ilianza kipindi cha pili kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la pili dakika 49 kupitia kwa Pius Raphael aliyepiga shuti lililomshinda kipa Kigoma, Bashiri Twalib.
Kocha wa Kigoma, Hamis Mabo alisema makosa machache yaliyofanywa na safu yake ulinzi yameigharimu timu yake.
“Kusema ukweli wa kujilaumu ni sisi wenyewe kutokana na makosa tuliyofanya, ila kikubwa ndiyo matokeo yalivyo na ni lazima tukubaliane nayo,” alisema Mabo.
Dodoma ilifanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kuifunga Morogoro kwa mabao  2-1, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe huku Kigoma ikiifungasha virago Mwanza kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Karume.
Mashindano haya ya vijana yanayofanyika kila mwaka nchini yana lengo la kuibvua vipaji vipya katika mwendelezo wa ukuzaji wa soka la Tanzania.
Kampuni wadhamini wa mashindano haya, Coca cola huleta wakufunzi kila mwaka nchini kwa ajili ya vijana wanaounda timu ya kombaini na kuangaliwa kabla ya kwenda kuendelezwa katika vituo vya nje.
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WATU MILIONI 11 TU KUPIGA KURA JUMAPILI

JUMLA ya Watanzania milioni 11.4 wamejiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Jumapili wiki hii, sawa na asilimia 62 ya lengo lililowekwa.
Katika uchaguzi huo, watakaochaguliwa ni wenyeviti wa vijiji na wajumbe wa halmashauri za vijiji, wenyeviti wa mitaa na wajumbe wa kamati za mitaa na wenyeviti wa vitongoji.
Mkoa wa Katavi umeongoza kwa kuandikisha asilimia 78 ya wapigakura huku mkoa wa Dar es Salaam umetajwa kufanya vibaya katika kuandikisha wapiga kura, ambapo waliojiandikisha ni asilimia 43 Pia katika uchaguzi huo wa Desemba 14, kutakuwa na ingizo jipya ambalo ni nembo ya chama ili kuwawezesha watu wasiojua kusoma na kuandika, kutambua kwa urahisi mtu wanayempigia kura.
Kwa walemavu ambao wako katika makundi maalumu, watalazimika kufika na ndugu zao, kwani ni marufuku kwa wasimamizi au walinzi au mtu yeyote anayehusika na uchaguzi, kumsaidia mpigakura kupiga kura yake.
Mkurugenzi wa Idara ya Serikali za Mitaa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Calist Luanda alisema hayo katika mkutano wake wa waandishi wa habari mjini hapa jana. Alisema katika uchaguzi huo, walitarajia kuandikisha wapigakura 18,587,742.
Alisema matarajio hayo yalipatikana, kutokana na taarifa za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, ambayo inaonesha asilimia 40 ya Watanzania wote wana miaka 18 na kuendelea.
Kati ya matarajio ya kuandikisha wapigakura 18,587,742, walioandikishwa ni 11,491,661, sawa na asilimia 62 ya matarajio,” alisema.
Alisema jukumu la serikali lilikuwa ni kuhamasisha wananchi wakajiandikishe na zaidi ya nusu ya watu waliotarajiwa kuandikishwa, wameandikishwa.
“Mkoa ulioandikisha Watanzania wengi ni Katavi asilimia 79 ya matarajio ukifuatiwa na mkoa wa Kagera asilimia 78,” alisema.
Alisema mkoa ambao haukufikia malengo chini ya asilimia 50 ni Dar es Salaam ulioandikisha asilimia 43 ya malengo yake, ukifuatiwa na Mkoa wa Kilimanjaro ulioandikisha asilimia 50.
Kwa upande wa halmashauri iliyovuka lengo ni Mpanda, iliyoandikisha asilimia 107 ya matarajio na halmashauri ya Babati asilimia 101 ya malengo waliyojiwekea.
Halmashauri zilizofanya vibaya ni Kilindi mkoani Tanga iliyofikia asilimia 21 ya matarajio na Same, mkoa wa Kilimanjaro asilimia 22 ya matarajio.
Alisema kutakuwa na karatasi za kura, ambayo itaandaliwa na halmashauri husika ambayo itakuwa na jina la mgombea, jina la chama, nembo ya chama na nembo ya halmashauri.
Alisema mpigakura atatakiwa kuweka alama ya tiki katika kisanduku kilichopo chini ya nembo ya chama, kuonesha kuwa amempigia kura mgombea aliyemtaka kumchagua.
Pia, vituo vya kupigia kura vinatakiwa kuwa wazi kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 10 jioni ya siku ya kupiga kura, hivyo wapigakura watakaokuwepo kituoni saa 10 jioni, wataruhusiwa kupiga kura hadi watakapokuwa wamemaliza kupiga kura.
“Kutakuwa na sanduku maalumu la kupigia kura lililotengenezwa kwa namna itakayomwezesha mpiga kura na kutumbukiza kura yake kwa urahisi bila kuruhusu kura hiyo kutolewa ndani ya sanduku hilo,’’ alisema.
Alisema kabla ya kuanza kupiga kura, msimamizi wa uchaguzi atawaonesha wapigakura sanduku la kupigia kura lililo wazi na atalifungua kwa lakiri, kwa namna ambayo itazuia kufunguliwa bila kukata lakiri.
Alisema vitambulisho vitakavyotumika ni vitambulisho vya wapigakura uchaguzi mkuu, kitambulisho cha kazi kama mfanyakazi, hati ya kusafiria, kadi ya benki, kadi ya bima ya afya, kitambulisho cha shule kwa mwanafunzi mwenye miaka 18 na kuendelea, kitambulisho cha udereva au kitambulisho cha uraia.
Chanzo:habari Leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

DC ATAKA WANAMGAMBO WALIOAJIRIWA KUJALI TIJA

 http://www.habarileo.co.tz/images/christopher-Kangoye.jpg
MKUU wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Christopher Kangoye amewataka vijana 120 wa wilaya hiyo waliopata ajira ya kupitia kampuni ya Suma JKT, kuzingatia uadilifu na uzalendo ili wawe na tija kwa taifa.
Vijana hao walipata ajira baada ya kumaliza mafunzo ya mgambo katika Kata ya Kimagai nje kidogo ya Mji wa Mpwapwa.
Kati ya vijana 166 waliohitimu mafunzo hayo kwa ustadi, vijana 120 walibahatika kuingia kwenye ajira moja kupitia SUMA JKT ambalo ni tawi la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) hapa nchini ambalo limejikita katika uzalishaji.
Kangoye, ambaye alikuwa Kamanda wa mafunzo na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya, aliwataka vijana kuwa waadilifu na kuonesha uzalendo kwa nchi yao.
Alisema mafunzo ya mgambo na JKT yamekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi hasa vijana ambao kwa sasa vijana wengi wamekuwa wakikosa uzalendo kadri siku zinavyozidi kusonga mbele na kutishia mustakabali wa amani ya taifa kutokana na uzalendo kupungua.
Alisema ajira 120 ambazo vijana hao wamezipata zimesaidia kupunguza idadi kubwa vijana wa wilaya hii ambao walikuwa hawana ajira rasmi za kujipatia kipato na kuendesha maisha yao.
Mratibu wa Mafunzo na Mshauri wa Mgambo wilayani Mpwapwa, Sajini Taji Wiliam Emmanuel alisema jumla ya vijana 370 walianza mafunzo hayo, hata hivyo waliobahatika kumaliza ni vijana 166 na waliopata ajira ni vijana vijana 120.
Aliitaka jamii kuondokana na dhana potofu kuwa mafunzo ya mgambo ni mateso kwa jamii bali alisema mafunzo hayo yanawasaidia vijana kuwaweka katika mazingira mazuri kiafya.
Alisema vijana hao watasafiri Desemba 15, mwaka huu kuelekea Dar es Salaam ambapo watasambazwa maeneo mbali ya mikoa ya Tanzania bara.
Chanzo;Habari Leo

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MAADHIMISHO YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI YAFANYIKA MKOANI DODOMA‏



 Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Dodoma Bi. Amina Mfafaki akifafanua jambo wakati alipokuwa akiongea wakati wa kufunga maadhimisho ya siku 16 ya kupinga ukatili kwa wanawake na watoto katika ukumbi wa Bwalo la polisi Dodoma.(Picha na John Banda)
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi David Misime akiongea jambo wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili kwa wanawake na watoto yaliyofanyika Bwalo la polisi Dodoma.
 Kamanda wa polisi wilaya ya Dodoma mjini Malingumu akizungumza akizungumza katika maadhimisho hayo.
 Staff Sajent Mwanajuma Mtuli wa polisi Dodoma akisisitiza jambo kwenye ufungaji huo wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili kwa wanawake na watoto.
 Baadhi ya Askari wakifuatilia jambo kwenye kilele hicho.

Wakina mama wajawazito wa wodi ya chikande walioalikwa kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukeketaji kwa wanawake na watoto uliofanyika katika Bwalo la polisi Dodoma.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

HOSPITALI MVUMI HAINA MASHUKA

HOSPITALI Teule ya Mvumi iliyoko wilayani Chamwino, inakabiliwa na upungufu wa mashuka, magodoro na dawa mbalimbali.

Akizungumza na Tanzania Daima juzi, Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Makundi Godfrey, alisema magodoro, mashuka na dawa katika hospitali hiyo ni tatizo na kusababisha wagonjwa kupata shida.

Kutokana na tatizo hilo, wakati mwingine wagonjwa wanaolazwa hapo wanalazimika kuja hospitali na mashuka yao.

Pamoja na kuwapo kwa uhaba wa dawa na vitendea kazi, bado wagonjwa wamekuwa wakiongezeka, jambo linaloongeza tatizo kwa wauguzi na waganga.

Kutokana na tatizo hilo, Mbunge wa Mtera, Dk John Malecela, alitoa vyandarua 100 kwa ajili ya wagonjwa na kina mama waliojifungulia hospitalini hapo.

Dk Malecela alisema vyandarua hivyo vinatakiwa kutumika kwa walengwa, badala ya kutumiwa na wafanyakazi wa hospitali hiyo, kwani iwapo vyandarua havitawafikia walengwa ni wazi kampeni ya kutokomeza malaria haitafanikiwa.
 Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WANACHUO WAWILI WA CHUO CHA ELIMU YA BIASHARA (CBE) DODOMA WAPATA GPA YA 4.9‏

Bw. Peragius  Cosmas mwanafunzi aliyehitimu shahada ya Uhasibu na kupata  GPA 4.91 akipokea cheti cha pongezi kutoka kwa Mkuu wa Chuo cha CBE Prof.Emanuel Mjema.
Bi. May Issa  mwanafunzi aliyehitimu shahada ya kwanza ya Usimamizi wa manunuzi  na kupata  GPA 4.92 Akipokea cheti cha pongezi kutoka kwa Mkuu wa Chuo cha CBE Prof.Emanuel Mjema.



Kwa kile ambacho kimeonekana ni tishio kwa chuo cha Elimu ya Biashara (CBE)  wanafunzi hawa  kutoka kampasi ya Dodoma  wameweza kupata ufaulu mkubwa katika masomo yao.

 Bi. May Issa  Mwanafunzi  aliyehitimu shahada yake ya kwanza ya Usimamizi wa  Manunuzi  katika mahafali ya 49 ya chuo cha Elimu ya Biashara CBE Dodoma mwaka 2014 ametangazwa  kuwa mwanafunzi wa kwanza aliyeongoza kwa ufaulu kwa kupata GPA ya  4.92. ambapo  aliweza kupata alama  A  28 , alama  B+ tatu  na  alama  B  moja  kati ya masomo  32  ya shahada yake ya kwanza  ya  Usimamizi wa manunuzi akifuatiwa na  Bw. Peragius Cosmas  aliyepata GPA ya 4.91.

 Kwa upande  wake Mwanafunzi mwingine  Bw, Peragius Cosmas  aliye kuwa akisoma Shahada ya kwanza ya Uhasibu   yeye pia alionyesha maajabu kwa kuweza kupata GPA ya  4.91  ambapo aliweza kupata alama  A  29 na  alama  B+ tatu    kati ya masomo  32  ya shahada yake ya kwanza  ya  uhasibu.

Hivi  karibuni katika Chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM)  pia tulishuhudia  Msichana   Doreen Kabuche aki ]ongoza kwa ufaulu UDSM kwa kuwa  Mhitimu bora wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2014, Doreen Kabuche alitangazwa kuwa kinara kwa ufaulu kwa kupata alama A 32 na B+ sita kati ya masomo 38 ya shahada ya Takwimu Bima (Actuarial Science). Kwa alama hizo, Doreen alipata wastani wa alama za ufaulu (GPA) 4.8 na kuacha alama ya 0.2 ili kufikia kiwango cha juu kabisa cha ufaulu cha alama tano,



 Bi. May  Issa akionekana mwenye furaha siku ya mahafali  ya 49 iliyofanyika hivi karibuni katika chuo cha Elimu ya biashara kampasi  ya Dodoma.
Bw. Peragius Cosmas akionekamna mwenye furaha  katika mahafali ya  49 ya  chuo cha CBE iliyofanyika hivi karibuni katika  Chuo cha Elimu ya Biashara kampasi ya Dodoma.
  Rais mstaafu wa Serikali ya Wanafunzi CBE  kampasi ya Dodoma 2013/2014 Bw. Remidius Emmanuel (kulia) akimpongeza  Bi. May  Issa kwa kufanya vizuri katika  masomo yake  kwa kipindi chote cha masomo yake.


Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

SAKATA LA ESCROW: KAFULILA: NILITISHWA SANA, SASA YAMETIMIA

 SIKU moja baada ya Bunge kupitisha maazimio nane ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (PAC), kutokana na sakata la uchotaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, Mbunge wa Kigoma Kusini, Bw. David Kafulila (NCCR-Mageuzi), ameweka wazi usumbufu alioupata katika sakata hilo.

Akizungumza na Majira jana, Bw. Kafulila ambaye ndiye aliyeliibua sakata hilo bungeni, alilishukuru Bunge kwa hatua waliyochukua baada ya kupokea ripoti ya PAC, kuijadili na kufikia uamuzi wa kuchukua hatua kwa wahusika.

Alisema baada ya kuibua ufisadi huo bungeni, aliingia katika vita kubwa na wabunge waliokuwa wanatumiwa na mafisadi pamoja na mafisadi wenyewe.

"Kutokana na vitisho nilivyokuwa nikivipata katika simu yangu ya mkononi na mitandao mingine, niliishi kwa tabu Mjini Dodoma nikibadili hoteli...sikuishia hapo bali nilikwenda polisi Dodoma mara mbili," alisema.

"Nilikuwa nakunywa kwa uangalifu sana hasa nikiwa Dodoma ingawa hata Dar es Salaam nilichukua tahadhari, ninachoweza kusema, ufisadi huu ni mkubwa uliohusisha mfumo mzima serikalini," alisema Bw. Kafulila.

Aliongeza kuwa, hatua tulizochukua kama Bunge zinaweza kuonekana kutosha kwa Bunge changa kama hilo lakini kwa mabunge yaliyokomaa, sakata hilo lilitosha kuiingiza nchi katika Uchaguzi Mkuu.

"Ni vyema Rais Jakaya Kikwete asafishe watendaji wake Ikulu ili aweze kuendesha nchi kwa misingi ya sheria na utawala bora...Benki ya Stanbic lazima warudishe fedha kwa kushiriki utakatishaji fedha haramu.

"Huu ni utaratibu wa kimataifa kama ilivyokuwa nchini Nigeria ambapo Stanbic imeingia kwenye kashfa ikidaiwa kushiriki utakatishaji fedha takriban dola za Marekani bilioni nane," alisisitiza Bw. Kafulila.

Juzi sakata hilo lilihitimishwa katika hatua nzuri bungeni baada ya Bunge kuazimia viongozi wote waliotajwa katika ripoti ya CAG wakihusishwa na sakata hilo, wawajibishwe.

Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Bw. Zitto Kabwe, alisema maazimio hayo yamefikiwa na Kamati ya Maridhiano katika kikao kilichoshirikisha Kambi ya Upinzani, CCM na Serikali.

Alisema Bunge hilo limeazimia mamlaka ya uteuzi iwawajibishe na kutengua uteuzi wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliachim Maswi na wajumbe wa Bodi ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO).

Maazimio mengine ni Rais kuunda tume ya kijaji ili kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Euden Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Mengine ni mamlaka husika za kifedha na kiuchunguzi ziitaje Benki ya Stanbic Tanzania Ltd na benki nyingine yoyote itakayogundulika kujihusisha na utakatishaji fedha zilizotolewa katika akaunti hiyo kuwa ni taasisi za utakatishaji fedha haramu.

Bw. Kabwe aliyataja maazimio mengine kuwa Serikali iandae na kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria iliyoiunda Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), kwa lengo la kuanzisha taasisi mahususi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa Taifa.

Pia walishauri Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO ili kuokoa fedha za shirika hilo na Serikali iwasilishe taarifa za utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme kabla ya kumalizika mkutano wa Bunge la Bajeti.

Azimio lingine Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, viwachukulie hatua stahiki za kisheria watu wote waliotajwa katika taarifa maalumu ya kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya akaunti hiyo na wengine ambao watagundulika kuhusika katika vitendo hivyo kutokana na uchunguzi unaoendelea.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MJADALA WA ESCROW: BUNGENI VURUGU TUPU

 MJADALA kuhusu ripoti ya uchunguzi wa fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow iliyowasilishwa bungeni Mjini Dodoma na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na utetezi wa Serikali kuhusu sakata hilo, jana umewagawa wabunge.

Ripoti ya PAC inatokana na uchunguzi uliofanywa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambapo mjadala huo ulianza jana jioni ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bunge ambaye ni Mbunge wa Ilala, Bw. Mussa Azzan Zungu.
 Kabla ya kuanza mjadala huo, Bw. Zungu aliwataka wabunge kuijadili ripoti hiyo kwa utulivu na kuvumiliana lakini hali ilikuwa tofauti na maombi yake.

Wabunge waliokuwa wakichangia mjadala huo, walitofautiana kimtazamo juu ya sakata hilo baadhi yao wakitaka viongozi waliotajwa wawajibishwe na wengine wakipinga.
Mbunge wa Singida Mashariki, Bw. Tundu Lissu (CHADEMA), alisema wanaotajwa katika ripoti hiyo lazima waachie ngazi kuanzia Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema pamoja na viongozi wengine.

Alijenga hoja kuwa fedha za Akaunti ya Escrow hazikuwa binafsi kwani haiwezekani fedha binafsi zipate maelekezo ya kutolewa kwenye akaunti kwa ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwenda Ikulu.
Alisema barua ya kutolewa fedha hizo kwenye akaunti hiyo iliandikwa na Ikulu kwa niaba ya Rais wakati fedha binafsi haziwezi kutolewa maelezo na Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mwanasheria wa Serikali wala Ikulu.

Aliongeza kuwa, kwa msingi huo fedha hizo zilikuwa za umma hivyo waliohusika kuanzia Waziri Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mawaziri na wabunge, wawajibishwe na kuwajibika.
Bw. Lissu alienda mbali zaidi akimtaka Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa Taifa kuwajibika kwani haiwezekani miamala ya fedha ifanyike bila wao kujua kinachoendelea.

"Wale wanaodai fedha hizo si za umma ni wale waliohongwa," alisema Bw. Lissu na kuongeza kuwa, wote waliotajwa kupokea mgawo wa fedha hizo wakiwemo watumishi wa Serikali wamelitia aibu Taifa.
Mbunge wa Muleba Kaskazini, Bw. Charles Mwijage (CCM), alisema jambo sakala hilo ni zito lakini kwa kuwa Kamati ya PAC imelifikisha mbele ya Bunge, linapaswa kufanyiwakazi na maamuzi magumu yatolewe na wabunge wote.

Alisema tangu kuanzishwa IPTL mwaka 1994, haoni sababu ya mtu kama Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Stephen Massele, kuambiwa awajibike kwa sababu ya kumsema Balozi wa Uingereza na kusisitiza Bunge linapaswa kuondoa kibuyu ambacho kimekuwa mzigo.
Aliongeza kuwa, katika ripoti ya CAG haoni sehemu ambayo Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, anaguswa na kutakiwa kuwajibika na mapendekezo ya PAC kutaka mitambo ya IPTL itaifishwe, alionya wabunge kuwa makini kwani kufanya hivyo ni kubeba mzigo wa deni linalodaiwa na Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong.

Alisema deni hilo linatosha kununua mtambo mpya ukafungwa Kinyerezi na kazalisha umeme mwingi zaidi ya ule wa IPTL.
Chanzo;Majira
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WANASHERIA WACHARUKIA MADAI YA RUSHWA BUNGENI

KAULI ya Spika wa Bunge, Anne Makinda ya kuwataka wabunge kuacha kujihusisha na vitendo vya rushwa vinavyoweza kuwaingiza matatani, huku akionya watakaokutwa na hatia wataibeba misalaba yao, imepongezwa na wanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na kutaka hatua zaidi za kiuchunguzi kuwabaini wahusika.
Makinda, alitoa onyo hilo Jumamosi usiku kabla ya kuahirishwa kwa Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge mjini Dodoma ambapo aliwataka wabunge kuachana na watu wanaofanya ushawishi kwa kutumia fedha ili kupenyeza hoja zao.
Pongezi za LHRC zilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho ya Sera LHRC, Harold Sungusia wakati akitoa tathmini ya mwenendo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na jinsi lilivyoshughulikia sakala la uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
“Kuna tuhuma za wabunge kutokuwa wasafi na kwamba baadhi yao wamekuwa wakituhumiwa kupewa rushwa ili kushinikiza maamuzi yasiyo na tija kwa taifa,” alisema Harold na kuongeza kuwa wanapongeza kauli ya Makinda kwa kuweka wazi suala hilo kwani si la kuachwa lipite, bali uchunguzi wa kina ufanyike kuwabaini wabunge wenye tabia za aina hiyo.
Alisena LHRC inazitaka mamlaka zenye dhamana ya kuchunguza mambo ya rushwa kulifuatilia jambo hilo na wale wote watakaobainika wachukuliwe hatua inayostahili kwa mujibu wa sheria.
Kadhalika alisema LHRC inalishauri Bunge kuichukulia uzito wa pekee kauli hiyo kuhusu baadhi ya wawakilishi hao wa wananchi waliopokea fedha ili kushawishiwa kupindisha ukweli na kisha Bunge liwachukulie hatua za kinidhamu ikibidi kuwafukuza ubunge.
Kuhusu uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Escrow alisema hilo ni jambo kubwa kuliko yote na kwamba ni kipimo cha maadili ya uongozi ambapo kwa Katiba ya sasa inatoa mianya mingi ya kutozingatiwa kwa miiko ya uongozi hasa baada ya kufutwa kwa azimio la Arusha.
Kuhusu majaji kutajwa katika sakata hilo, Ofisa Programu Dawati la Serikali, Hussein Sengu alisema suala hilo linaweza kuleta athari kwa wananchi kwa kukosa imani na vyombo hivyo na wengine kutumia Mahakama kama kichaka cha kuficha maovu.
Spika wa Bunge, akizungumza mjini Dodoma, alikemea suala la rushwa miongoni mwa wabunge akisema vitendo hivyo vinawaaibisha na vitawandolea uadilifu wao katika kuisimamia Serikali.
“Kuna hili la lobbying (kushawishi) linalofanywa na wafanyabiashara. Acheni kupokea rushwa, mtaaibika. Kama ninyi sio wasafi, mtawezaje kuwasimamia wengine,” alisema Makinda.
“Hakika mtajikuta mko ndani, na sisi hatutakuja kuwasaidia. Kama chombo hicho cha kuwasimamia wananchi kitaoza, nani atawasimamia wananchi? “Wananchi wanatutegemea sisi kwa hiyo acheni vitendo hivyo, vitawaaibisha na mtatiwa ndani na mimi sitakuja kuwatoa. Kataeni vitendo hivyo,” alisisitiza Spika Makinda.
Kauli yake imekuja baada ya kuwapo kwa madai ya matumizi makubwa ya rushwa katika sakata la akaunti ya Tegeta Escrow ya BoT, ambayo ilikuwa mali ya Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Wakati wa majadiliano ya sakata hilo linalohusisha uchotaji wa Sh bilioni 306 zilizokuwa katika akaunti hiyo, baadhi ya wabunge waliwatuhumu wenzao kwa kuhongwa ili kufanikisha njama za ama kuwatetea watuhumiwa au kuwakandamiza watu wasiohusika.
Miongoni mwa waliohusishwa na sakata hilo ni viongozi wa umma, watendaji wa serikali, wafanyabiashara, majaji, ambao inaaminika kwa namna moja au nyingine walihusika kufanikisha uchotaji huo wa fedha na wengine kunufaika na fedha hizo.
Alipochangia mjadala huo, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), alisema sakata hilo linasukumwa na makundi manne (ingawa baadaye aliongeza moja).
Lusinde aliyataja kuwa ni wanasiasa wenye ndoto za kuwania urais mwakani, walionufaika na fedha hizo, waliokosa fedha hizo, mawakili waliokuwa wakipata fedha nyingi kutokana na malipo ya kesi mbalimbali za IPTL na benki zilizotaka kununua hisa za kampuni hiyo ya Tegeta Salasala, Dar es Salaam.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Chanzo:Habari Leo

HONGERA MWALIMU WANGU DR NELSON ISHENGOMA KWA KUHITIMU MASOMO YA SHAHADA YA UDAKTARI.


Dr Nelson Ishengoma akiwa katika pozi mara baada ya kutunukiwa shahada yake ya udaktari katika Mahafali ya Tano ya Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) yaliyofanyika jana katika viwanja vya Chimwaga vilivyopo Chuoni hapo.
 Hongera sana Mwalimu wangu na sasa Mwanzo wa Jina linaanza na Dr. Sio kazi rahisi lakini Mungu ameweza kukusimamia na kukuongoza. Nakuombea kwa Mungu ufanikiwe zaidi na zaidi. Kutoka Kwa Mwanafunzi wako  Josephat Lukaza
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa