Home » » CCM: HUKUMU CHENGE, TIBAIJUKA, MWEZI UJAO

CCM: HUKUMU CHENGE, TIBAIJUKA, MWEZI UJAO

 
Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec), Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.
 
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewaweka kiporo makada wake wanne, akiwamo aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka na wenzake watatu waliotajwa kuhusika katika kashfa ya kupata mgawo wa fedha zilizochotwa kifisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Wengine waliotajwa kupata mgawo katika fedha hizo sambamba na Prof. Tibaijuka, ni wenyeviti watatu wa kamati za Bunge; Andrew Chenge (Bajeti), William Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala) na Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini), ambao wote hatima yao sasa itajulikana mwezi ujao.

Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec), Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema kwa mujibu wa taratibu za chama hicho, taarifa za kilichotokea kwenye kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili hazipaswi kutolewa kwa umma au kutangazwa mpaka baada ya kufikishwa kwenye Kamati Kuu ya chama hicho.

 Nape alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari katika Ofisi Kuu za CCM Kisiwandui visiwani hapa jana.

Alisema kumekuwapo na harakati nyingi katika vyombo vya habari na kwa watu mbalimbali kujaribu kupata taarifa ya nini kimetokea kwenye kikao hicho cha maadili.

Kutokana na hali hiyo, aliitaka jamii kutulia na kusubiri taarifa rasmi baada ya kufikishwa kwenye Kamati Kuu badala ya kuhangaika, kwani habari zilizotolewa kuhusu kikao hicho siyo za kweli.

Hata hivyo, alisema Kamati Kuu inatarajiwa kukutana mwezi ujao kujadili na kuchukua hatua, ikiwamo hatima ya makada sita wa CCM waliopewa karipio na kusimamishwa kushiriki au kugombea nafasi kwa mwaka mmoja na kuwekwa chini ya uangalizi baada ya kutiwa hatiani kwa kujihusisha na kampeni za urais kabla ya wakati.

Makada hao ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Steven Wasira; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba; Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.

Aidha, Nape alisema licha ya Kamati Kuu kupitisha ratiba ya shughuli za kawaida za chama kwa mwaka huu na kupanga kushughulikia ratiba ya mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM katika vikao vijavyo, bado kumekuwapo na harakati nyingi zisizo halali kwa wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali, hasa za urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema licha ya makada hao kutahadharishwa mara nyingi juu ya madhara ya harakati hizo kwa umoja na mshikamano wa chama, bado baadhi yao wamekuwa wakiziendeleza.

Nape alisema kwa muda mrefu kumekuwapo na uzushi mwingi juu ya baadhi ya wanaotaka kuwania nafasi hizo kujadiliwa na hata kuchukuliwa hatua na vikao vya chama.

Alisema maneno hayo yamekuwa yakisambazwa na makada hao wenyewe au wapambe wao.
“Uzushi huu hauna nia njema kwa CCM. Una lengo la kukigawa chama na kuonesha kama vile chama hakina kazi nyingine ila kujadili na kushughulika na watu hao,” alisema Nape.

Alisema CCM inawatahadharisha makada wanaowania mbio za urais pamoja na wapambe wao kujiepusha kusambaza taarifa zisizokuwa za kweli, kwani vitendo hivyo vinakigawa chama.

Nape alisema CCM haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya wote wanaosambaza taarifa hizo.

Aliwataka makada hao kuwadhibiti wapambe wao na kujichunga wenyewe dhidi ya hujumu hizo kwa chama, kwani zitawapotezea sifa ya kugombea.

“Wengi wanaosambaza taarifa hizi ni wagombea au wapambe wao wasiojiamini kutokana na matendo yao, ambayo hata wao wana mashaka na uadilifu wao. Hatuoni sababu ya mgombea anayefuata sheria, kanuni na taratibu za chama kuhofia kuchukuliwa hatua kila vikao vya chama vinapofanyika,” alisema Nape.

Aliwataka makada hao kuwa endapo wakitenda haki hakuna haja ya kuogopa vikao na kuzusha uongo na uzushi usio na ukweli na CCM inaamini matendo hayo hayatajirudia tena.

Pia aliwataka wanachama na wananchi kupuuza taarifa zinazosambazwa kwa kunukuu vyanzo visivyo rasmi na kama kuna hatua au taarifa kwa umma juu ya hatua yoyote katika mchakato huo itatolewa na wasemaji halali wa chama.

 
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa