Home » » CUF:GHASIA AJIUZULU

CUF:GHASIA AJIUZULU

  Ni kufuatia dosari chaguzi Serikali za Mitaa
fisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia.
Chama cha Wananchi (CUF), kimesema  endapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, hatajiwajibishwa kwa kujiuzulu, watatumia Bunge lijalo kumuondoa madarakani.
Bunge la kwanza mwaka huu linatarajiwa kuanza Januari 27  mjini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara , Magdalena Sakaya, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa wanahabari  na kueleza kuwa, vurugu, fujo na hujuma dhidi ya wapinzani zilizotokea katika uchaguzi wa serikali za mitaa, mwezi uliopita  chanzo chake ni waziri huyo.

Sakaya alisema yaliyotokea katika uchaguzi huo hadi kutangazwa baadhi ya watu ambao hawajashinda kwenye baadhi ya mitaa ni moja ya janja ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na serikali kuhujumu upinzani.

“Tunashangaa kwa nini eneo ambalo kilishinda CCM hawakumtangaza mshindi kutoka NCCR-Mageuzi, Chadema au CUF  badala yake maeneo tuliyoshinda upinzani, CCM na serikali yake imekuwa ikitumia mabavu kutangaza watu wasio washindi,” alisema na kuongeza:

“Wanaleta uhasama na chuki kwa wananchi, yote haya yametokea lakini serikali imekaa kimya, sio waziri Ghasia wala serikali yake, tunajua upo mkono wa serikali katika hili, kuwawajibisha wakurugenzi peke yao haitoshi hawa walikuwa wanapata mashinikizo toka juu,” alisema.

Pia alisema CUF inamtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni naye ajiuzulu  kwa kushindwa kuendesha uchaguzi huo.

Aliongeza kuwa, kwa sasa CUF pamoja na Umoja wa Katiba ya Wananchi, (Ukawa), wanasubiri waziri huyo ajiwajibishe au awajibishwe na Rais Jakaya Kikwete.

“Endapo hili litashindikana tutatumia bunge lijalo kushinikiza waziri huyu ajiuzulu,” alisema.

Alisema Ukawa unatarajiwa kukutana leo ambapo pamoja na mambo mengine wataangalia nini kifanyike kuhusiana na hujuma iliyotokea wakati wote wa uchaguzi wa serikali za mitaa ulipoanza hadi kutangazwa kwa baadhi ya watu wa CCM kuwa ni washindi wakati si kweli.

Sakaya alisema kuwa, yaliyofanyika kwenye uchaguzi huo ni kiashirikio tosha kuwa, uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu utatikisa  nchi.
 “CCM ndiyo watakaoangamiza taifa hili, hiki wanachokifanya sasa ndiyo mikakati yao uchaguzi ujao, wamejiandaa kupora ushindi wa Ukawa kwa kutumia vyombo vya serikali pamoja na vile vya dola,” alisema na kuongeza:

“Napenda kuwaeleza kuwa, moto tuliowaonyesha kwenye uchaguzi huu ni sawa na fukuto tu, tumejipanga zaidi ya tulivyowadhibiti kwenye mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa na uapishwaji ndivyo mbinu zaidi za kuwabana kwenye uchaguzi mkuu zinavyopikwa,” alisema.

Aliieleza CCM kuwa, nguvu ya Umma waliyokutana nayo kwenye uchaguzi huo itaongezeka zaidi kwenye uchaguzi ujao.

Alitaja baadhi ya mitaa ambayo wana taarifa za kuvurugwa zoezi la kuapishwa kuwa ni Mwinyimkuu kata ya Mzimuni, Mkwamani kata ya Kawe na Msisili A kata ya Mwananyamala.

Mitaa mingine ni Kigogo Freshi, Malapa na Kiwalani kata ya Magomabani, Kinyerezi, Mgobani, Bunda (Mara) na maeneo mengine ambayo wanaendelea kupokea taarifa zake.


CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa