Wajumbe wa kamati tatu za Kudumu za Bunge
ambazo wenyeviti wake wanatakiwa kuvuliwa nyadhifa zao kutokana na
kuhusika katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow, ‘wanasuasua’
kuwaondoa na kuchagua viongozi wengine.
Kwa nyakati tofauti wajumbe
wa kamati hizo ambazo ni Bajeti, Nishati na Madini na Katiba, Sheria na
Utawala wamekuwa wakishangazwa na hatua za wahusika hao kuendelea
kujitambulisha kuwa ni wenyeviti, sambamba na kuongoza vikao vya kamati
hizo, wakati wakijua wazi kuwa hawatakiwi kufanya hivyo.
Wenyeviti wanaotakiwa kuachia
nyadhifa zao ni Victor Mwabalaswa (Nishati na Madini), William Ngeleja
(Katiba) na Andrew Chenge (Bajeti).
Katibu wa Bunge, Dk Thomas
Kashilillah aliliambia gazeti hili jana kwamba jukumu la kuwaondoa
wenyeviti hao lipo mikononi mwa wajumbe wa kamati hizo, kwamba kama
wakishindwa Spika wa Bunge atachukua jukumu hilo.
Katika mkutano wake wa 16 na
17, Bunge liliazimia kuwa watu walioshiriki katika kashfa ya miamala ya
Akaunti ya Escrow wakiwepo viongozi wa Kamati hizo tatu, wachukuliwe
hatua za haraka na Kamati husika za Bunge kabla ya kuanza kwa mkutano wa
18 wa Bunge unaotarajiwa kuanza Januari 27 mwaka huu.
Akinukuu azimio hilo
Kashilillah alisema, “Wajumbe husika ndiyo wanaotakiwa kuwaondoa
wenyeviti hao, hilo ni lazima mlitambue jamani. Waulizeni ni lini
watafanya hivyo.”
Alisema ndiyo maana kamati ikiwa haina
mwenyekiti, wajumbe wenyewe huchagua mmoja kati yao kwa ajili ya
kuongoza kikao cha kamati.
“Spika hawezi kumwondoa
mwenyekiti wa kamati husika, anachoweza kufanya Spika ni kumhamisha
mwenyekiti kutoka kamati moja kwenda nyingine. Akifanya hivyo maana yake
ni kwamba mwenyekiti husika anapoteza sifa za kuwa mwenyekiti,”
alisema.
Alisema jambo hilo Spika
Makinda anaweza kulifanya kama wajumbe wa kamati hizo tatu zitashindwa
kuchagua wenyeviti wengine mpaka kufikia siku ambayo utaanza mkutano wa
18 wa Bunge.
Kuhusu Chenge ambaye
aliteuliwa na Spika Makinda kuwa mwenyekiti wa kamati ya Bajeti alisema,
“Chenge aliteuliwa katika kipindi cha mpito ambacho kikiisha
atachaguliwa mwenyekiti mwingine. Hivyo naye anaweza kuondolewa tu na
wajumbe wa kamati.”
Mvutano katika kamati
Taarifa kutoka ndani ya
kamati ya Bajeti zilieleza gazeti hili kwamba, juzi kamati hiyo
ilikutana na Wizara ya Maji na Uchukuzi na Chenge alijitambulisha kama
mwenyekiti, jambo ambalo liliwashangaza wajumbe wa kamati hiyo.
“Tumeshangazwa jinsi alivyojitambulisha kwa
sababu awali kamati tulikubaliana kuwa akae pembeni na kumwachia makamu
mwenyekiti, Dk Limbu (Festus) kuongoza vikao vya kamati. Inavyoonekana
ni kama anang’ang’ania nafasi hii,” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati
hiyo.
Mjumbe mwingine wa kamati
hiyo alisema, “Ilitushangaza kwa sababu Dk Limbu alikuwapo na kamati
ndiyo iliamua kuwa yeye awe mwenyekiti wetu kwa muda. Hili jambo
linatuchanganya na ni vyema likapatiwa ufumbuzi.”
Alisema wajumbe wa kamati
wanashindwa kuchukua hatua zaidi kwa sababu Chenge aliteuliwa kushika
nafasi hiyo na Spika wa Bunge, Anne Makinda na kwamba yeye ndiyo mwenye
mamlaka ya kumwondoa.
Mapema wiki hii, Dk Limbu
alikaririwa na gazeti hili akisema, “Suala la Chenge linasubiri uamuzi
utakaotolewa na Spika wa Bunge, Anne Makinda.
“Kamati imeamua kwa busara
Chenge akae pembeni na makamu mwenyekiti aongoze vikao huku ikisubiri
hatua atakazozichukua Spika (Makinda),”
Akizungumzia sakata hilo Makamu Mwenyekiti
wa kamati hiyo, Gosbert Blandes alisema kuwa wamekwama kutekeleza
maagizo ya Bunge ya kumuondoa kwenye madaraka Ngeleja, baada ya kukosa
mwongozo ndani ya kanuni.
“Kamati ilijadili kwa kina
suala hilo kwamba ni vipi tunaweza kulishughulikia, tulipata utata
mkubwa sana hatujaona kanuni ambayo tunaweza kuitumia, hivyo Ngeleja
anaendelea kuongoza vikao kihalali,” alisema Blandes.
Alisema bado hawajapokea
mwongozo wowote kutoka kwa spika, hivyo wanaendelea kusubiri huku
wakijadiliana kwa amani tofauti na inavyoripotiwa na baadhi ya vyombo
vya habari.
“ Kamati inaendeshwa kwa
mujibu wa sheria, hakuna mtafaruku wowote kwa pamoja tulijadiliana na
kuridhia mwenyekiti aendelee na majukumu yake hadi hapo tunakapopata
mwongozo,” alisema Blandes.
Kwa uapnde wake Mwabalaswa
alisema, “Kamati haina jukumu hilo ambalo Katibu (Kashilillah)
amekueleza, ila kama amekueleza hivyo sawa tu.”
Wabunge walia na Profesa Muhongo
Katika hatua nyingine wabunge walikosoa
kitendo cha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
kuendelea na kazi licha ya maazimo ya Bunge kuitaka mamlaka ya uteuzi
kumwajibisha.
Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo
Filikunjombe alisema, “Profesa Muhongo anaweza kuwa anafaa kufanya kazi
nyingine lakini si hii na naomba ieleweke kwamba maazimio yale si ya
Bunge bali ni ya wananchi hivyo lazima yakatekelezwa.”
Aliongeza: “Lakini atafanya kazi na nani (Muhongo)? Bajeti yake ataipitisha nani? Tutamwachia hatutampa ushirikiano.”
Filikunjombe ambaye ni Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya PAC alisema, “Profesa Muhongo anamwaibisha Rais
(Jakaya Kikwete) na anampa wakati mgumu sana.”
Mbunge wa Viti maalumu
(Chadema), Esther Matiko alisema, “Rais Kikwete alishasema kuwa fedha za
IPTL siyo za Umma hivyo kwa kauli yake hii ni dhahiri hatachukua
maamuzi ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge.”
“Ila cha kushangaza na kuona
jinsi hawa CCM wanacheza na akili za Watanzania, Swali la msingi fedha
si za Umma kwa nini wanatumia fedha za umma kushughulikia masuala
binafsi,” alisema Matiko.
Aliongeza: “Rais Kikwete kwa kofia ya
Mwenyekiti wa CCM wakiwa katika kikao cha Kamati Kuu yao huko Zanzibar
wamebariki utekelezaji wa maazimio ya Bunge...upande mmoja Rais Kikwete
anakana si fedha za umma upande mwingine anakubari maazimio ya Bunge hii
inawachanganya Watanzania na wasijue msimamo wa Rais Kikwete ni upi.”
Mbunge wa Iringa Mjini
(Chadema), Mchungaji Peter Msingwa alisema, “Kutochukua uamuzi ni
udhaifu wa taasisi ya Rais na ni ombwe la uongozi...ndiyo maana ana sita
sita kuchukua uamuzi.”
Mbunge wa Kasulu Mjini
(NCCR-Mageuzi), Agripina Buyogela alisema, “Ukimya wa Rais unatupa
mtihani ina maana hakuna mtu mwingine anayeweza kuwa Waziri wa Nishati
na Madini mpaka ang’ang’aniwe Profesa Muhongo.”
Mbunge wa Mgogoni (CUF),
Kombo Khamis Kombo alisema, “Ni jambo la dharau kwa wabunge na wananchi.
Haiwezekani yatolewe maazimio lakini hayatekelezwi. Huyo Muhongo
atachunguzwa vipi wakati bado anaendelea na wadhifa wake wa uwaziri.”
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment