Home » » TAMKO: MTANDAO WA WANAWAKE NA KATIBA WAWAKUMBUSHA WAKUU WA VYAMA VYA SIASA KUHUSU KUBEBA AJENDA YA USAWA WA JINSIA

TAMKO: MTANDAO WA WANAWAKE NA KATIBA WAWAKUMBUSHA WAKUU WA VYAMA VYA SIASA KUHUSU KUBEBA AJENDA YA USAWA WA JINSIA


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiDqX7IptxP7dUsyMWvgO79Awa31O78HDYWL90aAlR8GtmRWSLL13qXQqypbn9fsUsOOWkcvboXoorBZoBuMfxE0512drSXFtQH56E2uUH1mxxSO6ppnlJ4PaPMIy2KllNy41GpEpJ96X_N/s1600/PIX+16.JPG
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wakifuatilia Semina iliyoandaliwa na Mtandao wa Wanawake na Katiba kwaajili ya Wajumbe wa Bunge Maalum kuhusu masuala ya Jinsia na Katiba iliyofanyika Agosti, 2014 kwenye Ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa Mjini Dodoma.


Mtandao wa Wanawake na Katiba Tanzania unaounganisha wanawake kutoka asasi za kiraia za nyanja mbali mbali za kisiasa, kijamii na kiuchumi, unatambua jitihada zote zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa katika kuhakikisha kwamba Katiba Mpya ya Tanzania inajengwa katika misingi ya usawa wa jinsia. Kwa mtazamo wa Mtandao, Katiba Pendekezwa imejengwa katika misingi inayotambua  ulinzi wa utu, heshima na haki za wanawake  na hivyo inahitaji kuthaminiwa na kulindwa na wahusika mbalimbali, wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa nchini.  

Kwa mantiki hiyo ya kuhakikisha kwamba yaliyomo katika Katiba pendekezwa yanalindwa, Mtandao wa Wanawake na Katiba umekua ukifuatilia kwa makini mwenendo wa viongozi, na haswa viongozi wa vyama vya kisiasa katika matamko yao mbalimbali wanayoyatoa,  yakiwemo yale yanayohusu  mapendekezo ya kubadilisha sheria ya uchaguzi. 

Kwa mfano, viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa wamekuwa wakiikumbusha serikali kuzingatia katika mabadiliko ya Sheria mpya ya Uchaguzi, madai matano yakiwemo: Ushindi wa Mgombea Urais uwe wa kura za asilimia hamsini na zaidi, Nafasi ya Mgombea Binafsi itambuliwe, Tume Huru ya Uchaguzi iwepo na uwezekano wa kupinga matokeo ya uraisi mahakamani. 

Hata hivyo, matamko haya hayajumuishi kuingizwa kwa msingi wa usawa wa jinsia katika mabadilko ya Sheria yanayopendekezwa, pamoja na michakato mingine mbalimbali ya uchaguzi na matokeo yake. Mwenendo huu wa viongozi wa Vyama vya Siasa unatushangaza na kutuonyesha kuwa viongozi wengi wa kisiasa hawatilii maanani ajenda ya kuleta usawa wa jinsia katika uongozi wa nchi hii. Kwa maana hiyo, viongozi hawa wanaashiria  kutotambua mchango, nguvu, nafasi na haki wa mwanamke katika nyanja hii muhimu na hivyo kuduwazaa demokrasia na maendeleo ya nchi hii kwa ujumla.

Mtandao wa Wanawake na Katiba unawakumbusha na kuwataka viongozi hawa kutambua kwamba: 
·         Wanawake ni Zaidi ya asilimia 51% ya raia wa Tanzania ambao utawala wa nchi unawahusu.
·         Wengi wa wanachama wao ni wanawake, na hivyo wana nafasi kubwa ya kushawishi wananchi kutounga mkono itikadi, sera na mwenendo wa vyama vyao vya kisiasa;wanawake tumechoka kutumika na vyama vya siasa kama wapiga debe; wahamasishaji wa michangi ya vyama;
·         Wanawake ni idadi kubwa ya wapiga kura pamoja na watunzaji wakuu wa familia na amani ya nchi hii;
·         Vyama vya kisiasa visivyozingatia usawa wa jinsia na hivyo kuchochea sera za kibaguzi havina nafasi katika ujenzi wa taifa letu haswa kufuatia kukomaa kwa harakati za jinsia nchini
Hivyo basi, tunatoa rai kuwataka viongozi wa vyama vya kisiasa kuhakikisha wanazingatia yaliyomo katika Katiba pendekezwa na kuendelea kuyatetea huku wakihakikisha kwamba matamshi na sera za kibaguzi hazitavumuliwa.
# # #
Kama ungependa habari zaidi kuhusu mada hii, tafadhali wasiliana na TGNP ambao ni mojawapo wa wanachama wa mtandao kupitia +255754784050.


Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa