Home » » TUKISHIKA DOLA , SERIKALI ITAHAMIA DODOMA-ZITTO

TUKISHIKA DOLA , SERIKALI ITAHAMIA DODOMA-ZITTO

 
CHAMA cha ACT Wazalendo, kimesema kama wananchi watakipa ridhaa ya kuongoza dola katika Uchaguzi Mkuu ujao, kitaunda Serikali na kuwaapisha viongozi wake katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma ili kuhakikisha kuwa shughuli za Serikali zinahamia mkoani humo.

Kiongozi wa chama hicho, Bw. Zitto Kabwe aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Mashujaa, mkoani Dodoma na kuongeza kuwa, haiwezekani nchi ya Nigeria ifanikiwe kuhamisha Makao Makuu yake kutoka Lagos hadi Abuja; lakini Tanzania inashindwa.

Alisema ramani iliyotumika kujenga jiji la Abuja ndio iliyokuwa ya Tanzania, lakini Tanzania imeshindwa kuhamisha Makao Makuu ya Serikali kwenda Dodoma.

"CCM imewadanganya Watanzania kwa miaka mingi, Serikali inatumia gharama kubwa kuwalipa posho wafanyakazi wake kuja Dodoma ambako kuna ofisi zao na makazi yao.

"Katika orodha ya mikoa yenye maendeleo lakini inashika nafasi ya mikoa mitatu maskini ni pamoja na Dodoma ambao licha ya kuchangia pato la Taifa, inashangaza kuona kila Rais anapotakiwa aapishwe, huapisho huo hufanyika Dar es Salaam katika Uwanja wa Taifa," alisema Bw. Kabwe.

Katika hatua nyingine, chama hicho kimeahidi kujenga zahanati  kwenye Kijiji cha Chidilo, Kata ya Chipanga, Tarafa ya Mpalanga Wilaya ya Bahi, mkoani humo ambayo hadi kufikia Juni mwaka huu, itakuwa imekamilika.

Akitoa ahadi hiyo, Bw. Kabwe alisema sababu ya kujenga zahanati hiyo ni kutokana na wananchi wa kijiji hicho kukiamini na kuchagua Mwenyekiti wa kijiji kupitia chama hicho.

"Tutajenga zahanati hii kama zawadi kwenu kwa kutuamini na  kumchagua Mwenyekiti wetu anayetokana na ACT, pia tutafuatilia fedha zote kwa viongozi wa halmashauri hii ambazo mlichanga ili mjenge zahanati," alisema Bw. Kabwe.

Alisema inashindikana kujenga maisha bora kwa kila Mtanzania kwa sababu uchumi wa nchi unamilikiwa na watu wachache ambapo Bw. Kabwe pia alisimikwa kuwa Chifu na Mtemi wa Kabila la Wagogo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Bi. Anna Mghwira, alisema kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi ambapo mkoa huo ni moja kati ya mikoa yenye migogoro hiyo.

"ACT itahakikisha migogoro yote ya ardhi tunaikomesha mara moja bila kumuonea mtu haya," alisema Bi. Mghwira.

Katika hatua nyingine, chama hicho kimevuna wanachama  2,071 katika mikoa minne ambayo viongozi wake wamefanya
ziara kwa mara ya kwanza tangu waingie madarakani.

Katibu  Uenezi na Mawasiliano, Msafiri Mtemelwa, alisema mkoani Ruvuma wamepata wanachama 528, Njombe 26, Makambako 103, Mafinga 228, Iringa 471, Morogoro 715  ambapo hadi kufikia jana, kimevuna zaidi ya wanachama 3,000.


CHANZO GAZETI LA MWANANCHI

Ukiwa na tukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa