Na. Johary Kachwamba - MAELEZO, DODOMA
Serikali imewahimiza Wananchi kudai risiti pindi wanunuapo
mafuta kwenye vituo vya kuuza Petroli na Dizeli ili kurahisisha ukusanyaji wa
Kodi ya Mapato, Aidha kutokuchukua risiti ni kosa kisheria hivyo wote muuzaji
na mnunuzi wanastahili adhabu kwa mujibu wa sheria.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Nchemba amesema hayo bungeni
mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Rukia Ahmad, Mbunge wa Viti Maalum
aliyehoji kwanini Serikali isitoze kodi kwa jumla pale vituo hivyo vinaponunua
mafuta
Mhe. Nchemba amesema ulipaji wa kodi ya mapato hususani kwa
makampuni yanayouza mafuta unafuata mfumo wa wafanyabiashara kujikadiria
wenyewe na kulipa kodi kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato sura
132, kisha ukaguzi wa hesabu kufuata baadaye.
“baada ya kubaini kuwa kuna udhaifu katika utoaji risiti ambao
husababisha upotevu wa mapato, Serikali imeanzisha mfumo wa matumiz ya mashine
ya kodi ya kielektroniki kwenye biashara mbalimbali ikiwa ni pamoja na vituo
vya kuuza mafuta” Mhe. Nchemba
Hata hivyo mfumo wa matumizi ya mashine za kodi za kielektroniki
katika kutoa risiti za mauzo umetekelezwa kwa awamu mbili, awamu ya kwanza
iiwahusu wafanyabiashara waliosajiliwa na kodi ya ongezeko la thamani (VAT)
wakati awamu ya pili inahusu wafanyabiashara wengine waliobaki
“vituo vingi vya mafuta nchini havijasajiliwa na kodi ya ongezeko
la thamani (VAT) kwa kuwa mafuta ya Petroli na Dizeli hayatozwi kodi ya VAT”
aliongezea Mhe. Nchemba
Kodi za Ushuru wa bidhaa, ushuru wa mafuta na ushuru wa Petroli
hukusanywa Forodhani mara tu bidhaa hizi zinapoingizwa nchini, isipokuwa kwa
mafuta ya Petroli na Dizeli yanayoenda nchi za jirani. Kodi hizi ulipwa
forodhani na makampuni yanayoagiza mafuta ya Petrol na dizeli kwa kuzingatia
kiasi cha ujazo wa lita zilizoingizwa nchini kabla ya kuuza kwenye vituo vya
mafuta.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment