Home » » MBUNGE AFANYA IBADA KUFUTIWA KESI YA RUSHWA.

MBUNGE AFANYA IBADA KUFUTIWA KESI YA RUSHWA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mbunge wa Bahi (CCM), Omar Badwel.
Mbunge wa Bahi (CCM), Omar Badwel (pichani), amefanya ibada kubwa aliyoiita ya kumshukuru Mungu kutokana na kumsaidia kushinda kesi ya rushwa iliyokuwa ikimkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
 
Kesi hiyo ilikuwa ya madai ya kupokea rushwa ya Sh. milioni moja kutoka kwa aliyekuwa mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mkuranga.
 
Hata hivyo, Mahakama hiyo ilimwachilia huru Badwel Mei 29, mwaka huu ikieleza kuwa upande wa mashitaka yaliyofunguliwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (Takukuru) ulishindwa kuwasilisha ushahidi wa kuthibitisha tuhuma hizo na kumtia hatiani. Ibada hiyo ilifanyika jana katika viwanja vya Bahi sokoni  ilijumuisha madhehebu ya dini ya Kiislamu kutoka Wilaya ya Bahi wakiongozwa na  Shekhe wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Rajabu pamoja na viongozi wengi wa dini hiyo.
 
Akizungumza katika ibada hiyo, Badwel alisema ameamua kufanya hivyo kama ishara ya kumshukuru Mungu kwa kumsaidia kwenye hali ngumu aliyokabiliana nayo katika kesi hiyo.
 
“Kama mnavyojua, hakuna jambo dogo katika kesi inayokukabili, hata kama ni ya kusingiziwa lolote linaweza kutokea, unaweza ukahukumiwa kifungo au ukawa huru, lakini mimi namshukuru Mungu niliachiwa huru, hivyo ninamshukuru Allah,” alisema.
 
Aliwashukuru waumini wa dini zote kwa kumpa ushirikiano kwenye kazi za maendeleo jimboni  kwa  kipindi cha miaka mitatu ya kesi yake ilipokuwa ikiendeshwa. Badwel alisema kwa sasa atatumia muda mwingi kuwatumikia wananchi wa jimbo lake kwa kuchapa kazi na kwamba hatakuwa na muda wa malumbano ya kisiasa. Aidha, alisema baada ya ibada hiyo itafuatiwa na nyingine Jumapili ijayo itakayofanyika katika kijiji cha Mchito, wilayani hapa ikishirikisha madhehebu yote ya kikristo. Alisema ibada hizo zinafanyika katika viwanja vya wazi ili kila muumini na wananchi wengine wapate fursa ya kujumuika. 
 
Naye Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Rajabu alimshukuru Mbunge huyo kwa kufanya tukio hilo aliloliita kubwa na kuwa ni wachache wanaokumbuka kufanya hivyo.
 
“Angeweza kuishia kusema kuwa nimeshinda kwa juhudi  zake, lakini yeye ameamua kuujulisha umma huu kuwa Mungu alimsaidia. Hata katika afya ya akili na kimwili ingeweza kuyumba kama sio Mungu,” alisema.

CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa