Home » » Rais Nyusi awa Rais wa kwanza wa Msumbiji kulihutubia Bunge la Tanzania.

Rais Nyusi awa Rais wa kwanza wa Msumbiji kulihutubia Bunge la Tanzania.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Na: Immaculate Makilika  na Lydia Churi  - MAELEZO, DODOMA.

Rais  wa Jamhuri ya  Msumbiji  Mheshimiwa  Felipe Nyusi  amelihutubia Bunge la Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania  mapema leo mjini Dodoma, ambapo anakuwa ni  Rais  wa kwanza wa nchi hiyo  kulihutubia Bunge la Tanzania.

Rais Nyusi alisema ameamua kufanya ziara hii ya kwanza nchini na kulihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya kulihutubia Bunge lingine lolote la nchi nyingine kutokana na uhusianao  mwema ulipo baina ya nchi yake na Tanzania. “Nina furaha sana kwa uhusiano mwema wa nchi  ya Tanzania na Msumbiji ”, alisema Rais huyo.

Akimnukuu Baba wa Taifa Hayati  Mwalimu Julius Nyerere  Rais Nyusi alisema,  “Msumbiji ni jirani na ni nchi ndogo  hivyo  ni lazima iongeze  juhudi  ya kupigana hata baada ya  Uhuru,  tusisahau kamwe yale tuliyopitia  ili tuwe na Uhuru wa kweli ”.
Aliwataka wabunge wa  Tanzania kufanya kazi kwa pamoja  ili kuweza kupambana   na  adui  umaskini, na kuongeza kuwa  ameitembelea Tanzania   kuona  jinsi  ambavyo wanafanyakazi  ya  uzalendo kwa nchi yao.

Alitoa wito kwa  wabunge wa Tanzania kuchangia katika kuimarisha Uhusiano baina ya nchi hizi mbili na kuhakikisha wanapiga vita ufisadi na ugaidi ili  kuleta maendeleo na kujenga Amani kwa ukanda huu na Afrika kwa ujumla.

Aidha, Rais Nyusi  kabla ya kuhutubia Bunge akifuatana  na ujumbe wake kutoka Msumbiji  alitembelea  Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini  Dodoma ambapo alizungumza na   mwenyeji  wake  Mwenyekiti  wa CCM Taifa  Mheshimiwa  Dkt. Jakaya Kikwete na viongozi wa CCM Taifa  pamoja na viongozi wa Chama cha FRELIMO.

Rais Nyusi alisema anafurahishwa sana na ushirikiano mzuri  ulipo kati ya nchi hizi mbili tangu enzi za kupigania Uhuru, na kuahidi kuwa mawazo mazuri yaliyotolewa na  viongozi  wa mataifa haya mawili tangu uongozi wa Mwalimu Nyerere hadi Kikwete na  Samora Machel hadi Armando Guebuza  yatafanyiwa  kazi  ili hatimaye kusaidia kwa manufaa ya nchi hizi mbili.
Naye Rais Kikwete kwa Upande wake, alimshukuru  Rais  Nyusi kwa kutembelea Tanzania  mara tu baada  ya Kuchaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo  tangu achaguliwe ikiwa ni miezi 4 tu  iliyopita.

“Tulikua pamoja FRELIMO ilipoanzishwa, tulikua pamoja wakati  uhuru wa Msumbiji ulivyotishiwa na mabepari  naahidi kuwa   tutaendelea kuwa pamoja wakati wote, alisema Rais Kikwete.

Rais  Nyusi aliapishwa  kuwa Rais wa Jamhuri ya  Msumbiji  Januari 16, 2015 mara baaada ya Rais Armando Guebuza kumaliza muda wake. Rais Nyusi alianza ziara yake ya kikazi jijini Dar es Salaam  Mei 17, na baadae alitembelea  Visiwa vya  Zanzibar kabla ya kuhitimisha ziara yake  kwa kulihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  jijini Dodoma.


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa