Home » » WAKAZI: MIGOGORO YA ARDHI NI KIGEZO CHA KUWAPATA VIONGOZI UCHAGUZI MKUU

WAKAZI: MIGOGORO YA ARDHI NI KIGEZO CHA KUWAPATA VIONGOZI UCHAGUZI MKUU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Dodoma.
Migogoro ya ardhi wanayokabiliana nayo wakazi wa Kata ya Dodoma – Makulu, kwenye Manispaa ya Dodoma, imeelezwa kuwa itatumika kama kigezo kitakachotumiwa na wakazi hao, kuchagua viongozi katika ngazi za udiwani, ubunge na urais, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
 
Hayo yalielezwa na baadhi ya wakazi wa Mitaa ya Kisasa, Medeli na Bwawani, wakiwa kwenye ofisi za CCM za Kata ya Dodoma Makulu walipomsindikiza mtia nia ya kuwakilisha chama hicho katika uchaguzi wa diwani wa kata hiyo, Lazaro Chihoma, aliporejesha fomu.
 
“Wakazi wa mitaa karibu yote ya kata hii, tumekubaliana Chifu wetu (Chihoma) awe kiongozi wa kisiasa wa kata yetu, kwa sababu kwa muda mfupi ambao amekuwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Bwawani, ametetea haki zetu dhidi ya waliotudhulumu ardhi,” Mchungaji wa Kanisa la Mitume, Yohana Mabene, alieleza.
 
Naye George Michael, mkazi wa Mtaa wa Medeli, alisema mtaa huo hauna mwenyekiti kufuatia wananchi kugoma katika uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa nchini, kutokana na aliyekuwa mwenyekiti kwa zaidi ya miaka kumi, Stanley Chibwete, kudaiwa kuwa mgombea pekee aliyetakiwa kupigiwa kura.
 
Naye Chiloma ambaye pia ni chifu wa watu wa kabila la Kigogo, akizungumza mara baada ya kuwasilisha fomu za kuwania udiwani wa kata hiyo ambayo kwa sasa inaongozwa na diwani wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema ameridhia ombi la wananchi wa kata hiyo na aliahidi kuwatumikia bila kuwaangusha.
 
Alisema endapo atachaguliwa kuwa diwani wa kata hiyo, ataendelea kutumia njia ya mazungumzo na maafikiano, kati yake kwa niaba ya wananchi anaowaongoza pamoja na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa matumizi ya ardhi, kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake anayostahili.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa