Home » » Kikwete: Ukipiga kura ondoka

Kikwete: Ukipiga kura ondoka

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Rais Jakaya Kikwete.
Rais Jakaya Kikwete, amewaagiza Watanzania kuwa Oktoba 25, mwaka huu baada ya kupiga kura waende nyumbani kusubiri matokeo.
 
Amesema serikali haitavumilia wale watakaokaidi agizo hilo halali na kusababisha vurugu, badala yake watachukuliwa hatua za kisheria.
 
Kadhalika, alisema wasidanganyike na kuilazimisha serikali kufanya kile isichokitaka na kwamba kazi ya kulinda kura za wagombea wa nafasi mbalimbali itafanywa na mawakala waliteuliwa na wagombea hao.
 
Rais Kikwete alitoa agizo hilo jana mkoani Dodoma katika kilele cha mbio za Mwenge na maadhisho ya  kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu, Julius Nyerere.
 
“Naagiza Watanzania wenzangu, msidanganyike kwamba mkishapiga kura katika vituo vyenu msiondoke mfanye kazi ya kulinda kura, hilo siyo jukumu lenu, kila mgombea ana wakala wake anayefanyakazi ya kuangalia na kulinda kura… serikali haitavumilia kuona amani na usalama vinavurugwa, sheria itachukua mkondo wake, narudia tena ukishapiga kura usikae kwenye kituo, rudi nyumbani kasubiri matokeo,” alisema.
 
Aliongeza: “Kama mgombea umeweka wakala wako mzembe, hakuna wa kukufanyia kazi ya ulinzi na msiwadanganye wananchi kwamba wanawake wakishapiga kula warudi nyumbani na wengine wabaki kulinda kura, wanawachuuza msidanganyike.”
 
Akifafanua zaidi, alisema kila wakala katika vituo vya kupigia kura ana kitabu cha watu wanaostahili kupiga kura katika kituo husika kwa hiyo hakuna ubabaishaji kila kitu kinaeleweka.
 
Alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshatoa maelekezo ya kisheria kwamba baada ya kupiga kura watu waondoke, ni vizuri maelekezo hayo yakazingatiwa.
 
Akizungumzia usalama  siku ya kupiga kura, alisema serikali imejiandaa na kwamba katika kipindi chote cha uchaguzi hali itakuwa salama na watakaovunja sheria watakuwa wamefanya makosa ya jinai na sheria itachukua mkondo wake.
 
Akizungumzia kumbukumbu ya miaka 16 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, Rais Kikwete alisema hotuba zake mbalimbali zisipuuzwe na  usia wake kwa kuwa alisisitiza watu wasiwachague viongozi wasiokuwa na sifa, wapenda rushwa na wale wasiokuwa na nia njema na amani ya Tanzania.
 
RUSHWA
Alisema Mwalimu Nyerere, aliwausia Watanzania wawachague viongozi wanaokemea rushwa.
Alisema kuwa rushwa bado ni tatizo na kwamba wagombea katika uchaguzi wa mwaka huu wasiwe na kigugumizi mbele ya wananchi kuzungumzia namna watakavyoshughulikia rushwa.
 
“Wapo viongozi wanaowaomba ridhaa muwachague, wanakemea rushwa na wengine wanamung’unya kuhusu suala hilo kwa kuwa wana lengo la kwenda kutatua matatizo yao na siyo yenu, sisi Watanzania tumieni demokrasia tupate viongozi wazalendo,” alisema Rais Kikwete.
 
Aliwahakikishia wananchi kuwa serikali ijayo itapambana na rushwa kwa kasi kubwa.
Alisema zimebaki siku 10  za Watanzania kuwachagua viongozi kuanzia ngazi ya urais, ubunge na udiwani, hivyo kila mmoja anatakiwa kutumia demokrasia kwenda kupiga kura kumchagua kiongozi anayemtaka.
 
AFYA
Alisema serikali yake imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kukabiliana maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kwamba wazazi na walezi wajipange kuzungumza na vijana ili kupunguza kasi ya maambukizi kwa vijana nchini.
 
“Wazazi na walezi zungumzeni na vijana kuhusu kuepuka na kujitenga na masuala ya maambukizi ya VVU ili kupunguza wimbi la nguvu kazi ya leo na kesho kuingia kwenye wimbi hilo,” alisema.
 
Akizungumzia kuhusu malaria, alisema serikali ilisambaza vyandarua vyenye dawa nchi nzima na dawa mseto kwa ajili ya kukabiliana na maradhi hayo na kwamba maambukizi yameshuka hadi kufikia asilimia 51 na vifo vimepungua kufikia asilimia 70.
 
Kwa upande wa Zanzibar, alisema wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa na wamefikia asilimia 0.2 ya maambukizi.
Rais Kikwete alisema serikali imejenga kiwanda cha kuua viluilui vya malaria wanapozaliwa, wasiweze kukua na kusababisha maambukizi.
 
DAWA ZA KULEVYA
Kuhusu dawa za kulevya, alisema serikali yake imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwabana wauzaji na wasambazaji kwa kuwa zinaathiri sana vijana na kudhoofisha nguvu kazi ya leo na kesho.
 
Alisema walioathirika na dawa hizo wanaweza kutibiwa na kupona na kwamba serikali inaendelea kutoa huduma katika vituo vyake nchini kwa ajili ya tiba kwa warioathirika.
 
RC DODOMA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa, alisema kabla ya kilele cha maadhimisho hayo, vijana walifanya maonyesho ya ujasiriamali, pamoja na makongamano mbalimbali kuhusu afya zao na kuinuana kiuchumi.
 
WAZIRI MUKANGARA
Akimkaribisha Rais Kikwete, Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, alisema Mwenge ulitembelea wilaya zote na kuzindua miradi 1, 342 yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 463.5.
 
Alisema kwa mwaka 2016, sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge zitazinduliwa mkoani Morogoro na kuhitimishwa Mkoa wa Simiyu.
 
Sherehe hizo zilipambwa na watoto zaidi ya 1,000 wa halaiki kutoka shule za msingi na sekondari ambao walichora maumbo mbalimbali na vikundi mbalimbali vya utamaduni.
 
Aidha wilaya na taasisi mbalimbali zilitunukiwa vyeti vya kutambua michango yao mbalimbali katika shughuli za maendeleo.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa