Home » » Magufuli, hivi ndivyo mashangingi yanavyofilisi

Magufuli, hivi ndivyo mashangingi yanavyofilisi

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Utitiri wa magari aina ya VX-V8 na mengine ya aina hiyo maarufu kama ‘mashangingi’ huigharimu serikali mabilioni ya fedha kila mwaka na hiyo ndiyo sababu kubwa iliyomlazimu Rais Dk. John Magufuli kutangaza kuwa atadhibiti matumizi yake, imefahamika.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kwa kuhusisha taarifa kutoka vyanzo mbalimbali umebaini kuwa idadi ya mashangingi iliyopo serikalini yaweza kuwa takriban 2,778.

Kwa makadirio ya Nipashe, vyombo hivyo vya usafiri kwa maafisa wa juu wa serikali hugharimu taifa takribani Sh. trilioni 1.18 kwa ajili ya manunuzi peke yake huku kiasi kingine cha wastani wa Sh. bilioni 125.01 kikitumika kwa uendeshaji wake kwa mwaka.

Aidha, kiasi hicho cha makadirio ya fedha za kununulia mashangingi 2,778 peke yake (Sh. trilioni 1.18) ni sawa na misamaha yote ya kodi iliyotolewa nchini katika mwaka wa fedha wa 2013/14.

Kwa mwaka, kulingana na ripoti ya kamati ya Bajeti ya Bunge misamaha ya kodi nchini ilifikia kiwango cha juu cha Sh. trillion 1.18 kwa mwaka wa fedha wa 2013/14, sawa na asilimia 4.3 ya pato la taifa.

Kadhalika, jumla ya makadirio ya gharama za manunuzi na uendeshaji kwa mashangingi 2,778, yaani Sh. trilioni 1.31 ni sawa na asilimia 5.8 ya bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2015/2016 ya Sh. trilioni 22.4, kama ilivyowasilishwa bungeni Juni, 2015 na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum.

Katika uchunguzi wake, Nipashe imekadiria gharama ya mashangingi kwa kuchukulia kuwa mawaziri, naibu mawaziri, wakurugenzi wa idara na wakuu mbalimbali wa vitengo wizarani, wakuu wa mikoa; wakuu wa wilaya na makatibu tawala wa mikoa na wilaya ni miongoni mwa wale wanaoyatumia. Wengine waliokadiriwa kutumia mashangingi hayo, kwa mujibu wa uchunguzi wa Nipashe, ni pamoja na mameya wa manispaa, wakurugenzi wa majiji na baadhi ya wakurugenzi wa wilaya na pia wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kama Shirika la Umeme (Tanesco).

Akizungumza katika hotuba yake wakati akizindua bunge Novemba 20, 2015, Rais Magufuli alisema wazi kuwa serikali yake ya awamu ya tano itahakikisha kuwa inadhibiti matumizi ya magari ya kifahari kwa viongozi na watumishi wake waandamizi ili kuokoa matumizi makubwa ya fedha ambayo vinginevyo yangesaidia kuboreshwa kwa huduma za kijamii na kuwaondolea Watanzania baadhi ya kero zinazowakabili.

“Serikali ya awamu ya tano, itasimamia kwa karibu na kudhibiti ununuzi wa magari ya gharama kwa ajili ya viongozi na watumishi waandamizi wa Serikali. Kwa sababu unakuta mtu ni Injinia, unatakiwa uende ukakague barabara badala ya kuwa na pick-up, unataka kununua V-8. Sasa ni lazima tubadilishe huo mwenendo,” alisema Magufuli.

IDADI YA MASHANGINGI
Katika uchunguzi wake, Nipashe haikufanikiwa kupata takwimu rasmi za serikali kuhusiana na idadi ya mashangingi. Jitihada za kufuatilia katika Wizara ya Ujenzi ambako awali iliaminika kuwa ndiko takwimu za mashangingi zaweza kupatikana ziligonga mwamba baada ya mwandishi kuelezwa kuwa hivi sasa kila wizara husimamia yenyewe magari yake na ya taasisi zilizo chini yake.

Hata hivyo, uchunguzi binafsi wa Nipashe umebaini kuwa kwa nchi nzima, serikali kupitia wizara na taasisi au mashirika yake ya umma yakadiriwa kuwa na mashangingi 2,778.

Katika uchunguzi huo, Nipashe iliangalia muundo wa baadhi ya wizara na kuchukulia kuwa kila mkuu wa idara na kitengo hustahili kuwa na shangingi.

Katika uchunguzi huo, imebainika kuwa baadhi ya wizara zina viongozi wengi wanaotajwa kutumia mashangingi kutokana na upana wa shughuli zake kulinganisha na nyingine. Kwa mfano, muundo wa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano waonyesha kuwa kuna Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, wakurugenzi 11 wa idara/vitengo na wakuu wa seksheni 12.

Kwa sababu hiyo, Nipashe imekadiria kuwa wastani wa mashangingi yaliyopo kulingana na idadi ya wakuu hao yafikia 27, hapo achilia mbali wasaidizi wa wakurugenzi na wakuu wa vitengo ambao kama wakitumia mashangingi, wakichanganywa wanakuwa zaidi ya 50. Wizara ya Fedha yaonyesha kuwa kwa mpangilio kama huo, kuna watu takriban 52 wanaotumia mashangingi huku wizara nyingine zenye muundo usiokuwa mpana sana zikiwa na watu walau 10 wanaostahili magari hayo, baadhi wakiwa ni mawaziri, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu, wakurugenzi wa idara za rasilimali watu na utawala, wakurugenzi wa idara za fedha na wakurugenzi wa idara za mawasiliano.

Kwa sababu hiyo, Nipashe imekadiria kuwa kwa wastani, walau kila wizara ina mashangingi 10. Kwa sababu hiyo, kwa wizara zote 30, maana yake hadi sasa kuna jumla ya mashangingi 300 yanayotumiwa na vigogo katika wizara hizo.

Kadhalika, kwa mujibu wa Msajili wa Hazina, Lawrance Mafuru, hivi sasa idadi ya taasisi na mashirika ya umma ni 220. Nipashe inakadiria kuwa wakuu wa taasisi zote, wasaidizi wao pamoja na wakuu wa idara kama za utawala na fedha hutumia pia mashangingi aina ya VX-V8.

Hivyo, ikiwa kila taasisi au shirika la umma lina wastani wa viongozi 10 wanaotumia mashangingi, maana yake, kwa ujumla taasisi na mashirika yote ya umma nchini yana mashangingi 2,200. Makadirio hayo ni mbali na ukweli kuwa zipo taasisi na mashirika makubwa ya umma kama Shirika la Umeme (Tanesco) lenye mtandao mpana zaidi wa huduma zake nchi nzima na hivyo kuwa na viongozi wengi wanaostahili kutumia mashangingi, wakiwamo mkurugenzi mkuu, msaidizi wake, wakuu wa idara za fedha, utawala, mhasibu mkuu, idara za usambazaji, uzalishaji, masoko, mawasiliano na pia mameneja wa shirika hilo katika kanda na mikoa yote nchini.

Aidha, Nipashe imekadiria kuwa yapo mashangingi walau 62 yanayotumiwa na wakuu wa mikoa yote 31 nchini na makatibu tawala wa mikoa yao. Kadhalika, inakadiriwa kuwa yapo mashangingi 133 yanayotumiwa na wakuu wa wilaya na vile vile magari kama hayo walau 83 yakadiriwa kutumiwa na nusu ya idadi ya wakurugenzi wa halmashauri 166 zilizopo nchini pamoja na mameya wa manispaa, mameya wa majiji matano yaliyopo nchini na baadhi ya wenyeviti wa halmashauri za miji. Idadi hii yakadiriwa nusu kwa vile Nipashe imehakikishiwa kuwa siyo wakurugenzi wote wa halmashauri hutumia mashangingi.

Kutokana na makadirio hayo, ndipo Nipashe ilipopata makadirio ya jumla ya mashangingi yanayotumiwa na viongozi wa serikali nchini kote kuwa ni 2,778.

AINA YA MASHANGINGI
Kwa mujibu wa mtandao wa moja ya kampuni zinazoshughulikia mashangingi, ukubwa wa injini ya Land Cruiser VX ni CC 4,608 (LC 200 Petrol). Ulaji wake wa mafuta huwa ni lita moja kwa kilomita 4 hadi 5, kutegemeana na uendeshaji wa dereva na hali ya barabara. Tanki lake la mafuta lina uwezo wa kuchukua lita 138, likiwa na vyumba viwili ambavyo kimoja kikubwa huchukua lita 93 na kingine lita 45.

Mbali na magari aina hayo, yapo ya matoleo mengine kadhaa yenye sifa zinazotofautiana na mengine. Baadhi, yakiwamo aina ya LC 200 VX High Diesel ambayo hutumia dizeli na ulaji wake mafuta watajwa kuwa ni lita moja kwa kilomita nane kutegemeana na uendeshaji wa dereva kwani huweza pia kutembea umbali mfupi zaidi.

Chanzo kimoja kiliiambia Nipashe kuwa mashangingi aina ya LC 200 Petrol na mengineyo yanayotumia lita moja kutembea umbali wa kilomita 4 na tano hula mafuta zaidi kwa sababu yana mfumo wa mafuta wa kielektroniki na pia huwa na huduma mbalimbali zinazotumia mafuta na umeme maradufu kama vitoa hewa ya joto (heater) na viyoyozi.

“Magari haya yana viti vya watu nane, masofa yake ni ya ngozi na kwa kweli, ukipanda ndani yake ni raha tupu. Ni imara lakini yanastarehesha vile vile na ndiyo maana viongozi na watu wenye uwezo mkubwa kifedha hupenda kuwa nayo,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe.

Kulingana na takwimu ambazo Nipashe imezikusanya kutoka vyanzo mbalimbali, wastani wa gari jipya aina ya Land Cruiser VX-V8 hununuliwa kwa kiasi cha dola za Marekani 200,000, sawa na Sh. milioni 423. 31 kwa mujibu wa viwango vya ubadilishaji fedha vya jana kwa kikokotozi cha mtandao wa Oanda.

Chanzo kimeiambia Nipashe kuwa yapo pia mashangingi yanayouzwa kwa Sh. milioni 245,000, lakini kwa vile bei za vitu vya serikali huambatana na ‘cha juu’, mara zote ununuaji wa magari hayo huigharimu serikali mabilioni ya fedha kwani bei zake huwa tofauti na zile wanazouziwa watu au taasisi zisizokuwa za serikali.

Jambo hilo la kuongezwa bei katika manunuzi ya serikali, hata Rais Magufuli alilizungumzia wakati wa hotuba yake bungeni Ijumaa ya Novemba 20, 2015.

Kwa sababu hiyo, ikiwa kila gari miongoni mwa mashangingi 2,778 yaliyokadiriwa na uchunguzi wa Nipashe yatanunuliwa kwa mkupuo kwa Sh. milioni 423, maana yake magari hayo huligharimu taifa fedha hizo kiasi cha Sh. trilioni 1. 18.

GHARAMA ZA UENDESHAJI, VIPURI
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe katika baadhi ya gereji jijini Dar es Salaam umebaini kuwa shangingi moja lisilokuwa la serikali hufanyiwa matengenezo ya kawaida (service) kwa gharama ya wastani wa Sh. 400,000 kila baada ya kilomita 5,000 au kila baada ya miezi mitatu. Gharama hizi huhusisha mahitaji kadhaa yakiwamo ya ununuzi wa lita 11 za mafuta ya kulainisha injini yaitwayo ‘engine oil’ kwa Sh.10,000 kwa kila lita moja; mafuta ya kulainisha yaitwayo ‘oil filter Sh. 15,000, ‘pre-filter’ Sh. 10,000, air filter Sh. 30,000, grease kilo moja Sh. 10,000 na vitu vingine kadhaa. Kadhalika, gharama hizi (Sh. 400,000) huhusisha pia malipo ya ufundi.

Hata hivyo, yaelezwa kuwa ‘service’ kwa mashangingi ya serikali huwa ghali zaidi huku gharama zikitajwa kuwa jumla yake huwa ni kati ya Sh. milioni moja milioni 3.5 kulingana na aina ya shangingi. Nipashe imechukulia wastani wa gharama hizi kuwa ni Sh. milioni 2.25 kwa kila gari.

Kwa sababu hiyo, wastani wa gharama za ‘service’ moja kwa mashangingi 2,778 ya serikali ni Sh. bilioni 6.25. Na kama service hizi zitafanyika mara nne kwa mwaka, maana yake gharama za jumla zinazobebwa na serikali kwa mashangingi yote ni takriban Sh. bilioni 25.

Kadhalika, yaelezwa kuwa miongoni mwa sifa za mashangingi ni uimara wa vipuri vyake. Hata hivyo, inapotokea vimeharibika kwa namna yoyote ile, gharama zake huwa kubwa, hasa kwa mashangingi hayo ya serikali.

Kwa mfano, yaelezwa kuwa tairi zikiharibika au kubadilishwa baada ya kutembea umbali wa kilomita 50,000, bei yake huwa ni Sh. milioni 4; taa kubwa zikiharibika huuzwa Sh. milioni 7 (kwa zote mbili); nozzle zipo nane na kila moja huuzwa Sh. milioni 1.5, hivyo kwa zote ni Sh. milioni 12 na brakepads (breki) Sh. 650,000 kwa wateja wa kawaida huku kwa mashangingi ya serikali zikitajwa kufikia hadi Sh. milioni 3.5 pindi zinapobadilishwa.

Kwa sababu hiyo, gharama za kawaida za kubadilisha vipuri hivyo kwa shangingi moja kila inapobidi kufanya hivyo ni Sh. milioni 26.5, sawa na Sh. bilioni 73.65 kwa mashangingi yote 2,778.

Kuhusiana na mafuta, chanzo kimeiambia Nipashe kuwa viongozi wa serikali wanaotumia magari hayo huwa na mgawo maalum kulingana na nafasi zao.

Uchunguzi umebaini kuwa kwa kawaida, wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Wilaya, Mikoa, makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa wizara, makatibu wakuu na naibu waziri na mawaziri hupata mgawo wa lita 10 za mafuta kwa matumizi ya kawaida ya kila siku, sawa na lita 280 kwa mwezi. Hata hivyo, kiwango hiki huongezeka pindi panapokuwa na safari maalum za kikazi nje ya kituo cha kazi.

Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya mmoja wa zamani, watumiaji wengi wa mashangingi hutumia mafuta zaidi ya kiwango kilichowekwa cha kati ya lita 280 hadi 300 kwa mwezi. Badala yake, wapo ambao hutumia hata zaidi ya lita 500 kwa mwezi kutokana na sababu mbalimbali, zikiwamo ziara za nje ya maeneo yao ya kazi.

Kadhalika, imeelezwa kuwa mashangingi yaliyopo maeneo ya mijini kama Dar es Salaam hutumia mafuta mengi pia kwa sababu madereva wengi hubaki na magari hayo huku wakikaa maeneo ya mbali na wanapoishi mabosi wao, mfano ni pale dereva anayeishi Mbagala kulazimika kusafiri umbali mrefu kila uchao kumfuata bosi wake aishiye Tegeta na kumpeleka ofisini Posta kabla ya kumrejesha Tegeta na kisha naye kurejea nyumbani kwake Mbagala.

Aidha, imeelezwa kuwa bosi anapokwenda nje ya mkoa kikazi, mfano kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha, dereva hutangulia na gari tupu huku mkuu akisafiri kwa ndege na hivyo kazi kubwa inayofanyika ni kwenda kumpokea bosi uwanjani na kumpeleka tena uwanjani siku ya kusafiri tena.

Kadhalika, wapo vigogo pia wanaotumia magari hayo kwa matumizi ya nyumbani kama kwenda kununulia bidhaa sokoni na hapo matumizi ya mafuta huongezeka zaidi.

“Mgawo wa mafuta upo, lakini wakuu wengi hawaufuati kwa sababu matumizi ni makubwa… matokeo yake ni mzigo mkubwa wa gharama kwa serikali,” chanzo kingine kimeongeza.

Nipashe imechukulia kuwa kwa wastani, kila shangingi hutumia mafuta kiasi cha lita 400 kwa mwezi. Hivyo, kwa mashangingi 2,778, maana yake jumla ya mafuta ni lita 1,111,200 kwa mwezi, ambazo zikipigiwa hesabu ya bei elekezi ya petroli jijini Dar es Salaam iliyotolewa jana na Ewura ya lita moja kwa Sh. 1,977, maana yake serikali hugharimia kuendesha mashangingi hayo kwa Sh. bilioni 2.20 kwa mwezi, sawa na Sh. bilioni 26.36 kwa mwaka.
Hivyo, wastani wa gharama za jumla kwa mwaka za mafuta, matengenezo ya kawaida na kununua vipuri pindi inapobidi kufanya hivyo kwa mwaka ni Sh. bilioni 125.01.


KUONDOLEWA KWENYE MZUNGUKO
Nipashe imeelezwa kuwa licha ya kununuliwa kwa bei ya juu, mashangingi huanza kuondolewa katika matumizi ya serikali kutegemeana na taratibu za taasisi na wizara husika, hasa kwa kuangalia jinsi yanavyopungua thamani. Baadhi huyaondoa baada ya matumizi yake kufikia asilimia 50, wengine asilimia 60 na zipo taasisi zinazoyatumia kwa muda mrefu zaidi kabla ya kuyapiga mnada.

MASHANGINGI YALIIBUKA LINI?
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa kwa kiasi kikubwa, neno ‘shangingi’ kwa maana ya magari aina ya Toyota Land Cruiser yanayotumiwa na viongozi wa umma lilianza kuibuka baada ya uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 wakati wabunge walipoanza kupewa magari aina hiyo kwa ajili ya kuwarahisishia usafiri, hasa kutokana na hoja kuwa magari hayo huhimili pia misukosuko kwenye barabara duni zisizokuwa na lami, hasa kwenye maeneo ya vijijini.

Waziri Mkuu Mstaafu katika serikali ya awamu ya nne, Mizengo Pinda, aliwahi kusema bungeni mwaka 2012 kuwa serikali imedhamiria kudhibiti matumizi ya magari hayo ili kubana matumizi. Hata hivyo, jambo hilo halikufanikiwa kwa asilimia mia moja kwani vigogo wengi waliendelea kuyatumia.


TRILIONI 1.31/- ZAWEZA KUFANYA NINI?
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa fedha kiasi cha Sh. trilioni 1.31 zinazokadiriwa kuwa gharama za kununulia mashangingi ya serikali 2,778 na kuyahudumia kwa mwaka moja zaweza kufanya mambo mengi ya maendeleo kwa taifa, ikiwamo kuwapa mikopo wanafunzi wote wa elimu ya juu nchini, kujenga maelfu ya zahanati, kuchimba visima katika kila kijiji nchini na pia kumaliza tatizo la madawati nchini.

MIKOPO KWA KINA MAMA
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe umebaini kuwa kina mama wengi wanaojihusisha na shughuli za biashara ndogo ndogo huhitaji mikopo ya kuanzia Sh. 50,000 hadi Sh. 500,000 tu ili kufanikisha biashara zao.
Kwa sababu hiyo, kama fedha za kununulia mashangingi aina ya VX-V8 na kuyahudumia kwa mwaka (Sh. trilioni 1.31) zingetumika kuwakopesha wajasiriamali wanawake, maana yake wanufaika wangekuwa kina mama milioni 2. 62 ambao kila mmoja angepata Sh. 500,000.

MAABARA ZA SEKONDARI
Mkuu wa Shule ya Sekondari Tandika, Hussein Mpungusi, aliwahi kukaririwa Aprili 20, 2015, akisema kuwa wao walikamilisha ujenzi wa maabara mojawapo shuleni kwao kwa Sh. milioni 58.2. Kwa sababu hiyo, kama makadirio ya fedha za kununulia mashangingi na kuyahudumia kwa mwaka (Sh. trilioni 1.31) zingeelekezwa katika ujenzi wa maabara kama ya Sekondari ya Tandika, maana yake zingepatikana maabara takriban 22,509.

MADAWATI
Akizungumza na Nipashe hivi karibuni, Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu, alisema wastani wa bei ya dawati moja linalokaliwa na wanafunzi watatu wa shule ya msingi katika jimbo lake ni Sh. 15,000. Kwa sababu hiyo, fedha za kununua mashangingi 2,778 na kuyahudumia kwa mwaka (Sh. trilioni 1.31) zingetosha kununua madawati milioni 13.1 ya kiwango sawa kama ya Jimbo la Singida Magharibi na kumaliza tatizo hilo nchini kote na mengine yakabaki kwa kukosa wanafunzi wa kuyatumia.

ZAHANATI
Akizungumza na Nipashe Septemba 16 mwaka huu, Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga, January Makamba, alisema kuwa katika jimbo lake, wamekamilisha ujenzi wa zahanati za vijiji kadhaa kwa wastani wa Sh. milioni 80 kwa kila moja. Kwa sababu hiyo, kama fedha za makadirio ya ununuzi wa mashangingi na huduma zake kwa mwaka (Sh. trilioni 1.31) zingetumika kujenga zahanati za kiwango cha Jimbo la Bumbuli, maana yake taifa lingepata zahanati mpya 16,375.

VISIMA VYA MAJI SAFI
Aidha, kwa mujibu wa Kingu (Mbunge wa Singida Magharibi), gharama ya kuchimba kisima cha maji safi kwenye jimbo lake huwa ni wastani wa Sh. milioni 15. Kwa sababu hiyo, wastani wa gharama za serikali kununua mashangingi na kuyahudumia kwa mwaka (Sh. trilioni 1.31) zingetumika kuchimba visima vya kiwango sawa na vile vya Jimbo la Singida Magharibi, maana yake vingepatikana visima 87,333 na hivyo kila kijiji nchini kingepata mgawo wa visima vinne kwani kwa mujibu wa Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), nchi nzima ina vijiji 19,200.

MAGARI YA KUBEBEA WAGONJWA
Mwaka jana, Agosti 28, kulikuwa na taarifa kwenye vyombo vya habari kuwa kampuni ya Biolands International ilikabidhi msaada wa gari la kubebea wagonjwa (ambulance) aina ya Nissan Patrol kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela lenye thamani ya takriban Sh. milioni 76. Kwa sababu hiyo, ikiwa fedha za gharama za mashangingi (Sh. trilioni 1.31) zingetumika kununulia magari ya kiwango kama walilopata msaada Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, maana yake taifa lingepata magari mapya ya kubebea wagonjwa takriban 17,237 na hivyo kumaliza tatizo la ukosefu wa magari hayo katika vituo vya afya na hospitali nyingi nchini.

MIKOPO WANAFUNZI ELIMU YA JUU
Katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa shahada ya uhandisi wa madini katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anayepata mkopo wa asilimia 100 hulipwa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jumla ya Sh. 4,219,500 kwa mwaka. Mchanganuo wa mkopo huo kwa mwaka wote wa masomo ni Sh. 2,099,500 kwa ajili ya chakula na malazi, Sh. 200,000 ya vifaa, Sh. 620,000 kwa ajili ya mafunzo ya vitendo, ada Sh. milioni 1.3.

Kwa sababu hiyo, ikiwa makadirio ya fedha za ununuaji mashangingi na kuyahudumia kwa mwaka (Sh. trilioni 1.31) zingetumika kuwakopesha wanafunzi wa elimu ya juu kama wa mwaka wa kwanza wa shahada ya uhandisi wa madini wanaolipwa asilimia 100, maana yake wanafunzi wangekuwa wanafunzi 310,463. Ikumbukwe kwa mujibu wa Tume ya Vyuo Vikuu, wanafunzi wote nchini hawazidi 300,000.

VIPIMO CT-SCAN
Vyanzo mbalimbali vya Nipashe vinaeleza kuwa kipimo maarufu cha CT-Scan, aina ya Phillips huuzwa kwa wastani wa Sh. milioni 600 hadi bilioni moja. Hivyo, kama fedha za makadirio ya gharama za ununuaji mashangingi na kuyahudumia walau kwa mwaka mmoja (Sh. trilioni 1.31) zingetumika kununua mashine hizo za bei ya Sh. bilioni moja , maana yake zingepatikana CT-Scan 1,310 na kufungwa katika hospitali zote za rufaa nchini na nyingine nyingi zikabaki kwa hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati katika kila kijiji.

BARABARA ZA LAMI
Vyanzo mbalimbali vinaeleza kuwa wastani wa kujenga barabara ya lami ya umbali wa kilomita moja ni Sh. bilioni moja. Kwa sababu hiyo, kama fedha za makadirio ya gharama za kununua mashangingi ya serikali 2,778 na kuyahudumia kwa mwaka mmoja zingeelekezwa katika ujenzi wa barabara, maana yake taifa lingepata barabara mpya ya urefu wa kilomita 1,300, takriban sawa na kutoka Dar es Salaam hadi Bukoba, ambako kwa mujibu wa kikokotozi cha umbali cha mtandao wa Distancefrom, umbali wake wa ardhini ni kilomita 1,376.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa