Home » »
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali ya wabunge katika kikao cha tatu cha mkutano wa pili wa Bunge, mjini Dodoma jana.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hajapiga marufuku mikutano ya hadhara ya wanasiasa walioshindwa kwenye Uchaguzi Mkuu, akisema kauli yake ilinukuliwa vibaya.
Waziri Majaliwa alisema kufanya mikutano ya hadhara ni haki ya kila chama, kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Kauli hiyo aliitoa Desemba 24 akiwa nje ya kituo cha Jeshi la Polisi Ruangwa, ambako alikuwa ziarani.
“Naendelea kuwashukuru kwa mchango wenu mkubwa kiulinzi, lakini pia usimamizi wa zoezi zima la uchaguzi na hatimaye sasa watu wameshapatikana,” alisema Majaliwa siku hiyo ya Desemba 23.
“Na tumesema siasa tumezimaliza. Hatuhitaji tena watu kuja kutuvuruga. Mikutano ya shukrani itafanywa na wale tu waliochaguliwa kwenye maeneo yao. Wengine hao watulie.
“Vyama viache wale tu waliochaguliwa washukuru. Wengine watakuja kuleta maneno ambayo yatatuvuruga. Mimi naamini mko imara.”
Kauli hiyo ilitafsiriwa kuwa ni kupiga marufuku vyama vya upinzani kufanya mikutano ya kuwashukuru wananchi kwa kuwaunga mkono wakati wa Uchaguzi Mkuu, licha ya CCM kushinda urais.
Lakini mtendaji huyo mkuu wa Serikali, alisema wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo bungeni jana, kuwa kauli hiyo ilililenga jimbo la Ruangwa tu, ambako alishinda kiti cha ubunge kwa tiketi ya CCM.
Majaliwa alisema Serikali ya Awamu ya Tano inafuata demokrasia, kanuni na sheria na kwamba waandishi wa habari walimnukuu vibaya.
“Tuliamua kufanya kazi tu bila kuzingatia itikadi za vyama vyetu, kwamba tunaweka siasa pembeni na wanaotakiwa kupita (kushukuru) ni wale walioshinda katika maeneo yao,” alisema Majaliwa baada ya kuulizwa swali hilo na mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe.
Katika swali hilo, Mbowe alisema tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani yametokea mambo matano yanayoashiria kutoheshimu kukua kwa demokrasia katika Taifa, na dhamira ya kuondoa lengo hilo kubwa lililowekwa na Katiba ya nchi.
Alitaja mambo hayo kuwa ni kuzuia mikutano ya vyama vya siasa.
“Leo ni miezi mitatu na siku tatu katazo hilo linaendelea, na wewe (Waziri Mkuu) ulilibariki katika mkutano wako ulioufanya jimboni kwako Ruangwa,” alisema Mbowe.
“Unataka kulithibitishia Bunge, nchi na dunia kwamba wewe kama kiongozi mkuu wa Serikali una kusudio la kuzuia vyama vya siasa kufanya kazi zake za kisiasa ambayo ni haki yao kikatiba. Hata majeshi pia yanatumia nguvu na tumeona kilichotokea katika Uchaguzi Mkuu huko Zanzibar.”
Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema: “Nilifanya ziara jimboni kwangu kwa ajili ya kusalimia wapigakura wangu. Ninapokuwa Ruangwa nakuwa mbunge na sivai koti la Waziri Mkuu. Nilikutana na wapinzani, akinamama, wazee na madiwani wote. Nilichokisema mimi ni sawa na kauli za madiwani, wakiwemo wa upinzani kwamba jimbo hili tufanye kazi na tuondoe tofauti za kisiasa.”
Alisema shughuli zote alizozifanya Desemba 24 alipokuwa Ruangwa zingefuatiliwa kwa kina na wanahabari, zisingenukuliwa kuwa alizuia mikutano hiyo nchi nzima.
“Najua sheria, najua chama cha siasa kina haki yake na pia najua nchi inatambua vyama vinaweza kufanya mkutano. Kama tulichokiamua sisi Ruangwa kinaweza kufuatwa na maeneo mengine ya nchi, inaweza kuwaletea tija pia,” alisema.
Kuhusu majeshi, Majaliwa alisema lengo lake kuu ni kulinda amani na utulivu ndani ya nchi, kuhakikisha watu wanafanya shughuli zao kwa amani na utulivu na kwamba wanaweza kulazimika kutumia nguvu wanapoona utaratibu uliowekwa katika eneo husika unakiukwa.
Kuhusu Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kuzuia kurusha matangazo ya moja kwa moja matangazo ya shughuli za Bunge, Majaliwa alisema hilo limefanyika ili kupunguza gharama za uendeshaji wa shirika hilo.
CHANZO ; MWANANCHI.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa