Home » » KAMATI YA KINA ZITTO YABATIZWA 'GEREZA LA GUANTANAMO BAY'

KAMATI YA KINA ZITTO YABATIZWA 'GEREZA LA GUANTANAMO BAY'

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Zitto Kabwe.
Wakati Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ikigomea uchaguzi wa wenyeviti wa Kamati za Bunge, baadhi ya wabunge wamekuwa wakiwatania wenzao waliopo kwenye Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa kuwalinganisha na watuhumiwa wa ugaidi walioshikiliwa na utawala wa Marekani katika gereza la Guantamo Bay (hivi sasa Gitmo) lililopo nchini Cuba.
 
Gereza hilo ambalo hivi sasa limepewa jina la Gitmo, limekuwa likitumiwa na Marekani kwa kuwahifadhi wapiganaji wanaokamatwa Iraq na Afghanistan bila ya kuwafungulia mashitaka yoyote.
 
Wabunge waliopo katika kamati hiyo ni Hussein Bashe, wa Jimbo la Nzega Mjini, Dk. Charles Tizeba (Buchosa), Margaret Sitta (Urambo Mashariki) na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi.
 
Wengine katika kamati hiyo ni Dk. Faustine Ndugulile (Kigamboni), Kasuku Bilago (Buyungu), Dk. Raphael Chegeni (Busega), Peter Serukamba (Kigoma Kaskazini) na Dk. Elly Macha.
 
Wabunge wengine katika kamati hiyo ni Lucia Mlowe, Risala Kabongo, Dk. Jasmine Bunga, Jacqueline Ngonyani Msongozi na Susan Lyimo, ambao wote ni wa Viti Maalum.
 
Katika kamati hiyo iliyopachikwa jina la ‘Guantanamo Bay’, wapo pia Stephen Masele wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Mussa Azzan Zungu (Ilala), Juma Nkamia (Chemba), Seleman Bungara (Kilwa Kusini), Zitto Kabwe (Kigoma Mjini), Lazaro Nyalandu (Singida Kaskazini), Saed Kubenea (Ubungo) na Josephine Genzabuke wa Viti Maalum.
 
Mmoja wa wabunge ameiambia Nipashe kuwa chanzo kimojawapo kwa wenzao hao (wa kamati ya Huduma za Jamii) kutaniwa kuwa wako katika gereza la Guantamo ni kuwa na wabunge wengi wenye majina makubwa kisiasa na ambao awali walitarajiwa kuongoza baadhi ya kamati nyeti, lakini mwishowe wakapangiwa katika kamati wasiyoitarajia.
 
Kwa muda mrefu, Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC);  Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC); Bajeti; Katiba na Sheria; Nishati na Madini; Miundombinu, Ardhi, Maliasili na Utalii na ile ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama; zilizoeleka kuwa na watu wenye majina makubwa kisiasa; jambo ambalo ni tofauti na sasa kwani baadhi ya walioteuliwa hawana umaarufu mkubwa.
 
Baada ya wajumbe wa Kamati ya Huduma za Jamii kufanya uchaguzi wao na Serukamba kushinda uenyekiti, baadhi ya wabunge walionekana kumtania (Serukamba) kwa kumuita ‘Kiongozi wa Gereza la Guantanamo’ huku wengine wakimuita ‘Kiongozi wa Jamii’. Katika Bunge la 10, Serukamba alikuwa ni mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu.  
 
Pia, baadhi ya wabunge wa kamati hiyo, walionekana wakitaniana wenyewe kwamba sasa kazi yao itakuwa kukagua madarasa vijijini na pia ubora wa zahanati.
 
Mbali na kamati hiyo, wabunge pia walionekana kuwatania wajumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo ambayo imesheheni wanasheria maarufu.
 
Wajumbe hao walikuwa wakitaniwa kwamba baadhi yao, licha ya kuwa na weledi mkubwa kwenye sheria, wamepangwa katika kamati ambayo kazi yake kubwa ni kuangalia sheria zinazohusiana na vijiji na serikali za mitaa.
 
Baadhi ya wanasheria maarufu waliomo kwenye kamati hiyo, ni pamoja na Mbunge wa Bariadi Andrew Chenge, Halima Mdee (Kawe), William  Ngeleja (Sengerema), Tundu Lissu (Singida Mashariki) na Ridhiwan Kikwete (Chalinze).
 
Wabunge wengine maarufu kwenye kamati hiyo ni Prof. Anna Tibaijuka (Muleba Kusini), ambaye kwenye Bunge lililopita alikuwa Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi kabla ya uteuzi wake kutenguliwa kufuatia kuhusishwa kwake na kashfa ya Escrow pamoja na Sadifa Juma Khamis (Donge) ambaye pia ni Menyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
 
NAIBU KATIBU WA BUNGE
Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa juma, Naibu Katibu Mkuu wa Bunge, Uendeshaji, John Joel, alisema wameamua kupanga watu werevu kwenye sheria katika kamati hiyo kwa sababu serikali inaanzia kwenye mitaa na halmashauri.
 
Alisema katika eneo hilo kuna sheria nyingi zinazotungwa ambazo haziendani na zile zinazotungwa na Bunge, hivyo wameamua kuchagua watu makini ili wazisimamie.
 
SABABU KUITWA ‘GUANTANAMO BAY’
Inaelezwa zaidi kuwa mbali na kutarajiwa kuwamo kwenye kamati nyeti kama ya PAC, wengi waliomo kwenye kamati ya Huduma za Jamii walikuwa wakitarajiwa kushika nafasi za juu zikiwamo hata za uwaziri na pia uspika, akiwamo Zungu aliyekuwa mwenyekiti wa Bunge katika Bunge la 10.
 
Kadhalika, inaelezwa kuwa ndani ya kamati hiyo, wamo watu ambao wamekuwa wasemaji wa masuala mengi ndani ya CCM, akiwamo Bashe.
 
Jitihada za kumpata mwenyekiti wa kamati hiyo, Serukamba, kuzungumzia suala hilo jana zilishindikana baada ya simu yake ya mkononi kuita muda mwingi bila kupokelewa.
 
Zitto alipoulizwa kama anajua kuwa kamati aliyopo sasa inataniwa kwa jina la Guantanamo Bay, alisema ni kweli, lakini hajui ni kwanini.
 
“Kwakweli sijui kwa nini wanatuita hivyo, nadhani ni sababu ya kuwa kamati imesheheni wabunge wenye majina makubwa.
 
Maana toka juzi tukikutana na wabunge wengine wanasema ‘ah wazee wa Guantanamo’… tunacheka tu, sijui sababu. Ila wacha tufanye kazi kwa umakini kwenye sekta ya elimu, afya na michezo,” alisema Zitto ambaye katika Bunge la 10 alikuwa ndiye mwenyekiti wa PAC huku Serukamba akiongoza Kamati ya Miundombinu.
 
GUANTANAMO BAY
Mwaka 1903, Tomas Estrada Palma, aliyekuwa Rais wa Cuba, alilikodisha eneo hilo kwa Wamarekani.
 
Baada ya vitendo vya ugaidi kushamiri, mwanzoni mwa mwaka 2002, washukiwa wa kwanza wa ugaidi walipelekwa kwenye gereza hilo kwa amri ya aliyekuwa Rais wa Marekani, George. W. Bush na Rais wa sasa, Barack Obama, alipoingia madarakani mwaka 2009, aliahidi kufunga gereza hilo ingawa hadi sasa hajatimiza ahadi yake hiyo.
 
Baadhi ya wadadisi wanaamini kuwa Marekani ilifungua gereza hilo nje ya ardhi ya Marekani ili wanajeshi wake wapate fursa ya kutumia mbinu zilizopigwa marufuku katika ardhi yao za kuwahoji wafungwa.
 
Kwa muda mrefu, gereza hilo pia limekumbwa na tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu,  wafungwa wakidaiwa kuteswa, kupigwa na hata kulazimishwa kukiri baadhi ya makosa wasiyowahi kuyatenda.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa