Home » » MADIWANI WAGOMEA UAMUZI WA WENZAO WALIOPITA.

MADIWANI WAGOMEA UAMUZI WA WENZAO WALIOPITA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
BARAZA jipya la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro limekataa mpango uliopitishwa katika vikao vya Baraza la Madiwani lililomaliza muda wake ambalo liliridhia ununuzi wa ekari 400 za ardhi kutoka kwa watu wanne tofauti kwa gharama ya Sh milioni 800 ili kujenga machinjio ya kisasa.
Kwa kauli moja wameeleza kuwa kiwango hicho ni kikubwa na kushauri kutafutwa kwa eneo lingine ambalo litakuwa kwa gharama nafuu kwa ajili ya ujenzi wa machinjio hayo ya kisasa ili kiwango kingine kitumike katika shughuli za maendeleo ya wananchi.
Hoja hiyo ya kukataa kununuliwa ekari hizo kwa gharama hiyo ilitokea baada ya Katibu wa Baraza la Madiwani ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hivyo, Theresia Mahongo , kuwasilisha ajenda inayohusu ununuzi wa eneo la ardhi kwa ajili ya ujenzi wa machinjio mapya kutokana na lile la zamani kuwa chakavu, kuzungukwa na makazi ya watu, hivyo kusababisha kero.
Baraza hilo la madiwani lilikutana juzi ikiwa ni kikao chake cha kawaida ambacho kilipitia ajenda mbalimbali zilizohusu maendeleo ya halmashauri hiyo ikiwemo ya ujenzi wa machinjio mapya, mazingira, ujenzi holela na elimu.
Akichangia hoja ya mpango wa ujenzi wa machinjio mapya ya kisasa, Diwani wa Lukobe, Castor Ndulu, alitaka kujua eneo lililotengwa lina ukubwa gani, mmiliki wake pamoja na gharama za ununuzi wa ardhi hiyo.
Hoja hiyo ilipatiwa majibu kutoka kwa Ofisa Mipango Miji wa Manispaa, Steven Balonzi , kuwa eneo hilo ni mashamba ya watu wanne na yana ukubwa wa ekari 400 na gharama yake ni Sh milioni 800.
Kutokana na majibu hayo, Ndulu pamoja na wenzake walikataa kwa kupinga mpango huo wa kununua ekari hizo kwa gharama ya Sh milioni 800 na kutaka mchakato huo ufanyike upya kwa kuangalia maeneo mengine ya ardhi yatakayonunuliwa kwa bei ndogo.
Mbali na hilo, pia Ndulu alitaka kujua utekelezaji wa agizo la aliyekuwa Katibu Mkuu Tamisemi, Jumanne Sagini, alilolitoa Desemba Mosi, mwaka jana alipofanya ziara Manispaa ya Morogoro ambapo alibaini mambo kadhaa ikiwamo ya kujengwa kwa ukuta wa Hoteli ya Flomi eneo la hifadhi ya bomba la mafuta la Tazama.
Katika maagizo yake, Sajini alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa kuchukua hatua kwa watumishi waliohusika utoaji wa vibali vya ujenzi katika maeneo ya hifadhi ya bomba hilo.
CHANZO ; HABARI LEO.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa