Home » » Mambo sita kutikisa Bunge

Mambo sita kutikisa Bunge

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399

By Fidelis Butahe, Mwananchi
Dar es Salaam. Mambo sita makubwa yanatarajiwa kuibuka kwenye Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano likaloanza vikao vyake wiki ijayo, huku CCM ikionekana kuanza kujizatiti kwa kufanya kikao cha wabunge wote jana.

Mkutano huo wa pili wa Bunge la Kumi na Moja utakuwa wa wiki mbili, lakini uliojaa matukio makubwa kama ya hali ya kisiasa Zanzibar, hotuba ya Rais John Magufuli, utekelezwaji wa maazimio kuhusu sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, sera ya elimu bure hadi sekondari, mchakato wa kupata Katiba Mpya na utekelezaji wa operesheni bomoabomoa.

Kufutwa kwa uchaguzi Zanzibar ndilo linaloonekana kuwa suala kubwa baada ya wabunge wanaounda Ukawa kupiga kelele wakitaja jina la mgombea urais wa visiwa hivyo kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad wakati mpinzani wake, Ali Mohamed Shein akiingia kwenye chombo hicho cha kutunga sheria kusikiliza hotuba ya Rais Magufuli.

Zanzibar ni suala nyeti

“Hili ni suala nyeti na tutalikomalia kweli kweli,” alisema mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alipoulizwa na gazeti la Mwananchi kuhusu hoja ambazo anaona zitatikisa Bunge.

“Nyinyi subirini mambo kwa vitendo sitaki kuongea sana. Nadhani mengine mnayajua. Lipo sakata la escrow. Mpaka sasa sijaandaa hotuba yangu, lakini itoshe kusema kuwa mambo ni mengi,” alisema Lissu, ambaye ni mwanasheria mkuu wa Chadema.

Zanzibar iliingia kwenye mgogoro huo baada ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi wa rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani kwa madai kuwa sheria na kanuni zilikiukwa na kuahidi kuitisha uchaguzi mwingine ndani ya siku 90.

Hata hivyo, Maalim Seif, CUF na vyama vingine vya upinzani wanapinga kitendo hicho wakisema mshindi wa uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25 atangazwe na wanasema waziwazi kuwa mgombea huyo wa CUF ndiye aliyeshinda.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Hamad Salum pia aliungana na Lissu katika suala la Zanzibar akisema ni lazima wabunge waibue mgogoro huo.

Alisema suala la Zanzibar linapaswa kujadiliwa peke yake kwa maelezo kuwa hatma ya maisha ya Wazanzibari yapo shakani.

“Hakuna anayejua kesho hali itakuwaje Zanzibar. Jambo hili linapaswa kupatiwa ufumbuzi wa haraka sana,” alisema.

Kauli kama hiyo aliitoa mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya.

“Wabunge lazima wahoji mustakabali wa Zanzibar. Mpaka sasa mazungumzo kati ya CCM na CUF ni kama yamekufa na tukiacha suala hili hivihivi, hali itakuwa mbaya Zanzibar,” alisema Sakaya ambaye anaingia kwenye chombo hicho kwa mara ya kwanza.

Hotuba ya Rais

Mkutano huo wa pili wa Bunge, utajikita zaidi kujadili hotuba ya Rais Magufuli wakati akizindua chombo hicho, ambayo ilitoa mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano, ikitaja vipaumbele na aina ya utekelezaji wake.

Tayari Rais Magufuli ameanza kutekeleza ahadi zake kwa kubana matumizi ya Serikali, kubana mianya ya rushwa, kutoa elimu bure kuanzia chekechea hadi sekondari, na kupambana na tabia ya ufisadi na uzembe serikalini, lakini wadau wanaona bado kuna mambo yanayohitaji kusukumwa.

Akizungumzia kasi ya ukusanyaji kodi, Zitto pia alisema wabunge watahoji iwapo makusanyo ya Januari yatashuka, lakini pia suala la watendaji wa Serikali kuondolewa kwa sababu ya rushwa.

“Mwezi Desemba mwaka jana TRA ilikusanya kodi kubwa (Sh1.4 trilioni), lakini ikumbukwe kuwa kila unapofika mwezi huo makusanyo huwa juu. Hivyo wabunge wanaweza kutumia makusanyo ya mwezi Januari kama yatakuwa chini ni lazima wataikosoa Serikali,” alisema.

Naye Sakaya alizungumzia utatuzi wa migogoro ya ardhi.

“Pia tutataka kujua utekezaji wa Serikali kuhusu migogoro ya ardhi kati ya wakulima, wafugaji na hifadhi. Kamati teule ya Bunge iliyoundwa mwaka 2014 ilitoa taarifa na mapendekezo yake na kuipa Serikali miezi sita kukamilisha utekelezaji. Tutataka kujua Serikali imetekeleza vipi,” alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo alisema, “Wabunge wakemee haya yanayoendelea sasa kwa mawaziri kuwasimamisha watu kazi na kuwafukuza. Nasema hivi kwa sababu hii si aina nzuri ya utawala bora na hatusikii utetezi wa upande wa pili (wanaofukuzwa na kusimamishwa),” alisema.

“Tunataka mabadiliko, lakini wabunge wanapaswa kusisitiza ukuu wa taasisi na mfumo na kukemea ukuu wa viongozi wa Serikali. Sasa hivi hadi mfanyakazi kuchelewa kazini waziri ndiyo anasimamia? Haiwezekani mtu yuko Bukoba aombe kibali cha kusafiri Ikulu.”

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Hamad Salim alisema jambo la msingi katika utekelezaji wa masuala yaliyomo kwenye hotuba ya Rais ni kutokuwapo kwa mfumo.

“Wanapaswa kuweka muundo wa utekelezaji, kuonyesha tumetoka wapi na tunakwenda wapi na hili lifanyike bila ushabiki wa vyama,” alisema.

Elimu bure

Wakati Serikali ikianza kutekeleza sera yake ya elimu bure, mmbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe alisema anaona mapungufu kwa kuwa kuna maswali mengi kuliko majibu.

“Leo (jana) ninatembelea shule mbalimbali jimboni kwangu. Kuna mambo nimebaini, likiwemo hili la ruzuku ya utekelezaji wa elimu bure kutoka serikali kutokidhi mahitaji,” alisema Zitto.

“Yaani wanafunzi ni wengi kuliko ruzuku ya Serikali jambo ambalo limekuwa na changamoto kubwa.”

Serikali imetenga Sh100 bilioni kila mwezi kwa ajili ya kuziwezesha shule kutekeleza sera hiyo ya elimu bure, lakini kumeibuka changamoto za uendeshaji wa shule zinazowafanya walimu walalamikie ukata, huku wale waliokaidi wakivuliwa nyadhifa zao.

Sakata la escrow

Zitto pia alisema vyama vinavyounda Ukawa vya NCCR-Mageuzi, Chadema, NLD na CUF ni lazima vitaibana Serikali kuhusu utekelezaji wa maazimio saba ya Bunge kuhusu escrow.

“Na hili linatokana na Rais kumteua (Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter) Muhongo na (aliyekuwa katibu mkuu wa wizara hiyo, Eliakim) Maswi. Hawa na wenzao walitajwa katika ripoti na walitakiwa kuwajibika, sasa wamerudishwa,” alisema.

Bunge lilimuona Profesa Muhongo na Maswi kuwa hawakutekeleza wajibu wao ipasavyo katika kushughulikia sakata la escrow na kusababisha Serikali kupoteza mapato yake. Hata hivyo, Baraza la Maadili la Viongozi wa Umma liliwasafisha kuwa hawakufanya vitendo vya kukiuka maadili.

Katika hilo, Sakaya alisema utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu escrow lazima litaibuliwa kwenye mkutano huo, ambao pia utapokewa miswaada kadhaa kutoka serikalini.

Bomoabomoa
Suala jingine linalotazamiwa kutikisa mkutano huo ni utekelezaji wa operesheni ya kubomoa nyumba zilizojengwa kinyume na sheria na taratibu baada ya kazi hiyo kuhusisha vitendo vinavyotafsiriwa kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Wengi walilalamikia Serikali kuwa haikutoa muda wa kutosha kwa wananchi kujiandaa na hivyo kusababisha baadhi ya waliobomolewa kuendelea na maisha juu ya vifusi, na wengine kupoteza maisha.

Operesheni hiyo, ambayo inapingwa mahakamani, inatarajiwa kuhusiaha zaidi ya nyumba 15,000.

Katiba mpya

Wakati vyama vya upinzani vikiwa havijaridhishwa na utangazaji wa matokeo ya kura za wagombea urais na kutopatikana kwa mshindi wa Zanzibar, wapinzani wanaweza kuchukulia suala la Katiba mpya kuwa hoja kuu kwenye Bunge la Kumi na Moja.

Ukawa walipinga matokeo ya kura za rais wakisema NEC ilikuwa ikitangaza tofauti na yalivyokuwa vituoni, lakini chombo hicho kikaendelea kutangaza hadi mshindi alipopatikana.

Wakati mchakato wa Katiba mpya ukielekea kukwama, vyama hivyo vilitaka Serikali ifanye mabadiliko kwa kuingiza suala la tume huru ya uchaguzi, lakini haikufanyika.

CCM wajifungia Dom

Wakati huohuo, kikao cha wabunge wa CCM jana kilianza kwenye ukumbi wa White House chini ya katibu mkuu wa chama hicho, Abdulahman Kinana huku kukiwa na usiri mkubwa ingawa taarifa zilieleza kuwa walijadili mambo makuu matatu.

Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zilidokeza ajenda kuu tatu kuwa zilikuwa ndizo zikijadiliwa na wabunge hao na kwamba wataendelea nazo leo ili kuwekana sawa.

Mmoja wa wabunge hao alitaja baadhi ya ajenda kuwa ni Wajibu wa wabunge wa CCM kwa Serikali ambayo ndiyo inasemekana kupewa nafasi kubwa kuliko nyingine.

Pia tathimini ya uchaguzi ndani ya chama hicho pamoja na mchakato mzima ulivyokuwa katika kura za maoni.

Nyongeza na Habel Chidawali

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa