Home » » WABUNGE; MAGUFULLI USIJALI WANAOKUBEZA.

WABUNGE; MAGUFULLI USIJALI WANAOKUBEZA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
RAIS John Magufuli pamoja na mawaziri wake, wamehimizwa kutovunjika moyo kwa kauli za kubeza kazi wanazofanya, badala yake wahakikishe wanaendelea na kasi yao kudhihirisha wanachofanya si moto wa kifuu.
Hayo yalielezwa jana bungeni wakati wabunge wakichangia Hotuba ya Rais Magufuli aliyoitoa Novemba mwaka jana wakati wa ufunguzi wa Bunge la 11. Katika mjadala huo ambao wabunge wote waliendelea kumpongeza Rais Magufuli kwa kazi anayofanya, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) alishauri Serikali kuwasilisha bungeni sheria zote zinazokinzana na kasi ya Rais, zifanyiwe mabadiliko ya haraka.
Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda (CCM) alimpongeza Rais Magufuli kwa hatua ya kubana matumizi na kuchukua hatua kwa watumishi wasiowajibika. Alisema kazi hiyo inatambuliwa pia na wananchi, kiasi kwamba ikishafika kipindi cha taarifa ya habari, wamekuwa wakikimbilia kuangalia televisheni kwa ajili ya kuona ni nini rais na mawaziri wake wanasema.
Mbunge wa Mufindi Kusini, Mendard Kigola (CCM) alisema hotuba ya Rais Magufuli, imekuwa mwongozo pia kwa wabunge kwa yale wanayopaswa kuyasimamia majimboni mwao kutokana na kugusa mambo yote ambayo wananchi wanahitaji.
Alisema kilichomfurahisha ni namna ambavyo Rais amemudu kutekeleza ahadi, alizotoa wakati wa kampeni ndani ya kipindi kifupi cha miezi mitatu. Alitoa mfano wa mpango wa elimu bure na kusema hakuna mtu ambaye hasikii wala haoni kazi inayofanyika.
“Kufanya utekelezaji ndani ya miezi mitatu…kuna watu wengine wanasema anatekeleza kidogo kidogo…tusimkatishe Rais tamaa, ameanza kufanya kazi na anaonekana kwa Watanzania,” alisema Kigola.
Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe alimpongeza Rais kwa hotuba aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa Bunge akisema ndiye Rais ambaye Watanzania walikuwa wakimhitaji kwa ajili ya mageuzi nchini huku akisisitiza kwamba taifa liko kwenye dharura likihitaji uongozi wa aina hii.
Bashe alisema wapo watu ambao wamekuwa wakisema Rais amekuwa akivunja na kukanyaga sheria katika mambo ambayo amekuwa akifanya sasa. Mbunge huyo alisema lipo tatizo la uwapo wa sheria ambazo baadhi ya watu wamekuwa wakizitumia kuiibia nchi.
Alisema sheria za namna hiyo zimekuwa zikiwapa fursa watendaji wengi kuiibia nchi yetu. Alishauri kwamba jambo linalopaswa kufanywa sasa ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Waziri mwenye dhamana ya sheria kukaa na kuleta bungeni sheria zote alizoziita za hovyo wazifute.
Bashe alisema utashi wa kisiasa wa Rais Magufuli umeonekana hivyo wabunge wanapaswa kumsaidia kuhakikisha mambo anayotaka kuyatekeleza ikiwemo ujenzi wa viwanda, yanafanikiwa. Alihimiza ufanyike uamuzi sahihi wa uwekezaji katika viwanda kwa kuhakikisha vinavyoanzishwa vinalenga kuinua wananchi walio wengi hususan wakulima.
Kuhusu ujenzi wa reli ya kisasa, alisema taarifa hizo zimekuwepo kwa muda mrefu bila utekelezaji jambo aliloomba wabunge katika bajeti ijayo wahakikishe fedha zinatengwa, vinginevyo wasikubali kuipitisha.
Wakati wabunge wakitoa kauli hizo dhidi ya wanaobeza utendaji wa Rais, juzi katika mkutano na waandishi wa habari, Kambi ya Upinzani kupitia kwa Kiongozi wake, Freeman Mbowe, walishutumu hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa dhidi ya watumishi wazembe na wabadhirifu.
Mbowe alisema watendaji na watumishi serikalini wamekuwa wakifukuzwa kazi kinyume cha taratibu, bila uchunguzi wala ushahidi. “Mawaziri wanafukuza hovyo watu, sisi tunang’ang’ana kwamba wanatumbua majipu,” alisema Mbowe.
CHANZO ; HABARI LEO.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa