Home » » AG AKEMEA WABUNGE KUSHABIKIA VURUGU.

AG AKEMEA WABUNGE KUSHABIKIA VURUGU.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, George Masaju amewataka wabunge kusimamia utekelezaji wa sheria wanazotunga na si kuhamasisha uvunjaji wa sheria za nchi. Alitoa kauli hiyo jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF).
Mbunge huyo alihoji kwa nini serikali haiwachukulii hatua watu wanaofanya uhalifu Zanzibar na kama wameshindwa, wananchi wawaadhibu wahalifu hao kwa kuwapiga mawe? Pia Mbunge huyo alitaka Waziri wa Mambo ya Ndani atamke kama wameshindwa kudhibiti uhalifu huo, wananchi washughulikie wahalifu hao kwa kuwapiga mawe na magari yao.
Akijibu swali hilo mwanasheria mkuu wa serikali, alisema hoja ya Mbunge huyo sio sahihi na kusisitiza, “Waziri hawezi kutamka watu wavunje sheria, wabunge wanatunga sheria wanatakiwa kusimamia utekelezaji wake”.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angelah Kairuki alisema kuhusiana na hoja kuwa vyombo vya dola vinakiuka haki za binadamu, endapo mbunge huyo ana malalamiko awasilishe kwenye tume ya haki za binadamu ili yapate kushughulikiwa.
Mbunge wa Rombo, Joseph Selesini (Chadema) katika swali la nyongeza alihoji kwa kuwa matukio ya wananchi kuchukua sheria mkononi yanasababishwa na mambo mawili, ikiwemo polisi kwenda kwenye tukio wakiwa wamechelewa na wahalifu wanapokamatwa baada ya muda wanaachiwa.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni alisema Jeshi la polisi linajitahidi kufanya kazi, idadi ya polisi haitoshelezi kutokana na polisi mmoja kuhudumia watu 300 hadi 350.
“Wakati mwingine inatokea baadhi ya polisi wana mapungufu na wamekuwa wakichukuliwa hatua za kisheria na wale wanaotenda makosa ya jinai sheria imekuwa ikifuata mkondo wake,” alisema.
Katika swali la msingi,Mbunge huyo wa Konde alihoji juu ya matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi yamezidi kuongezeka na kusababisha madhara na vifo kwa watu wasio na hatia.
Akijibu swali hilo, Masauni alisema vitendo vya mtu au watu kujichukulia sheria mkononi ni uhalifu ambao umeanza kushamiri katika jamii ikiwemo visiwa vya Zanzibar. Alisema katika kipindi cha mwaka 2013/2014 jumla ya matukio 2,041 yaliripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi nchini.
Mwaka 2013 kulikuwa na matukio 1,112 ambapo Zanzibar yaliripotiwa 14 na mwaka 2014 yalipungua na kufikia matukio 929, kati ya hayo watuhumiwa walichukuliwa hatua stahiki ikiwemo kufikishwa mahakamani.
CHANZO : HABARI LEO.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa