Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angela Kairuki.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angela Kairuki, amesema atawachukulia
hatua viongozi waliotumia vibaya fedha za Mpango wa Kunusura Kaya
Masikini unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Awamu ya Pili
(Tasaf III).
Alisema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Bunda
(Chadema), Ester Bulaya, aliyehoji fedha za Tasaf III zimekuwa
zikitumiwa vibaya na kwamba kuna mgombea urais uchaguzi mkuu uliopita
alitumia fedha za hizo kufanyia kampeni.
Kairuki alisema amepata malalamiko hayo na kwamba anayafanyia kazi ili kuwabaini waliohusika na suala hilo.
Alisema atawachukulia hatua kwani fedha za Tasaf zinatakiwa kutumika kwa malengo yaliyowekwa na siyo vinginevyo.
Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya
(CUF), Kairuki alisema asilimia 30 ya vijiji na mitaa katika
halmashauri zote imepangwa kufikiwa na mpango huo mwaka huu.
Alisema vijiji 54 sawa na asilimia 70 ya vijiji vyote katika wilaya
ya Kaliua, mkoa wa Tabora viko katika mpango wa tatu wa kunusuru kaya
masikini (TASAF III).
“Serikali ilitoa maagizo ili kufikia vijiji, mitaa na shehia zote
zilizobaki. Vilivyoanza ndiyo nvilikuwa na hali mbaya zaidi,” alisema.
Kairuki mpango huo hutambulishwa kijijini na wataalam kutoka
halmashauri husika kwa kusimamiwa na uongozi wa kijiji, kisha kuweka
vigezo vya kaya masikini.
“Wakusanya taarifa huchaguliwa kutoka miongoni mwa vijana wanaoishi
kijijini hapo ambao hupita nyumba kwa nyumba kuorodhesha kaya
zinazokidhi vigezo vilivyoainishwa na mkutano mkuu wa kijiji,” alisema.
Alisema orodha ya kaya zilizoorodheshwa na timu ya wakusanya
taarifa husomwa mbele ya mkutano wa kijiji na kisha majina kujadiliwa.
“Kutokana na orodha hiyo, kaya hizo hujaziwa dodoso maalum
linaloandaliwa na TASAF makao makuu kwa lengo la kupata taarifa zaidi za
kaya. Dodoso hilo huchambuliwa kupitia mfumo maalum wa kompyuta ili
kupata kaya masikini sana zinazokidhi vigezo,” alisema Kairuki.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment