Home » » MAGUFULI ARIDHIA MKOA MPYA, WILAYA TANO.

MAGUFULI ARIDHIA MKOA MPYA, WILAYA TANO.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
RAIS John Magufuli ameridhia kuanzishwa kwa mkoa mpya wa Songwe na kuanzishwa kwa wilaya za Kibiti, Ubungo, Kigamboni, Malinyi na Tanganyika. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alitoa taarifa hiyo jana mjini hapa, kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Mkoa wa Songwe unaundwa na wilaya za Mbozi, Momba na Ileje. Kwa upande wilaya mpya zilizoanzishwa mikoa yake kwenye mabano ni Kibiti (Pwani), Ubungo na Kigamboni (Dar es Salaam), Malinyi (Morogoro) na Tanganyika (Katavi).
Mchakato wa kuanzishwa kwa maeneo mapya ya utawala ulihitimishwa kwa Tangazo la Serikali la Januari 29, mwaka huu. Waziri alisema Mkoa wa Songwe uliomegwa kutoka Mbeya pamoja na wilaya hizo, zimeanzishwa kwa mujibu wa sheria.
Aliagiza wakuu wa mikoa ambao katika mikoa yao imeanzishwa mkoa pamoja na wilaya mpya, wafanye maandalizi muhimu kuwezesha kuanza rasmi. Miongoni mwa mambo ambayo waziri amesisitiza yatiliwe mkazo ni upatikanaji wa majengo ya ofisi na huduma muhimu kuweka mazingira ya shughuli za kiutawala, kuanza kufanyika katika maeneo hayo ya kiutawala.
Waziri alifafanua Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inampa mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uwezo wa kugawa nchi kwa kadri ambavyo ataona inafaa.
Alisema kwa kutumia madaraka hayo kikatiba, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, Oktoba 18, mwaka jana alitangaza nia ya kugawa Mkoa wa Mbeya na kuanzisha Songwe kwa Tangazo la Serikali Namba GN 461.
Alisema tarehe hiyo, rais alitoa tangazo namba GN 462 iliyokusudia kuanzisha wilaya hizo. Tangazo hilo liliweka muda wa wananchi kutoa maoni yao, ushauri na hata pingamizi. Alisema siku 30 zilizowekwa, hakukuwa na pingamizi zozote.
Kuongezwa kwa Mkoa wa Songwe kunafanya idadi ya mikoa ya Tanzania Bara kufikia 26. Mikoa mingine iliyoongezwa katika Serikali ya Awamu ya Nne ni Geita, Katavi, Njombe na Simiyu. Awali, mikoa ya Tanzania Bara ilikuwa 21 ambayo ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Lindi, Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Singida, Tabora na Tanga.
Zanzibar ipo mikoa mitano ambayo ni Kaskazini Pemba, Kusini Pemba, Mkoa wa Mjini, Mkoa wa Kusini Unguja na Mkoa wa Kaskazini Unguja. Wakati huo huo, Waziri Simbachawene amesema wizara yake imeshatoa maelekezo kuwa uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam ufanyike Februari 8, mwaka huu.
 CHANZO : HABARI LEO.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa