Home » » MAOFISA MAENDELEO YA JAMII WAONYWA UKEKETAJI

MAOFISA MAENDELEO YA JAMII WAONYWA UKEKETAJI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Serikali imesema haitasita kuwachukulia hatua maofisa maendeleo ya jamii ambao watashindwa kuwajibika kutokomeza vitendo vya ukeketaji katika maeneo yao.
 
Aidha, maofisa hao wametakiwa hadi kufikia Machi 31, mwaka huu wawe wametoa taarifa wizarani kuhusu wazazi ambao hawajawapeleka watoto wao shule ili wachukuliwe hatua za kisheria.
 
Agizo hilo lilitolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alipokuwa akizungumza katika siku ya kupinga ukeketaji dhidi ya watoto wa kike na wanawake, iliyofanyika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki.
 
“Ofisa maendeleo ya jamii yeyote ambaye vitendo hivi vitatokea katika eneo lake tutamchukulia hatua, lazima waongeze jitihada hata kama kuna changamoto ya rasilimali fedha na vitendea kazi,” alisema.
 
 Mwalimu alisema maofisa hao wanatakiwa  kuwatumia watendaji wa kata na vijiji kupata taarifa na kuhakikisha hatua sahihi zinachukuliwa ili kukomesha ukeketaji.
 
Alisema katika malengo yake, Tanzania imejiwekea itakapofika mwaka  2030 kusiwe na mtoto yeyote ambaye atakeketwa.
 
“Serikali haitakubali kutumia kigezo cha mila na desturi kuendeleza vitendo vya ukeketaji dhidi ya watoto wa kike na wanawake kwani vina madhara makubwa kiafya, kielimu, kisaikolojia na kimaendeleo,” alisema waziri huyo.
 
Alisema ukeketaji ni janga la kitaifa, hivyo ni lazima mapambano yake yawapo ili kutokomeza vitendo hivyo, kwani wa utafiti wa kidemografia na afya Tanzania uliofanyika mwaka 2010 katika mikoa mitano umeonyesha ukeketaji upo kiwango cha juu.
 
Aliitaja mikoa inayoongoza kwa vitendo hivyo kuwa ni Manyara asilimia 71, Dodoma asilimia 64, Arusha asilimia 59, Singida asilimia 51 na Mara asilimia 40,  na kote vimetokana na imani na mila potofu.
 
 Alisema mila hizo zimeanza kujitokeza katika mikoa mingine kama Dar es Salaam, Morogoro na Pwani, kutokana na watu wa makabila mbalimbali kuhamia mikoa hiyo.
 
Aliwataka maafisa hao kushirikiana na jeshi la polisi kuhakikisha wanamkamata mzazi au mlezi au  mtu yeyote anayefanya vitendo vya ukeketaji na kesi hizo zitasimamiwa ipasavyo.
 
 Naye Kaimu Mkurugenzi wa Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Cynthia Mushi, alisema bado kuna changamoto katika kukabiliana na vitendo hivyo kutokana na kukosekana miundo na mifumo ya ulinzi.
 
Alisema hali hiyo inaweza kutoa ulinzi wa kutosha kwa wasichana walio katika hatari na walioathirika na ukeketaji na mila kandamizi.
CHANZO:GAZETI LA  NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa