Home » » MAWAZIRI WATATU WATAJWA KASHFA ZA UFISADI MKUBWA

MAWAZIRI WATATU WATAJWA KASHFA ZA UFISADI MKUBWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Rais Dk. John magufuli.
 
Mawarizi wa tatu wa Rais Dk. John magufuli, juzi walipata wakati mgumu Bungeni baada ya kuhusishwa na kashfa zilizotokea katika wiozara walizokuwa na wanazoendelea kuziongoza. 
 
Mawaziri hao ni William Lukuvu wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Profesa Sospeter Muhongo wa Nishati na Madini na Dk. Harrison Mwakyembe wa Katiba na Sheria.
 
Lukuvi alihusishwa na tuhuma za uporaji wa ardhi kwa kutumia nafasi yake wakati Profesa Muhongo akilipuliwa kuhusiana na sakata la Escrow ambalo lilimfanya ajiuzulu nafasi aliyo nayo sasa wakati wa serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
 
Dk. Mwakyembe kwa upande wake, alihusishwa na kashfa ya ununuzi wa mabehewa mabovu kutoka India uliofanywa na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL). Wakati wa ununuzi wa mabehewa hayo, Dk. Mwakyembe alikuwa Waziri wa Uchukuzi ambayo ndiyo yenye dhamana ya kusimamia reli.
 
Akichangia hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango, juu ya mwongozo wa kuandaa mpango wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2016/17, Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonist (Chadema), alisema Lukuvi anahusika katika uporaji wa viwanja vya wananchi.
 
Alisema katika sekta ya ardhi, kuna migogoro ya ardhi ambayo inarudisha maendeleo ya wananchi nyuma.
“Dar es Salaam sasa mnavunja nyumba za watu wa mabondeni, kutokana na zoezi hilo watu zaidi ya 99, 000 watakuwa hawana makazi.
 
“Mnavunja nyumba zao halafu viwanja hamuwapi, Lukuvi amehusika na uporaji wa viwanja wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Katika hali kama hii wananchi wataishi maisha gani?” alihoji.
 
Alisema baadhi ya mawaziri badala ya kufanya kazi, wanashindana kuoenakana kwenye vyombo vya habari.
 
Alisema kasi ya Serikali kuwaletea wananchi maendeleo ni ndogo, kwa kuwa katika kipindi cha miaka 15 Serikali imepunguza umasikini kwa asilimia 14 tu.  
 
Kwa upande wake,  Kubenea alisema licha ya Profesa Muhongo kujiuzulu kwa sababu ya kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow, anashangaa ni kwa nini amerudishwa bungeni akiwa waziri wa wizara ile ile.
 
Alisema mbali na Profesa Muhongo, mmoja wa mwenyekiti wa wa kamati ya Bunge lililopita aliyejiuzulu kwa sababu ya kashfa hiyo, sasa hivi ni Mwenyekiti wa Bunge.
 
Dk. Mwakyembe naye alikuwa na wakati mgumu baada ya baadhi ya wabunge wa upinzani kumtaka awajibishwe kwa kashfa ya mabehewa mabovu ambayo yalinunuliwa na serikali iliyopita.
 
Baadhi ya wabunge hao walionekana kumpania Dk. Mwakymbe tangu juzi ambapo kila wakichangia hoja ya mwongozo wa kuandaa mpango wa bajeti 2016/17, walikuwa wakimtaja kwa kuwa  aliyekuwa mrithi wake, Samuel Sitta, alibaini ubovu wa mabehewa hayo.
 
Mbunge wa Viti Maalum, Jessica Kishoa (Chadema) ambaye ni mke wa aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, alimtuhumu Dk Mwakyembe kuwa amehusika katika sakata la uingizaji wa mabehewa mambovu ambayo yameisababishia  serikali hasara ya mabilioni.
 
Aisema taifa  limeingia  hasara ya sh. bilioni 238 kwa kununua mabehewa mabovu na  aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi kipindi hicho yuko bungeni na ameshindwa kuwasilisha ripoti ya sakata hilo.
 
“Kazi iliyopo ni kupanga mipango ambayo haitekelezeki mpaka leo. Tunahitaji ripoti ya mabehewa ipo wapi haipatikani na Dk. Mwakyembe yupo hapa hili nalo ni jipu,” alisema.
 
LUKUVI, MWAKYEMBE WAJITETEA 
Kutokana na tuhuma hizo, mawaziri Lukuvi na Dk. Mwakyembe walikanusha kuhusika na kutaka wanaozisema wapeleke ushahidsi kama wanao.
 
Akijibu tuhuma hizo nje ya ukumbi wa Bunge, Lukuvi alisema hana kiwanja chochote alichopora na kusema hizo ni tuhuma za kupakaziwa.
 
Alisema mbunge huyo alilenga kuzungumzia viwanja vya Mabwepande ambavyo wakati vinatolewa hakuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam na hajawahi kufika huko hata siku moja.
 
“Kama anazungumzia kwa ujumla sina kiwanja hata kimoja nilichopora wakati nikiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Kama  ana ushahidi aulete,” alisema.
 
Kwa upande wake, Dk. Mwakyembe alisema mbunge huyo amesema uongo na serikali haijawahi kutumia  zaidi ya Sh. bilioni 60 kununua mabehewa na kwamba   mbunge huyo amelidanganya bunge na kumtaka atoe vithibitisho juu ya jambo hilo na akifanya hivyo atajiuzulu.
 
Dk. Mwakyembe aliomba ufafanuzi kuhusu utaratibu kwa Mwenyekiti wa Kikao hicho, Mary Mwanjelwa, ambapo alisema ni vyema watu wakaacha kugeuza bunge kama kijiwe cha kubishana kwa mambo yasiyo ya msingi.
 
Kauli hiyo ya Dk. Mwakyembe ilizua sintofahamu kwani kabla Mwenyekiti wa bunge kutoa nafasi Kishoa kutoa uthibitisho, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alitumia kifungu cha 63 (4) akisema kwa mujibu wa kifungu hicho anayepaswa kutoa uthibitisho ni Dk. Mwakyembe ambaye anamtuhumu mbunge huyo.
 
Kufuatia kauli hiyo ya Mdee, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, alilazimika kusimama na kusema ushahidi au uthibisho ambao Mdee amemtaka Dk. Mwakyembe atoe ameshaueleza na kusema serikali haijawahi kununua mabehewa ya zaidi ya Sh. bilioni 60.
 
Alisema aliyedanganya bunge ndiye anayetakiwa kuwasilisha uthibitisho kwa kuwa waziri ameshatoa ufafanuzi.
 
Dk. Mwanjelwa  alimtaka Kishoa kumpelekea uthibitisho ndani ya siku tatu kuhusiana na tuhuma hizo.
 
Kadhalika, Dk. Harrison Mwakyembe alilazimika tena kutoa ufafanuzi wa ununuzi wa mabehewa 274 ya Kampuni ya Reli  tanzania (TRL) baada ya Halima Mdee kudai kuwa ni mabovu.
 
Dk.  Mwakyembe alisimama na kutoa  ufafanuzi wa mabehewa hayo huku akisema yuko tayari hata kujiuzulu ubunge kama kashfa hiyo ni ya kweli. 
 
Katika kikao cha sita cha Bunge ambacho kiliongozwa na  Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga, Mdee alisema katika Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2011/12-2015/16, serikali ilipanga kukarabati reli ya kati kilomita 2,700 lakini hadi sasa zimekarabatiwa kilomita 150 tu.
 
Mdee alisema Mabehewa  ya Mwakyembe 274 ni feki kwa kuwa waliambiwa na Sitta na akaunda kamati  ili kuchunguza.
 
Hata hivyo, Mdee alikatishwa baada ya Dk. Mwakyembe kuomba kuhusu utaatibu ambapo alisimamia ili amweleze Mbunge huyo kuwa bungeni hakuna ubabe na kwamba akimwambia Mdee ampelekee mabehewa ambayo hayafanyi kazi.
 
"Kwenye  mikataba kuna kipengele kinaitwa ‘defect liability period' wewe ni msomi wa sheria unajua," alisema Mwakyembe ambaye pia alikatishwa  na wabunge wa upinzani waliotaka kutoa taarifa. 
 
Hata hivyo, Mdee aliposimama tena alimtaka  Dk. Mwakyembe aseme kama amevunja kanuni gani ili aijibu lakini  Dk. Mwakyembe alijibu kwa kuhoji kama wako kwenye kikao au vurugu kama Kariakoo.
 
"Halima sikiliza, kama ni ubabe kaufanye huko nje,” alisema Dk. Mwakyembe huku akisoma kanuni ya 63 (3) na (4).
 
Hata hivyo, Mwenyekiti wa bunge alisema bunge linaendeshwa kwa kanuni na sheria huku akiwataka watoa taarifa kufuata utaratibu.
 
Katika hatua nyingine,  Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alisema serikali isiwe na kigugumizi kuhusu kutaja kujenga reli ya kati na michepuko yake katika kiwango cha 'standard gauge' katika mpango huo.
 
Alisema ni vyema kutaja ili reli ya kati isiishie tu kwenye ukarabati  na kuishia kujenga  reli kutoka Tanzania hadi Rwanda.
 
"Mkiacha kutaja sehemu mnayoenda kujenga reli kwa kisingizio hamuwezi kutaja kila kitu wakati maeneo mengine mmetaja. Kama  mtakuja hapa bila mwelekeo wa reli ya kati nitakuwa mtu kwanza kusema rasimu ya mpango siikubali," alisema.
 
Alisema mpango huo ni mzuri isipokuwa unahitaji kutekelezeka  na wakiuacha, wataacha mapendekezo ya wabunge hautaweza kutekelezeka na itabaki hadithi na porojo.
 
Imeandaliwa na Freddy Azzah na Augusta Njoji
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa