Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema Awamu
ya Tatu ya mpango wa kusambaza umeme vijijini unaotekelezwa na Wakala wa
Umeme Vijijini (REA) hautaanza mpaka kukamilika kwa miradi ya awamu ya
pili na ya kwanza.
Alisema hayo bungeni juzi wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge
wa Mkalama, Allan Kiula (CCM) aliyetaka kufahamu lini vijiji vilivyo
katika jimbo lake vitapata umeme kutokana na miradi ya REA inayoendelea.
Profesa Muhongo alisema Februari 6 na 7, mwaka huu watafanya mkutano
wa tathmini ya miradi inayotekelezwa na REA awamu zote. “Tunataka kujua
makandarasi waliopo kazini, malipo waliyopewa kama yanalingana na kazi
wanazofanya na je kazi zinaendeleaje,” alisema.
Alisema baada ya mkutano huo akishirikiana na Naibu Waziri na
makatibu wakuu wa wizara hiyo watakwenda nchi nzima ili kuangalia kitu
gani kinachoendelea.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Makambako, Deo Sanga (CCM) alitaka
kufahamu lini miradi ya umeme itakamilika katika vijiji vya Mawande,
Utengule, Luhota, Ngamanga, Ikwata, Mlowa, Mkolonga, Ibumila, Mahongole,
Manga Usetule, Kifumbe, Mtanga, Kitandililo, Ibatu, Nyamande Mtulingala
na Mbugani.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard
Kalemani alisema Serikali imeweka mkandarasi Lucky Exports ambaye kwa
sasa anatekeleza mradi wa REA awamu ya pili mkoani Njombe.
Alisema kazi ya usanifu imekamilika kwa sasa na mkandarasi anasubiri
kusaini mkataba kati yake na REA kabla ya Machi, 2016 ili aanze
utekelezaji wa mradi katika vijiji vya Ikwete, Kifumbe, Luhota, Manga,
Mlowa, Mwande, Ngamanga, Usetule na Utengule.
Alisema kazi hiyo itachukua miezi sita na kuwaunganishia umeme wateja
wa awali 1,875, mpaka kukamilika kwake kazi hiyo itagharimu Sh bilioni
3.3 na vijiji vya Mahongole, Manga, Mbugani, Mtanga, Mtulingala na
Nyamande vimewekwa kwenye mradi awamu ya tatu.
CHANZO ; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment