Home » » ‘MSIZUNGUMZE MANENO AMBAYO HAYANA TIJA KWA TAIFA’

‘MSIZUNGUMZE MANENO AMBAYO HAYANA TIJA KWA TAIFA’

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji mstaafu Damian Lubuva amewataka wanasiasa walioshindwa katika uchaguzi mkuu uliopita wajipange kwa ajili ya uchaguzi ujao wa mwaka 2020 na si kuzungumza maneno ambayo hayana tija kwa taifa.

Alitoa kauli hiyo jana mjini hapa wakati akifungua mkutano wa tathimini wa asasi za kiraia kuhusu elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Uchaguzi umekwisha wanasiasa msiwapotoshe wananchi, walioshinda wameshinda na walioshindwa wameshindwa sasa tujipange kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020… wanaotoa hukumu kwenye uchaguzi ni wananchi wenyewe sio Tume wananchi kwa utashi wao huchagua wanayemtaka,” alisema.
Alisema katika uchaguzi mkuu uliopita Tume ya Uchaguzi haikuwa na chama wala haikupendelea chama chochote bali ilifanya kazi kwa kufuata kanuni na taratibu za nchi na kuongeza kuwa hakuna hata mgombea mmoja aliyekwenda tume kuonesha ushahidi kuwa aliibiwa kura.
Jaji Lubuva alisema kumekuwa na maneno kuwa tume inatakiwa ifukuzwe kutokana na kuonekana kukipendelea chama fulani.

Akitoa mfano alisema mwaka 2010 watu milioni 20 walijitokeza kujiandikisha lakini waliopiga kura ni milioni nane na pia mwaka 2015 jumla ya watu waliojiandikisha walikuwa milioni 22.5 lakini waliopiga kura ni milioni 15.5.
Jaji Lubuva alisema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kura zilizoharibika zilikuwa 227,889 sawa na asilimia 2.65 wakati katika uchaguzi mkuu mwaka 2015 kura zilizoharibika zilikuwa ni 402,248 sawa na asilimia 2.5, hali ambayo inaonesha watu wakielimishwa kura zinazoharibika zinapungua.

Mwenyekiti huyo wa tume alisema mwaka 2015 jumla ya asasi za kiraia zilizoomba kutoa elimu ya mpiga kura zilikuwa 551 lakini asasi zilizoruhusiwa kufanya hivyo zilikuwa 447.
CHANZO: GAZETI LA HABARI LEO

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa