Home » » SAKATA LA MABILIONI YA UINGEREZA LAIBUKA TENA BUNGENI.

SAKATA LA MABILIONI YA UINGEREZA LAIBUKA TENA BUNGENI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe.
Sakata la mabilioni ya Uingereza ambayo yaliisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 12, limeibuka tena bungeni.  
 
Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, ndiye aliyeibua sakata hilo jana na kutaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalumu kwenye mikopo ya zaidi ya Sh. trilioni sita ambayo serikali imekopa kwa mtindo wa kampuni kama ilivyoomba ule wa Benki ya Standard kupitia mshirika wake, benki ya Stanbic Tanzania.  
 
Akiuliza swali hilo, Zitto alisema kati ya mwaka 2011/2012 hadi mwaka huu, jumla ya fedha ambazo serikali ilikopa nje ya nchi kwa mfumo wa aina hiyo ni sh. tirioni 6.8.  
 
Alisema katika taarifa ya hukumu ambayo Naibu Waziri wa Fedha, Ashatu Kikaji, ameielezea inaonyesha kuwa na mtindo wa kutumia kampuni kwa ajili ya kupata mikopo umekuwa ukitumika na benki nyingi za kibiashara nchini. 
 
 “Je serikali haioni kwamba umefika wakati CAG kufanya ukaguzi maalumu wa mikopo yote ya kibiashara ambayo serikali imechukua kati ya mwaka 2011/212 na 2015/2016 ili kujua kama kulikuwa na aina za rushwa zilizokuwa zikifanyika?” aliuliza Zitto.  
 
Alisema katika hukumu ya Uingereza ilikuwa na lengo ya kuilinda benki ya Uingereza ambayo ndiyo ilitoa hongo kwa maofisa wa nchini ili kupata biashara.  Pia aliuliza: “Je, serikali haioni kwamba ni wakati muafaka sasa wa kufungua kesi dhidi ya benki hiyo ya Uingereza ili iwe fundisho kwa kampuni za nje zinazohonga ili kupata biashara katika nchi za Afrika?.  
 
Akijibu swali hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alisema CAG ana majukumu ya kikatiba kufanya hiyo kazi na anaweza kulitekeleza wakati wowote ili kujidhirisha kama mikopo hiyo imekuwa ikipatikana kwa namana ambayo inaifanya nchi kuingia kwenye hasara.  
 
Katika swali la pili la nyongeza, Masaju alisema kama Zitto ana taarifa zozote zinazoweza kuwasaidia kufungua shauri la madai au la jinai ashirikiane na vyombo husika na pale watakapoona lina sifa watafanya hivyo.  
 
Alisema kwa upande wa Tanzania tayari Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeitaka benki ya Stanbic iwe imeshalipa faini Sh. bilioni tatu ifikapo January 30, mwaka huu.  Kwa mujibu wa Masaju, serikali utaufanyia kazi ushauri wa Zitto kwa kuzingatia sheria za ndani ya nchi na uhusiano wa sheria katika jumuiya ya kimataifa.  
 
Katika swali la msingi, Zitto alihoji ni kwa nini serikali haichukui hatua kwa benki ya Stanbic ili ilipe faini zaidi.  Zitto alifafanua kuwa mwaka 2013 iliuza hati fungati ya thamani ya dola za Marekani milioni 600 (zaidi ya Sh. bilioni 1.2) kupitia benki ya Standard yenye tawi lake nchini, ambayo ni benki ya  Stanbic.  
 
Alisema shirika la Corruption Watch la Uingereza kwa kutumia vyanzo vyake, lilibaini kuwa hati fungani hiyo imeipa serikali ya Tanzania hasara ya ya dola milioni 80, sawa na Sh. bilioni 160 wakati serikali imelipwa faini ya dola milioni sita sawa na Sh. bilioni 12 tu.  Akijibu hilo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Ashatu Kijaji, alisema katika mashtaka yaliyofunguliwa na SFO dhidi ya benki ya Standard, kiasi kilichobainika ni dola milioni sita sawa na asilimia moja ya mkopo ambazo Tanzania haikupaswa kutozwa.  
 
Alisema tozo iliyotakiwa kulipwa kwa benki ya Standard ni asilimia 1.4 badala yake tozo iliyoingizwa kwenye mkataba ambayo ni asilimia 2.4 na ilithibitika kuwa tozo ni asilimia moja ya ziada haikuwa halali.  
 
“Katika hukumu iliyotolewa na mahakama huko Uingereza, benki ya Standard Group iliamuriwa kulipa faini ya dola milioni 32.2. 
 
Kati ya hizo kiasi cha dola milioni saba zinalipwa kwa serikali ya Tanzania ambazo ni dola milioni sita (Sh. bilioni 1.2) zikiwa ni fidia na dola milioni moja zikiwa ni riba,” alisema Ashatu.   
 
Alisema serikali imefuatilia taarifa ya hasara kwa serikali ya Tanzania ya dola milioni 80 iliyotajwa na Zitto na kwamba hawakupata usahihi wake.  
 
“Taarifa ya hasara ya dola za kimarekani milioni 80 imetajwa katika taarifa yenye kichwa cha habari ‘How Tanzania was short changed in Stanbic bribery payback’ iliyochapishwa na gazeti la The Guardian, likinukuu taarifa ya Corruption Watch ya Uingereza,” alisema Ashatu.  
 
Alisema taarifa hiyo haikutoa maelezo ya namna hasara ya dola milioni 80 ilivyopatikana kwa kuwa taarifa hiyo ilinukuliwa kutoka Corruption Watch pia haielezi hasara hiyo ilivyokokotolewa.  
 
Alisema kuwa serikali inamshauri Zitto kuwasilisha taarifa alizo nazo ili waiangalie kama ina vigezo vya kutosha kuisaidia serikali kujenga hoja ya madai ya hasara hiyo.  
 
Pia alisema BoT imeiandikia Benki ya Stanbic ya kusudio la kuitoza faini ya Sh. bilioni tatu kwa kosa la kufanya miamala inayokiuka sheria na kanuni za benki na taasisi za fedha.  
 
Aidha alisema sheria inaitaka benki ya Stanbic kutoa utetezi katika kipindi cha siku 20 ambazo zimeisha Jumamosi iliyopita. Alisema endapo BoT haitaridhika na utetezi wa Stanbic, italazimika kulipa faini hiyo.  
 
Novemba 30, mwaka jana, Mahakama ya Crown Southwark ya jijini London, Uingereza, iliamuru serikali ya Tanzania irejeshewe dola za milioni sita (sawa na Sh. bilioni 12.6) kutokana na kubainika kuwapo kwa udanganyifu baada ya kesi hiyo kufunguliwa kwenye mahakama ya kwamba asilimia moja ya mkopo huo ambayo ni dola milioni sita zililipwa kwa Kampuni ya EGMA.   
 
EGMA ni kampuni ya kitanzania iliyohusika katika uwezeshaji wa upatikanaji wa mkopo wa serikali wa Sh. trilioni 1.3 na inatuhumiwa kupokea kiasi cha Sh. bilioni 12 kama rushwa kwa kuwezesha upatikanaji wa mkopo huo.  
 
Wanaotuhumiwa katika sakata hilo ni mmiliki wa EGMA ambaye alikuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitillya; Ofisa Mkuu Mtendaji wa zamani wa Stanbic  Tanzania, Bashir Awale; aliyekuwa Mkuu wa Uwekezaji wa benki hiyo, Shose Sinare; baadhi ya vigogo wa serikali ya Tanzania na maofisa wa Benki ya Standard ya Uingereza.  
 
Kashfa yenyewe ilitokana na Benki ya Standard kukubali kuipokesha serikali ya Tanzania dola milioni 600 (Sh. trilioni 1.3) mwaka 2012 kwa masharti ya kulipwa riba ya asilimia 1.4, lakini Benki ya Stanbic Tanzania iliongeza asilimia moja, hivyo kufanya serikali kutakiwa kulipa riba ya asilimia 2.4.
 
Benki ya Stanbic iliyokuwa ikishughulikia suala hilo ikishirikiana na maofisa wa serikali ya Tanzania, ilidai nyongeza hiyo ilikuwa kwa ajili ya malipo kwa wakala, ambaye ni EGMA iliyopewa kazi ya kushauri mauzo ya hati fungani ingawa zilitumika kuhonga maofisa wa serikali.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa