Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SERIKALI imefunga ofisi ya kuuza madini ya tanzanite iliyopo London
nchini Uingereza ili kuhakikisha madini hayo yanauzwa nchini tu. Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema hayo jana wakati
akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu (CCM)
aliyetaka kufahamu mpango wa serikali katika kuhakikisha madini ya
tanzanite yanatambulika kama mali ya Tanzania.
Akijibu swali hilo, Waziri Muhongo alisema serikali itahakikisha
madini hayo yanauzwa nchini. “Hata London tumefunga ofisi, tunataka
madini hayo yauzwe hapa nchini tu,” alisema Profesa Muhongo.
Aidha, Mbunge wa Simanjiro, James Millya (Chadema) akiuliza swali la
nyongeza, alitaka kufahamu lini serikali itasaidia vijana waliojiingiza
kwenye uchimbaji madini kutokana na kunyanyasika na hatua gani
zinatumika kudhibiti soko la madini ya tanzanite.
Akijibu maswali hayo, Profesa Muhongo alisema si kweli kama serikali
haijawasaidia wachimbaji wadogo. “Serikali isingewathamini
wasingenichagua kuwa mlezi wao kitaifa,” alieleza.
Alisema Serikali imekuwa ikitoa ruzuku kwa vikundi ambapo kila
kikundi kilipewa Dola za Marekani 50,000 (Sh milioni 105) na ruzuku ya
jumla ni Dola za Marekani 100,000 (Sh milioni 210), na Shirika la Madini
la Taifa (STAMIC0) limeweka Idara kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Alisema utafiti umekuwa ukifanyika kabla ya kuwapatia wachimbaji
wadogo maeneo. Akijibu maswali ya msingi ya Millya, Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani alisema Serikali ya Tanzania
inawasaidia wafanyabiashara wa madini wakiwemo wa tanzanite kwa
kuwawekea mazingira mazuri ya kibiashara kwa kuhakikisha wanakuwa na
leseni halali ili wafanye biashara zao kiuhalali kwa kutumia mitaji yao
ya fedha na kulipa kodi stahiki kwa mujibu wa sheria.
CHANZO ; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment