Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
UJENZI wa Reli ya Kati ya kisasa umetawala mjadala bungeni huku
wabunge wengi wakiitaka serikali kuhakikisha bajeti ijayo, inakuja na
majibu juu ya hilo. Wabunge wengi waliochangia mpango wa Bajeti ya
Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 juzi na jana, walitaka serikali
ioneshe kwamba ujenzi huo utaanza mara moja katika mwaka ujao wa fedha.
Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndugulile (CCM) alihimiza serikali
kuweka kipaumbele cha ujenzi kwa ajili ya kuinua uchumi. Mbunge wa Viti
Maalumu, Mwanne Nchemba (CCM) pia alisisitiza akisema, “Serikali
isidharau kwa sababu reli ni tegemeo kubwa kwa wananchi na pia kwa
ubebaji wa mizigo.”
Akizungumzia gharama kubwa za ujenzi, Mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel
Nsazugwanko (CCM), alishauri serikali isiogope kukopa. “Hoja kwamba
hakuna fedha, hatutaki kuisikia badala yake serikali ije na mkakati wa
makusudi...bila kuwa na reli tunacheza ngoma,” alisema.
Nsazugwanko aliendelea kusema, “Waziri usipokuja na mkakati wa
kujenga Reli ya Kati, hatuwezi kuelewana bungeni.” Aliwataka wabunge
wote kusimama kidete juu ya suala hilo.
Alitoa mfano wa Kenya kwamba wameanza kujenga reli ya Mombasa kwenda
Kigali huku akisisitiza pia serikali ihakikishe inajenga reli pia kwenye
michepuko kuelekea maeneo yenye rasilimali, kama vile madini Burundi na
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Alisema bila kujenga Reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa, pia bandari
za Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma na Kalema zitadorora. “Tutashawishiana
wabunge wote tuombe uje tena... bila Reli ya Kati, hakuna viwanda,”
alisisitiza.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto alisisitiza umuhimu wa ujenzi wa
reli na kuitaka serikali kuwa makini kwenye siasa za kikanda kwa
kuhakikisha mtandao wa reli unakamilika. Alitaka pia wapate tafsiri ya
Reli ya Kati kwa maana ya matawi yake, na kuongeza kuwa mwaka jana
ilianzishwa kodi ya maendeleo ya reli ambayo kila mzigo unaoingia nchini
unatozwa asilimia 1.5 ya maendeleo ya reli.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba (CCM) alimtaka Waziri
mwenye dhamana ataje Reli ya Kati inayolengwa kujengwa, ihusishe matawi
ya Kaliua-Mpanda-Kalema; Uvinza- Msongati; Isaka-Keza. “Suala la reli ni
la kufa na kupona,” alisema.
Wakichangia maeneo mengine, Mbunge wa Kigamboni, Ndugulile alishauri
Bandari ya Dar es Salaam ipanuliwe na ifanye kazi kwa saa 24 huku
akisisitiza ushirikishaji wa sekta binafsi katika miradi ya maendeleo.
Kwa upande wa maji, alishauri kuwe na mpango kama wa Wakala wa Umeme
Vijijini (REA) kwa ajili ya kuwezesha huduma vijijini na uwepo mfuko kwa
ajili ya maji kama ilivyo kwa barabara.
Vile vile katika michango ya wabunge wengi, walishauri uanzishaji
viwanda uendane na jiografia ya maeneo husika sanjari na rasilimali
zinazopatikana. Kwa upande wa usafiri wa anga na ununuzi, Zitto alisema
serikali haiwezekani ikawa inanunua ndege kila wakati.
Alishauri taasisi na watu wanaonufaika na kuwepo kwa ATCL, ambazo ni
pamoja na TANAPA na Ngorongoro, ziruhusiwe kuwa na hisa kwenye shirika
hilo la ndege. Akizungumzia ahadi ya Sh milioni 50 kwa kila kijiji,
Zitto alishauri zitumike kutoa motisha wananchi wengi wajiunge na huduma
ya hifadhi ya jamii.
Aidha, Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema) alipinga
mapendekezo ya kutaka Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuwasilisha mapato
yao kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kwa kile alichosema kutaua
halmashauri.
CHANZO ; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment