Home » » WABUNGE CCM WAMBANA MAGUFULI.

WABUNGE CCM WAMBANA MAGUFULI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wakati serikali ya Rais Dk. John Magufuli ikipanga kuja na bajeti yake ya kwanza ya Sh. trilioni 22.99, baadhi ya wabunge CCM na wale wa upinzani wameunda Umoja wa Wabunge wa Reli (UWR), lengo likiwa kushinikiza reli ya kati ianze kujengwa kwenye bajeti hiyo.
 
Wabunge hao wametahadharisha kuwa iwapo bajeti hiyo haitaonyesha mpango wowote wa kuanza kwa ujenzi huo, watahakikisha wanaikwamisha.
 
Mwenyekiti wa umoja huo ni Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige (CCM) huku Katibu wake akiwa Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo).
 
Hatua ya wabunge hao imekuja ikiwa ni siku chache tangu wabunge wa upinzani wakwamishe mapendekezo ya mwelekeo wa mpango wa miaka mitano ya serikali ya Rais Magufuli kuwasilishwa bungeni.
 
Zitto alisema wanataka kwenye bajeti ijayo, serikali ionyeshe kuwa kuna fedha za kujenga reli kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) na kuunganisha Burundi (Musongati) na Tanzania kupitia Uvinza na mfumo mzima wa Reli kutoka Dar es Salaam - Kigoma/Mwanza na matawi ya Manyoni-Singida, Kaliua-Mpanda - Karema, Isaka-Keza (Ngara), Ruvu-Tanga/Moshi.
 
Baadhi ya wabunge waliomo kwenye umoja huo ni wale wa Dar es Salaam inapoanzia Reli ya Kati, Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Katavi na Kigoma.
 
Gharama za kujenga reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa ni dola za Marekani bilioni 7.6 (takriban Sh. trilioni 15).
 
Zitto jana aliliambia Nipashe kuwa sehemu ya fedha hizo zilitakiwa kutoka katika mkopo wa dola milioni 600 (takriban Sh. trilioni 1.28) ambao Tanzania ilikopa Benki ya Standard kupitia mshirika wake Stanbic Tanzania na baadaye kuibuka kuwa kashfa baada ya riba kuongezwa na serikali kupata hasara ya takriban Sh. bilioni 12.
 
Akitoa mchango wake bungeni, alisema serikali ianze kujenga mtandao wa reli yake ya ndani badala ya kung'ang'ania ile ya Afrika Mashariki.
 
Akizungumza nje ya viwanja vya Bunge, Mbunge wa Nzega, Hussen Bashe (CCM), ambaye ni mmoja wa wajumbe wa umoja huo, alisema kwenye mwongozo wa hotuba ya bajeti iliyowasilishwa bungeni juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ujenzi wa reli hiyo haumo.
 
“Wanataka kujenga reli ya kitu wanaita 'central corridor' ambacho wala hakitusaidii. Wanataka tu kujenga kwa shinikizo la EAC (Jumuiya ya Afrika Mashariki). Hii reli watakayojenga itasaidia sana Rwanda kuliko sisi,” alisema Bashe.
 
Alisema kwenye bajeti ijayo, wanataka waone mkandarasi kapatikana wa kuijenga reli hiyo na waambiwe ni lini ujenzi utaanza.
 
“Tutahakikisha bajeti hii haipiti na wakitulazimisha kuipitisha mimi. Nitashawishi wabunge wenzangu kwanza wa CCM tutoke nje ya bunge,” alisema Bashe.
 
Akichangia bungeni jana, alisema ni muhimu kwa reli hiyo kujengwa kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge).
 
Alisema reli hiyo ina umuhimu wake katika kuwasaidia wakazi wa mikoa hiyo lakini pia kwa nchi jirani kwani itaweza kuingizia Tanzania mapato kwa kusafirisha mizigo mbalimbali.
 
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba (CCM), alisema waziri lazima aeleze reli wanaijenga wapi kwenda wapi kwa sababu kwenye hotuba yake hakuna kitu alichosema.
 
Pia alisema utaratibu wa maduhuli yote kupelekwa katika mfuko mkuu wa serikali kutasababisha halmashauri na mashirika ya umma kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kukosa fedha.
 
Alisema uzoefu unaonyesha kuwa fedha zinapokusanywa na kupelekwa katika mfuko mkuu wa serikali zimekuwa zikichelewa kupelekwa katika maeneo mbalimbali.
 
‘’Mkifanya hivyo mtaua taasisi zetu hizi na tunaposema kugatua madaraka maana yake nini? Fedha zikienda katika mfuko mkuu wa serikali zimekuwa zikichelewa kurejeshwa katika maeneo mbalimbali, nawaomba wabunge wenzangu msikubali hili,’’ alisema.
 
Katibu wa UWR, Zitto, alisema baadhi ya wabunge wa upinzani ambao wako kwenye umoja huo ni pamoja na yule wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), John Heche (Tarime Vijijini- Chadema), Magdalena Sakaya (Kaliua-CUF) na Kasuku Bilago (Buyungu - Chadema).
 
Katika hotuba yake bungeni jana, Dk. Mpango alisema sura ya bajeti ya mwaka 2016/17, itakuwa ni jumla ya Sh. trilioni 22.99 mapato ya ndani yakiwa Sh. trilioni 15.8 sawa na asilimia 68.7 ikilinganishwa na asilimia 62.2 mwaka 2014/15.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa