Home » » RC apendekeza kuvunjwa halmashauri mbili

RC apendekeza kuvunjwa halmashauri mbili

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Chiku Galawa amependekeza kuvunjwa kwa halmashauri za Dodoma na Chamwino kutokana na maeneo hayo kuonekana kama hayana viongozi.
“Natamani kuona halmashauri za Dodoma na Chamwino zinavunjwa ili ziweze kuundwa upya kutokana na utendaji wa viongozi wake kwani inaonekana kama hakuna viongozi,” alisema.
Alisema hayo juzi mjini hapa wakati wa kikao cha kwanza cha Bodi ya barabara kwa mwaka 2015/2016 na kusema alichofanya ni kutoa mapendekezo na mamlaka husika itaangalia juu ya suala hilo.
Alisema mambo mengi katika maeneo hayo yamekuwa yakienda ndivyo sivyo licha ya kutoa maelekezo mbalimbali. Alisema kusuasua huko kwa utendaji kunaweza kuchukua muda mrefu kuwatoa wananchi hapo walipo katika kupiga hatua za kimaendeleo.
Alibainisha kuwa wameunda kikao kinachofanyika kila mwezi ili kutatua matatizo na kero mbalimbali za wananchi. Aidha alisema kuanzia sasa ni marufuku kuona mifugo inatembea katika maeneo ya mijini na hata vijijini kuwe na sehemu moja ya kukatisha mifugo.
“Mifugo inazurura ovyo tu mijini hakuna wa kuzuia kumekuwa kama hakuna viongozi,” alisema.
Alisema katika baadhi ya maeneo wananchi wamelima mpaka karibu na mifereji ya barabara hali ambayo kwa kiasi kikubwa inasababisha ng’ombe kupita kwenye barabara za lami kwa umbali mrefu na kutaka hifadhi za barabara zisitumiwe kwa ajili ya kilimo au uzoaji wa mchanga.
Aidha alisema nyumba zisizo na vyoo katika manispaa ya Dodoma ni asilimia 40 tu ambapo pia katika baadhi ya maeneo visima vimechimbwa karibu na vyoo hali ambayo inahatarisha afya za watumiaji wa maji kukumbwa na magonjwa ya mlipuko na hata kuhara.
“Uchafu umezagaa kila mahali kama hakuna halmashauri kila mtu anavunja sheria,” alisema.
Akizungumza wiki iliyopita katika ziara yake wilayani Chamwino, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Seleman Jaffo alitaka watendaji katika wilaya ya Chamwino kujitafakari upya kutokana na wilaya hiyo kuwa ya mwisho nchini kwa ukusanyaji wa mapato.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Sada Mwaruko wastani wa makusanyo ya mapato kwa mwezi ni katika halmashauri hiyo ni Sh milioni 17.
 Chanzo Habari leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa