Home » » RC azuia vyandarua kufugia kuku

RC azuia vyandarua kufugia kuku

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa amepiga marufuku vyandarua kufugia kuku, shughuli za bustani akisema watakaobainika kufanya hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Alisema hayo jana mjini hapa wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kuzungumzia masuala ya maendeleo na changamoto zilizopo, ikiwa ni pamoja na masuala ya usalama wa chakula, changamoto za sekta ya elimu na umasikini wa kipato.
Aidha watakaobainika wakiuza vyandarua vilivyotolewa na serikali kwa ajili ya kujikinga na malaria, watachukuliwa hatua.
Gallawa alisema katika maeneo mengi watu wamekuwa wakitumia vyandarua hivyo katika bustani na kufugia kuku, jambo ambalo halikubaliki. Ugawaji wa vyandarua ulianza Februari 7, mwaka huu, lengo likiwa ni kuhakikisha kaya zote 453,844 mkoani Dodoma zinafikiwa na kupewa vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu kwa asilimia 100.
Alisema jumla ya vyandarua 1,595,041 vilipangwa kugawiwa mkoani Dodoma na mpaka sasa ugawaji umefikia asilimia 96 ya lengo, maeneo machache yaliyosalia yalitakiwa kukamilisha ugawaji jana. Pia aliwataka wananchi kupuuza uvumi kuwa vyandarua hivyo vina dawa ya sumu inayoweza kuwaathiri.
Chanzo: Habari leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa