Home » » WAZIRI MHAGAMA AAGIZA IDARA YA MAAFA KUFANYA TATHIMINI YA MAAFA BAHI

WAZIRI MHAGAMA AAGIZA IDARA YA MAAFA KUFANYA TATHIMINI YA MAAFA BAHI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama ameiagiza Idara ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu kufanya tathimini ya hali halisi za athari zilizosababishwa na ndege aina ya kwerea kwerea katika mashamba ya mtama na uwele yaliyopo Mkoani Dodoma katika Wilaya Bahi.

Waziri Mhagama aliyasema hayo wakati wa Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria cha Kupitisha Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kilichofanyika jana katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kiliibua hoja za wajumbe ikiwemo hoja iliyo bainisha athari za maafa kwa wakazi wa Wilaya ya Bahi kuhusu ukosefu wa chakula baada ya mashamba yao kuvamiwa na ndege waharibifu aina ya Kwerea kwerea.

Hoja hiyo iliibuliwa na Mbunge wa Bahi Bw. Omar Badwel alisema wananchi wake wapo katika wakati mgumu hivyo wanahitaji msaada kutoka serikalini kwa kuwa mazao yao yamevamiwa na ndege hao.

 “Kwerea kwerea wamekuwa ni changamoto kwa wakazi wa wilaya yangu hususani maeneo ya Manyoni ninaomba serikali kupitia Idara ya Maafa isaidie kwa kuwapa chakula na mbegu Wananchi ili waweze kujikimu na kuitatua changamoto hiyo”Alisema Badwel.
“Mazao yaliyoshambuliwa na kuharibiwa na ndege aina ya kwerea kwerea ni mazao ya mtama na uwele, Alisisitiza”.

Waziri Mhagama alisema anatafuta uwezekano wa kuona umuhimu wa kushirikisha Wizara ya kilimo na Mifugo kwa kuangalia namna zinavyoweza kushirikiana kuondoa wadudu waharibifu wa mazao mkoani Dodoma.

“Serikali itafanya tathmini kwa waathirika hao wa maafa Wilayani Bahi, ni vizuri Idara ya Maafa ifanye hivyo haraka ili kusaidia kunusuru hali ya wakazi wa Dodoma”Alisisitiza Mhagama.
Waziri Mhagama alimpongeza Mhe.Badwel kwa kuwajali wananchi wa Bahi kwa kuibua jambo muhimu hivyo aliahidi kulitafutia ufumbuzi wa haraka.

“Suala hili ni muhimu kwa kuwa linagusa maisha ya Wananchi moja kwa moja sisi kama  serikali tumelichukua kwa uzito na tutahakikisha Idara ya maafa inatembelea maeneo husika kwa ajili ya kufanya  tathimini za haraka kwa waathirika waliopoteza mazao yao ili kujua namna tunavyoweza kutoa msaada wa haraka katika maeneo husika ” alisema Mhagama.

Awali; kikao hicho kililenga kupitia na kujadili bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu yenye fungu namba 25 (Ofisi Binafsi ya Mhe.Waziri Mkuu), 37(Sera, Uratibu a Bunge), 15 na 65 (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) na fungu 27 na 61 (Tume ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume ya Uchaguzi.


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa