Home » » Bunge laitaka Serikali kuharakisha ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge.

Bunge laitaka Serikali kuharakisha ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


 
Na Tiganya Vincent_MAELEZO-Dodoma.
 
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeshauri Serikali kuharakisha ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge ili kuisaidia Bandari ya Dar es salaam kukabiliana na ushindani kutoka bandari ya nchi jirani.
Hatua hii itasaidia kuleta maendeleo ya haraka hapa nchini kupitia upokeaji na usafirishaji wa  mizigo mingi ya nchini na nje ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Profesa Norman Sigala wakati akiwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano ya mwaka ujao wa fedha.
Amesema kuwa nchi nyingine za wanachama wa Afrika Mashariki zinaendelea kujenga reli kwa kiwango cha standard gauge kutoka Mombasa kupitia Nairobi , Kampala hadi Kigali kwa kasi kubwa.
Mhe. Profesa Norman alisema kuwa ili Bandari za Tanzania ziweze kushindana na Bandari za Kenya katika kupokea mizigo ya nchi za Uganda na Rwanda ni vema reli ya kati ikajengwa kwa kiwango cha standard gauge ili iziunganishe nchi hizo na reli inawezesha kusafirisha mizigo bila vikwazo.
Aliongeza kuwa kukamilika kwa reli kwa kiwango hicho itasaidia kuwanufaisha mikoa 15 ya Tanzania bara.
Profesa Norman alisema kuwa ni vema Serikali ikaharakisha ujenzi wa reli ya kati na matawi yake yote ambayo ni kutoka Dar salaam kwenda kigoma, Uvinza hadi Msongati kwa ajili ya mizigo ya Burundi.
Alisema kuwa tawi jingine ni lile la kutoka Tabora hadi Kalemi kwa ajili ya mizigo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) na ile ya kutoka Tabora kupitia Shinyanga hadi Mwanza kwa ajili ya Ukanda wa ziwa.
Kwa upande wa Msemaji wa Kambi Rasmi  ya Upinzani Bungeni Mhe. James Mbati akiwalisha maoni ya Kambi hiyo alisema kuwa reli ya kati ikiboreshwa itasaidia kutwala soko la usafirishaji wa abiria na mizigo ya ndani na nje ya nchi kama vile DRC, Burundi , Uganda na Rwanda.
Alisema kuwa hivi watanzania wanatakiwa kuwa na reli ambayo itaendana na ya sasa inayowezesha usafirishaji wa mizigo kwa kasi na uwezo mkubwa wa kubeba mzigo mzito.
Mhe. Mbati alishauri kuwa ili kufupisha ujenzi wa reli hiyo ni vema kukawa na wakandarasi ambao watapewa vipande vidogo vidogo vya takribani kilometa 200 ambavyo vitajengwa kwa wakati.
Naye Waziri wa Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbalawa alisema kuwa Serikali kupitia Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli(RAHACO) inaendelea na uboreshaji wa miundo mbinu ya reli ili kuongeza uwezo wa njia zilizopo za reli ya kati za kubeba mizigo mizito zaidi.
Alisema kuwa mara ya kukakamilisha kwa uboreshaji wa reli hiyo kutasaidia uhimilivu wa  mwendo kasi wa juu na kupunguza ajli za treni.
Wizara hiyo imeliomba Bunge kuidhinisha shilingi 4,895,279,317,500.00 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali katika mwaka wa fedha ujao.
Kati ya fedha hizo shilingi 2,212,141,496,500.00 ni kwa ajili ya sekta ya ujenzi, shilingi 2,587,333,762,000.00 ni kwa ajili ya sekta ya uchukuzi na shilingi 95, 804,059,000.00 ni kwa ajili ya sekta ya mawasiliano.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa