HALMASHAURI ya wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma imetakiwa kutenga
asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya akinamama na vijana na
kuhakikisha zinawafikia walengwa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mohamedi Utaly wakati
akizungumza na vikundi vya wajasiriamali kwenye kongamano la
wajasiriamali lililofanyika juzi katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu
Mpwapwa.
Utaly alisema halmashauri itenge asilimia 10 ya mapato yake ya ndani
kwa lengo la kupunguza na kuviwezesha vikundi vya akinamama na vijana
ili kujikwamua na umasikini wa kipato na kuwezesha vikundi hivyo
kumiliki mali.
Pia aliitaka halmashauri hiyo kutenga maeneo ya wajasiriamali hao,
kuzifanyia maonesho bidhaa wanazozalisha kwa kujitangaza zaidi kuinua
uchumi wao binafsi na uchumi wa wilaya nzima.
Katibu wa maandalizi wa kongamano hilo, Mary Luambano alisema lengo
la tamasha hilo ni kuviwesha vikundi vya akinamama na vijana kutumia
fursa zinazowazunguka kujipatia kipato na kuinua maisha ya kila siku na
jamii kwa ujumla lakini pia kuzitumia taasisi za kifedha katika
kujipatia mikopo yenye masharti nafuu.
Luambano alisema wajasiriamali wengi wamekuwa wakishindwa kufikia
malengo yao ya kuanzisha biashara kubwa kutokana na changamoto
zinazowakabili kwa kukosekana kwa mpango kamili wa uwekaji akiba, elimu
ndogo ya ujasiriamali na mazingira rafiki ya kufanyia biashara hizo.
Alisema kumekuwa na changamoto kubwa ya wajasiriamali wengi juu ya
mikopo wanayoipokea kutokuwa msaada kwao baadhi yao mikopo hiyo imekuwa
chanzo cha kuwarudisha nyuma na kufilisika kabisa kutokana na kutumia
fedha ya mkopo vibaya lakini riba kubwa zinazotozwa na tasisi za kifedha
kwa wajasiriamali.
Mwalimu wa vikundi vya ujasiriamali ambavyo vipo chini ya Mradi wa
Tunajali, Erasto Dyamaza alisema mpaka sasa vikundi vya hisa vina mtaji
wa kiasi cha Sh milioni 131.
Alisema kuna ulazima kwa serikali katika mipango yake izingatie
mahitaji muhimu ya kijinsia kama zinavyotaka sera na mikataba mbalimbali
ya kimataifa ikiwa katika malengo makuu ya kufanya maamuzi, udhibiti wa
rasilimali, uhakika wa kupata chakula, ukatili wa kijinsia na mirathi.
Chanzo Gazeti la Habari Leo
0 comments:
Post a Comment