Home » » MAKALA KUTOKA IDARA YA HABARI MAELEZO

MAKALA KUTOKA IDARA YA HABARI MAELEZO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Maadili ni Msingi wa Uwajibikaji katika Utumishi wa Umma
 
Anitha Jonas - MAELEZO
 
TANGU enzi za Azimio la Arusha, suala la maadili limekuwa likisisitizwa kama nguzo muhimu katika utoaji wa huduma kwa umma. Lengo lilikuwa ni kuhakakisha kwamba kila mtumishi wa Umma anatekeleza wajibu wake kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa.
 
Kutofanikiwa kwa Azimio la Arusha kulitokana na baadhi ya Viongozi kujua kwamba utekelezaji wa malengo ya azimio hilo ungekwamisha nia ovu waliyokuwanayo kama Watumishi wa Umma katika kuwahudumia Wananchi. Ndio maana juhudi ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere za kutaka azimio hilo liungwe mkono hazikuzaa matunda.
 
Pamoja na kuwepo sheria, kanuni, miongozo na mikakati ya kukuza maadili kwa watumishi wa Sekta ya Umma na watu binafsi, wananchi bado wamekuwa wakilalamika kuwepo urasimu usio wa lazima wenye lengo la kutengeneza mazingira ya rushwa na huduma zisizoridhisha. Aidha, wapo baadhi ya wafanyabishara binafsi wasiozingatia maadili na hata kufikia hatua ya kuchochea utoaji wa rushwa au kuzalisha bidhaa zisizo na viwango. 
 
 
Katika jitihada za kuhakikisha kwamba watumishi wa Umma wanakuwa waadilifu na wanafuata maadili mema, Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete ilibuni mikakati ya kuwa na utaratibu mpya kwa viongozi na watumishi wa Sekta za Umma na Binafsi kusaini Ahadi ya Uadilifu (integrity pledge).
 
Ahadi ya Uadilifu ni tamko rasmi na bayana la dhamira ya kuwa na mwenendo wa kimaadili na kuunga mkono kampeni ya kitaifa ya maadili na mapambano dhidi ya rushwa. Kwa kusaini tamko hilo, mhusika au taasisi inakuwa imejipambanua kwa Umma kuwa haitajiingiza katika masuala yasiyo ya kimaadili katika utoaji huduma na uendeshaji wa biashara.
 
Kwa mujibu wa Kamishina wa Maadili Jaji Salome Kaganda, kuna aina tatu za hati za Ahadi ya Uadilifu yaani; Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma, Watumishi wa Umma na Sekta binafsi ili kila kundi liwajibike kwa namna yake.
 
Akizindua Hati za Uadilifu mwezi agosti 2015, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema, kuwepo kwa Hati hizo ni hatua kubwa  muhimu na ya kihistoria katika safari ya kuboresha na kuhuisha mifumo ya uadilifu iliyopo ili iweze kwenda sambamba na mazingira na nyakati zilizopo.
 
Dkt. Kikwete hakusita kuelezea chimbuko la Hati ya Madili kwa kusema, “Kwa muda mrefu kumekuwepo na changamoto kubwa katika kupambana na rushwa kama moja ya tatizo kubwa la utovu wa uadilifu nchini.
 
Tumechukua hatua kadhaa ikiwemo kutengeneza Mkakati wa Mapambano Dhidi ya Rushwa na mabadiliko katika Sheria ambayo ilisaidia kuanzishwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Tumepata mafanikio makubwa na ya kutia moyo ingawa bado zipo changamoto na manung’uniko ambayo hatuwezi kuyapuuza.”
 
Dkt. Kikwete alifafanua kuwa, kwa madhumuni ya kuyaongezea mapambano haya nguvu na kasi, Serikali iliamua Mpango wa Mapambano dhidi ya Rushwa uingizwe katika Mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ili kutoa msukumo wa pekee katika utekelezaji wake.
 
Akielezea juu ya Mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Mkurugenzi Mtendaji wa BRN Bw. Omar Issa alisema kuwa Ahadi ya Uadilifu ni moja ya maeneo 12 yaliyo katika Mpango wa Mapambano dhidi ya Rushwa chini ya Mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa sasa (BRN).
 
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji huyo, matokeo ya utafiti uliofanywa katika kutekeleza mpango huo imeonekana kwamba moja ya changamoto iliyoonekana katika eneo la utoaji huduma na uendeshaji biashara nchini ni tatizo la rushwa na utovu wa maadili katika taasisi za umma na binafsi. Hivyo kulikuwa na haja ya kuweka mikakati ya uwajibikali na kufuata maadili katika utumishi wa Umma na Sekta binafsi.
 
Katika kuweka msisistizo wa suala la maadili na uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma, Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli ametoa agizo kwa watumishi wote wa umma kujaza Hati ya Ahadi ya Uadilifu (integrity pledge) ambayo imeeleza wazi masharti ya namna mtumishi wa Umma anavyopaswa kufanya kazi.
 
Lengo ni kusaidia kukuza maadili na mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa katika Sekta ya Umma na binafsi kwa kuwa ahadi au tamko hilo linashawishi viongozi, watumishi wa Umma na Makampuni binafsi kuwa tayari kufanya kazi kwa kufuata misingi ya maadili na kupambana na rushwa kwa hiari yao wenyewe.
 
Akiunga mkono juhudi za Dkt. Magufuli katika kusimamia nidhamu kwa Watumishi wa Umma, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema kwamba Hati ya Uadilifu (integrity pledge) itakuwa chachu ya harakati za kukuza uadilifu na mapambano dhidi ya rushwa nchini. “Ahadi ya uadilifu itaweka kauli thabiti ya kimaadili ambayo itaonyesha nia ya kutekeleza majukumu ya viongozi na watumishi wa  umma,” alisisitiza Balozi Sefue.
 
Alifafanua kuwa, ujazaji wa Hati hiyo hiyo utakuza utamaduni wa viongozi, watumishi wa Umma na Sekta binafsi kwa ujumla kuwa tayari kufanya kazi kwa kufuata misingi ya maadili na kupambana na rushwa kwa hiari yao.
 
 
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora Bi. Angela Kairuki amesema kwamba mtumishi wa umma anatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu na uadilifu bila kutoka nje ya mstari.
 
Mara baada ya kuapishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw Agrey Mwanri amesema atasimamia ipasavyo maadili ya utumishi wa Umma hususan katika kutekeleza miradi ya maendeleo katika mkoa wake huku akiahidi kuwawajibisha watumishi watakaokiuka maadili ya utumishi wa umma.
 
Tangu achaguliwe kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe Magufuli amewachukulia hatua baadhi ya viongozi wa Umma kwa kushindwa kusimamia utekelezaji wa majukumu waliyopewa. Viongozi hao ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dkt. Shaaban Mwinjaka, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mapato, Mkurugenzi wa Vitambulisho vya Taifa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Dkt.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa