Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko, Dodoma.
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi
amepiga marufuku ununuzi wa mashamba, unaofanywa na kampuni binafsi na
kuyapima kuwa viwanja. Akihitimisha mjadala wa hotuba ya bajeti ya
wizara hiyo, Lukuvi alisema atakayenunua shamba, anapaswa kuhakikisha
linabaki hivyo na kama anataka liwe viwanja, ni vema akakabidhi
halmashauri libadilishwe matumizi.
“Kama kuna mtu binafsi amenunua mashamba kwa lengo la kupima viwanja
imekula kwako kabidhi halmashauri itapanga, kupima na kumilikisha
wenyewe kwani kuna watu wanakuja na brief case zao na kutajirika kwa
kupima viwanja,” alisema Lukuvi.
Lukuvi aliagiza halmashauri kutofikiri ardhi ni kwa ajili ya
kujitajirisha pekee na kusisitiza kuwa kuanzia sasa hati za viwanja
zitatolewa baada ya mwezi mmoja badala ya ilivyokuwa awali miaka miwili.
Akizungumzia ujenzi holela, alisema awali serikali ilikuwa na jukumu
la kupima na upangaji pekee yake, lakini hawakufanya vya kutosha jambo
lililosababisha wananchi kuwatangulia na kujenga.
Kuhusu utoaji hati, alisema ofisini kwake kuna hati zaidi ya 4, 800
za watu waliokuwa hawajachukua wakiwemo walio nje ya nchi. Alisema
mlundikano huo wa hati, unatokana na hisia za wamiliki kudhani
zingechukua muda mrefu.
Alisisitiza wahusika waende kuzichukua. na kuwataka kwenda kuchukua.
Lukuvi alisema kuanzia sasa utoaji hati utaishia wilayani baada ya
kugawa mamlaka kwenye kanda kanda nane ambako yuko msajili atakayesaini.
Alisema vifaa vipo kwenye kanda. Aidha, alisema wameanzisha programu
ya kupima na kupanga ardhi kwa kushirikiana na sekta binafsi kwa
kuanzisha kampuni 58 za kupanga na kupima zilizosajiliwa.
Alisema kampuni binafsi zitapima na kupanga, lakini uamuzi wa mwisho
utakuwa wa halmashauri. Akizungumzia suala la fidia, Waziri alisema lipo
kisheria ikiwa eneo limechukuliwa kwa maendeleo au huduma.
Alitaka wananchi waliochukuliwa maeneo hayo, kutokuwa na wasiwasi na
alisisitiza ni sawa na wameweka fedha benki kwa kuwa wakicheleweshewa
fidia, watalipwa na riba.
Akizungumzia migogoro ya ardhi, alisema wizara yake imejipanga
kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Kilimo na kufikia mipaka ya
kijiji na kijiji, wakiwa na wataalamu na kufanya marekebisho ya mipaka
ikibidi.
Chanzo Gazetila Habari Leo
Chanzo Gazetila Habari Leo
0 comments:
Post a Comment