SERIKALI imeamua kufufua mashamba yote ya kilimo na mifugo nchini.
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mwigulu Nchemba amesema kwa
kuanzia, wiki ijayo maofisa wa Benki ya Kilimo Tanzania watatembelea
shamba la mifugo la Kitulo, Makete.
Hatua hiyo inatokana baada ya kuonana na Mkuu wa Wilaya ya Makete, Daud Yassin aliyekumbushia ahadi ya kufufua shamba hilo.
Mwigulu alisema hayo bungeni wakati akijibu swali la nyongeza la
Mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwanko (CCM) aliyehoji sababu za
kituo cha kuzalisha mbegu cha Bugaga kutelekezwa.
Kwa mujibu wa Mwigulu, serikali itafufua mashamba yote na imekuwa
katika maandalizi tofauti kuhakikisha mashamba hayo yanafufuka.
“Nia ya serikali ni kuhakikisha kuwa mashamba yote ya mifugo na
kilimo yanafufuka. Tunafanya maandalizi kwa kila eneo husika.
Tutahakikisha tunafanya utaratibu wa kuyafufua ili kusaidia vijana
katika kilimo na masoko,” alieleza Mwigulu.
Katika majibu yake kuhusu shamba la mbegu la Bugaga, Naibu Waziri wa
Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha alisema limekaa kwa muda
mrefu bila ya kuzalisha kutokana na ufinyu wa fedha, limepangwa
kufufuliwa katika mwaka 2016/17 lizalishe mbegu kwa wingi.
Hivi karibuni, Waziri Mwigulu alikutana na Mkuu wa Wilaya ya Makete
aliyefika mjini hapa kuonana naye ili kukumbushia ahadi yake ya Machi
mwaka huu alipotembelea shamba la Kitulo na kuahidi serikali italifufua
shamba hilo.
Chanzo Kutoka Habari Leo
0 comments:
Post a Comment