Home » » Serikali kuwaunga mkono Wananchi wa Busiri katika uchimbaji madini.

Serikali kuwaunga mkono Wananchi wa Busiri katika uchimbaji madini.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. Na Benedict Liwenga, MAELEZO, Dodoma.

Serikali imewaunga mkono Wachimbaji Wadogo wa Madini wa Busiri kwa kuwatafutia maeneo ya uchimbaji wa madini, ambapo Wizara ya Nishati na Madini imetenga eneo lenye ukubwa wa hekta 11,031 lililokuwa chini ya Leseni za Utafutaji namba PL 3220/2005 ambayo ilikuwa ikimilikiwa na Bw. Daudi Mbaga pamoja na PL 5853/2009 iliyokuwa ikimilikiwa na na Meru Minerals Resources Limited ambazo zilizoisha muda wake.

Hayo yamesemwa leo Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri, Wizara ya Nishati na Madini, Mhe. Medard Kalemani wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi kuhusu mikakati ya Serikali ya kuwaunga mkono Wachimbaji wadogo wadogo wa Busiri.

Mhe. Kalemani ameeleza kuwa, hadi mwishoni mwa mwezi Machi, 2016, Wizara yake imegawa kwa wananchi wa Busiri leseni 81 za Uchimbaji Mdogo wa Madini (PMLs) katika eneo hilo, sawa na takribani hekta 810 kati ya hekta 11,031 za eneo lililoachwa kwa ajili ya Wachimbaji Wadogo.

“Wizara imegawa leseni nyingine 30 za uchimbaji mdogo (PMLs) katika eneo lililopo katika kijiji cha Kuntakama takribani kilomita moja eneo la uchimbaji mdogo wa madini la Busiri”, alisema, Mhe. Kalemani.

Ameongeza kuwa, mkakati mwingine wa Serikali ni kuendelea kulitumia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kutoa huduma ya ugani kwa wachimbaji madini wadogo wa kijiji cha Busiri na wengine wote nchini ikiwemo kutoa ruzuku kupitia Mfuko wa Wachimbaji Wadogo.

“STAMICO pia itaendelea kuwapa elimu wachimbaji wadogo na kuwahamasisha kuunda Vikundi vya Uchimbaji ili waweze kusaidiwa kwa pamoja”, alisema Mhe. Kalemani.

Aidha, Serikali imekuwa ikiwatembelea wachimbaji madini wa eneo tajwa mara kwa mara kwa kutumia Maafisa na Wataalamu wa Ofisi ya Kanda ya Ziwa Viktoria Magharibi na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi-Bukoba.

Amefafanua kuwa, tarehe 11 Machi, 2016 Afisa Madini Mkazi wa Bukoba alifika na kufanya mkutano na kikundi cha Busiri Mining Co-operative Society Limited chenye Leseni Na. PML 001712WLZ.

“Ili kutekeleza ombi la sasa la Mheshimiwa Mbunge, Wizara yangu itamtuma Afisa Madini wa Kanda ili awatembelee tena na kuwaelimisha juu ya fursa zilizopo za kuendeleza wachimbaji wadogo ili uchimbaji uwe wenye tija na kutoa ajira na kuondoa umaskini kupitia uchimbaji wa madini”, aliongeza, Mhe. Kalemani.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa