Na.Aron Msigwa - MAELEZO
Serikali imesema kuwa inaendelea na utaratibu wa kuzitambua na
kuzirasimisha bandari Bubu zote zilizokidhi vigezo ambazo zinatumiwa na
wafanyabiashara kupitisha bidhaa mbalimbali ili ziweze kuchangia katika
Pato la Taifa kulingana na wingi wa bidhaa zinazopitishwa katika
bandari hizo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin
Ngonyani ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma leo wakati akijibu
maswali ya Wabunge waliotaka kujua mkakati wa Serikali katika kudhibiti
bidhaa zinazoingizwa nchini na wafanyabiashara wasio waaminifu kupitia
bandari bubu hali inayoikosesha serikali mapato.
Mhe. Ngonyani amekiri kuwepo kwa ongezeko la wafanyabiashara wasio
waaminifu wanaotumia bandari hizo katika maeneo mbalimbali nchini hasa
ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi, Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria na
maeneo ya mipakani ambayo yanaingia moja kwa moja kwenye makazi ya watu
akieleza kuwa wengi wa wafanyabiashara wanakwepa kodi na kutafuta
urahisi wa kupitisha mizigo yao.
Amesema maeneo hayo yamekuwa chanzo kikubwa cha upitishaji wa
bidhaa zisizokidhi viwango, Silaha na Biashara haramu na kubainisha kuwa
baadhi ya wafanyabiashara wa ndani wasio waaminifu wamekuwa
wakishirikiana na raia wa kigeni kuagiza na kuingiza bidhaa hizo kupitia
bandari hizo kwa lengo la kukwepa kodi.
Amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya tano inalishughulikia kwa
nguvu zote suala hilo kupitia watendaji wake wakiwemo wakuu wa mikoa wa
maeneo husika ambao hushirikiana na mamlaka zinazohusika vikiwemo vyombo
vya ulinzi na usalama kudhibiti njia na maeneo yote yanayotumiwa na
wafanyabiashara hao.
" Kama Serikali tunaendelea kufanya vikao kwa kushirikiana na wakuu
wa mikoa na mamlaka zinazohusika kuangalia namna ya kurasimisha bandari
bubu zilizobaki ili tuweze kukusanya mapato ya Serikali yaliyokuwa
yakipotea kutokana na wingi wa mizigo inayopitishwa" Amesema Mhandisi
Ngonyani.
Amefafanua kuwa mwaka katika kipindi cha mwaka 2015 na mwezi
Januari, 2016, doria zilizofanyika katika maeneo yanayotumiwa na
wafanyabishara hao zilifanikisha kukamatwa kwa wafanyabiashara 98 ambao
wote walichukuliwa hatua za kisheria ikiwem mali zao kutaifishwa pamoja
na kuwafikisha mahakamani.
Kuhusu bandari bubu zilizotambuliwa na kuzirasimishwa na Serikali
katika Pwani ya Bahari ya Hindi ni Mbweni ya jijini Dar es salaam,
Mlingotini mkoani Pwani, Kisiju na Nyamisati mkoa wa Pwani na Bandari
bubu ya Kilambo mkoani Mtwara.
Aidha, amesema Serikali inaendelea na utaratibu wa kurasimisha
bandari binafsi umefanyika katika ziwa Victoria mkoani Mwanza na maeneo
mengine ambayo serikali inaendelea kuyafanyia kazi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad
Masauni amesema kuwa Serikali inaendelea kuvijengengea uwezo vikosi
vyake vya ulinzi na usalama kwa kuviongezea vifaa vya kisasa ili viweze
kuimarisha doria nchi nzima ili kukabiliana na vitendo vyote vya
uvunjaji wa sheria.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na wananchi
kukusanya taarifa za kiharifu ili kuwabaini na kuwakamata wafanyabishara
wote wanaojihusisha na uagizaji na uingizaji wa bidhaa kupitia bandari
bubu ambaoumekua ukiisababishia serikali ikose mapato.
" Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinaendelea kukusanya taarifa
za kiharifu kutoka kwa wananchi ili kukabiliana na wimbi hili, pia
tunaendelea kuviongezea nguvu vikosi vyetu vya ulinzi na usalama ili
viweze kutimiza majukumu yao ipasavyo" Amesisitiza Mhe.Masauni.
0 comments:
Post a Comment