Home » » Serikali za Vijiji zakumbushwa kusimamia Sheria ya Ardhi.

Serikali za Vijiji zakumbushwa kusimamia Sheria ya Ardhi.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Na Benedict Liwenga, MAELEZO, Dodoma.

SERIKALI za Vijiji nchini zimekumbushwa kusimamia vizuri Sheria ya Ardhi Na. 5 ya mwaka 1999 ambayo imeweka utaratibu wa kufuata kwa mtu anayehitaji kupata ardhi kwa matumizi mbalimbali.

Agizo hilo limetolewa leo Bungeni Dodoma na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani Jafo wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Chemba, Mhe. Juma Nkamia ambaye alitaka kujua utayari wa Serikali wa kufuta uamuzi uliotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara wa kuwazuia wakulima ili kuondoa mgogoro wa muda mrefu.

Mhe. Jafo ameeleza kuwa, tamko lililotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara liliwahusu wakulima waliokuwa wavamizi katika eneo la hifadhi ya Wanyamapori ya Makame kutoka katika Wilaya za Kiteto, Babati, Chemba, Kondoa na Mkoa wa Iringa waliokuwa wanaendesha shughuli za kilimoi katioka hifadhi hiyo kinyume cha Sheria.

Amefafanua kuwa, uamuzi huo ulitolewa kufuatia azimio la kikao cha pamoja cha Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya za Kiteto cha Chemba kilichokaa tarehe 12 Novemba, 2015.

“Kikao hicho kilishirikisha viongozi wa Vijiji vitano vinavyounda Mamlaka ya Hifadhi (WMA) ambavyo ni Ngobolo, Katikati, Ndedo, Irkiushbor na Makame pamoja na wawakilishi wa wakulima 10 kutoka kila Wilaya”, alisema Mhe. Jafo.

Aidha, kwa mujibu wa Sheria, hairuhusu shughuli yoyote ya kibinadamu ikiwemo kilimo, ufugaji au makazi kuendeshwa katika hifadhi.

“Naomba kutoa wito kwa wananchi kuzingatia Sheria za nchi ili kuepuka migogoro katika jamii, Serikali za vijiji zinakumbushwa kusimamia vizuri Sheria ya Ardhi Na. 5 ya mwaka 1999 ambayo imeweka utaratibu wa kufuata kwa mtu anayehitaji kupata ardhi kwa matumizi mbalimbali, lengo ni kuzuia migogoro ya ardhi isiyokuwa ya lazima ambayo kwa sehemu kubwa inatokana na kutozingatiwa kwa Sheria za ardhi”, alisema Mhe. Jafo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa