Na Fatma Salum- MAELEZO, Dodoma.
Serikali
imebainisha kuwa Sheria Mpya ya Ushirika (Sheria namba 6 ya mwaka 2013)
imesaidia kupunguza changamoto za wanachama wa Vyama vya Ushirika
pamoja na wakulima wa Tumbaku nchini.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mhe.
Tate William Ole-Nasha aliyasema hayo leo bungeni Mjini Dodoma wakati
akijibu maswali ya wabunge kwenye kipindi cha maswali na majibu.
Mhe.
Ole-Nasha alisema kuwa baadhi ya marekebisho ya Sheria hiyo
yanayowanufaisha wanachama wa Vyama vya Ushirika wakiwemo wakulima wa
tumbaku ni pamoja na kuwachukulia hatua viongozi wabadhirifu wa vyama
hivyo.
“ Katika maeneo yanayolima tumbaku viongozi wabadhirifu wa Vyama vya Ushirika 26 Mkoani Ruvuma wakiwemo Maafisa Ushirika wawili wamesimamishwa kazi na kufikishwa mahakamani.” alisema Ole-Nasha.
Pia
Mhe. Ole-Nasha alifafanua kuwa sheria ya sasa inakataza vyama kukopa
zaidi ya asilimia 30 ya mali zake (Own Capital) ili kuzuia vyama hivyo
kuingia kwenye madeni makubwa yasiyolipika na hatimaye kusababisha migogoro ndani ya vyama.
Akizungumzia
mafanikio upande wa tozo, Ole-Nasha lisema kuwa kuanzia sasa Mkutano
Mkuu utakuwa chini ya uenyekiti huru utakaochaguliwa na wajumbe wa
mkutano huo kinyume na awali ambapo Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku ndiye
aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu.
“Lengo
ni kulinda maslahi ya wakulima ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa tozo
zote zinazoidhinishwa na Mkutano Mkuu zinakuwa na maslahi kwa wakulima
wa Tumbaku.” Aliongeza Ole-Nasha.
Kwa
mujibu wa Ole-Nasha Serikali inatambua uwepo wa kodi nyingi na tozo
kwenye mazao mbalimbali ya chakula na biashara hivyo kwa kushirikiana na
wadau imedhamiria kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara katika sekta
ya kilimo kwa kupitia upya taratibu, vibali, tozo, kodi, ushuru na ada
nyingine zinazotozwa ili kutoa nafuu kwa wakulima.
0 comments:
Post a Comment